Simba walioingiza kikosi chao cha pili kwenye michuano hiyo, kinachonolewa na Kocha Suleiman Abdallah Matola, ilipata mabao yote yote kupitia kwa kiungo chipukizi anayeinukia vema katika soka ya Tanzania, Christopher Edward kipindi cha pili.
Christopher ambaye hukomazwa pia kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kikosi cha kwanza cha Simba, alifunga bao la kwanza penalti dakika ya 50, baada ya beki Miraj Adam kuangushwa kwenye eneo la hatari.
Edward ambaye ni kipenzi cha kocha Mserbia wa Simba, Profesa Milovan Cirkovick, alifunga bao la pili dakika ya 55 baada ya kuwapiga chenga mabeki watatu wa Zimamoto kabla ya kumchambua kipa wa timu hiyo ya Zanzibar.
Pamoja na Simba SC kuwania ubingwa wa michuano hiyo, lakini sasa Christopher ameingia kwenye mbio za kiatu cha dhahabu cha michuano hiyo, kwa kufikisha mabao manne, akiwa anaongoza.
Katika michezo mingine ya kuhitimisha hatua ya makundi ya michuano hiyo, Uwanja wa Chamazi, Jamhuri FC iliichapa 4-0 Mtende, zote za Zanzibar mabao ya washindi yakifungwa na Sadik Rajab dakika ya 20, 44, Issa Achimwene aliyejifunga dakika ya 82 na Suleiman Khatib dakika ya 88.
Kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Azam FC ilitoka nyuma kwa bao 1-0 na kuifunga Polisi Moro FC mabao 2-1, mabao yake yakitiwa kimiani na beki Said Mourad dakika ya 20 na Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 70, wakati la Maafande wa Morogoro lilitiwa kimiani na Mokili Rambo dakika ya kwanza. Polisi ilimpoteza mchezaji wake, Abdallah Rajab dakika ya 88 aliyetolewa nje kwa kadi nyekundu.
CHANZO CHA HABARI: BIN ZUBEIRY
No comments:
Post a Comment