LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Desmond Elliot amesema alijitokeza kuwa kipenzi cha mama yake baada ya kumpelekea pesa kutokana na ujira aliolipwa kwa kazi ya kucheza filamu.
Elliot ameueleza mtandao wa naijerules wiki hii kuwa, mama yake huyo aliona fahari kubwa kutokana na kazi yake hiyo na tangu wakati huo, akawa kipenzi chake kikubwa.
Msanii huyo mwenye sura yenye mvuto alisema, mama yake alipatwa na kiwewe cha furaha siku alipomuona kwa mara ya kwanza kwenye filamu ya Kinigeria.
"Alipokuwa hanioni katika filamu nilizoshiriki kuzicheza, alikuwa akilalamika sana kwa sababu siku zote nilikuwa nikitoka nyumbani asubuhi na kurudi usiku,"alisema.
"Kwa mara ya kwanza aliniona katika filamu ya Suitors, ambayo nilicheza sehemu ya muhusika wa kawaida. Alipatwa na kiwewe cha furaha," aliongeza msanii huyo.
Pamoja na kufurahishwa na kazi yake hiyo, Elliot alisema mama yake hakuwa mtu wa kudekeza watoto wake na kuongeza kuwa, kuna wakati aliwahi kumfikisha polisi.
"Baada ya kunifikisha polisi, alimweleza ofisa wa zamu kumsaidia kunifundisha nidhamu na kunipiga. Aliwahi kufanya hivyo mara mbili," alisema Elliot.
Elliot ni baba wa watoto wanne, akiwa amezaa mapacha mara mbili. Alisema wazazi wake hawana historia ya kuzaa watoto mapacha, lakini hilo lipo katika familia ya mkewe.
"Nilipopata mapacha kwa mara ya kwanza, nilifurahi na kumshukuru Mungu. Lakini mara ya pili, sikuwepo nchini, nilikuwa nje ya nchi. Mke wangu aliponipigia simu kunijulisha, sikuamini. Aliponiuliza kwa nini, nilimweleza sikutarajia," alisema.
Elliot alisema bado anahitaji kupata watoto wengine watatu zaidi. Alisema lengo lake ni kuwa na watoto saba.
Mcheza filamu huyo alisema amejipanga vyema kuhakikisha anawalea vyema watoto hao ikiwa ni pamoja na kuwapatia elimu nzuri kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
Elliot alisema anapenda sana watoto na kwamba baadhi ya wakati anapokuwa nyumbani, huwa akiwaogesha badala ya kazi hiyo kufanywa na mkewe.
No comments:
Post a Comment