KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 29, 2012

WOLPER SASA KUTENGENEZA FILAMU ZAKE



BAADA ya kucheza filamu za wasanii wenzake kwa muda mrefu, hatimaye mwanadada Jacqueline Wolper ameamua kuanzia sasa kuandaa filamu zake mwenyewe.
Mtandao wa filamucentral ulimkariri Wolper akisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, ataandaa filamu hizo kupitia kampuni ya JB Production.
Msanii huyo mwenye umbo na sura jamali alisema, atafanyakazi hiyo kwa kushirikiana na meneja wake, Leah Mwendamseke ‘Lamata’.
Wolper alisema tayari ameshaanza kuandaa filamu yake ya kwanza itakayojulikana kwa jina la Malipo.
Mwanadada huyo alisema ameamua kujitosa kwenye fani hiyo kwa lengo la kuongeza ujuzi na kipato.
Alisema ana hakika filamu yake hiyo mpya itawasisimua mashabiki kutokana na mvuto wa hadithi na waigizaji, ambao alisema wameigiza kwa kiwango cha juu.
“Mara nyingi ninapopanga kufanya kitu fulani, lazima nihakikishe nakimaliza kwa asilimia mia moja,” alisema msanii huyo mwenye mvuto.
Aliongeza:” Kwa vile nimeingia mzigoni kwa dhamira moja, nawaomba mashabiki wajiandae kushuhudia maajabu kutoka katika kampuni yangu mpya ya kutengeneza filamu.”
Aliwataja baadhi ya wasanii walioshiriki kucheza filamu yake hiyo mpya kuwa ni Blandina Chagula ‘Johari’, Stanley Msungu ‘Seneta’, Hashim Kambi ‘Ramsey’, Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’, Ahmed Ulotu ‘Mzee Chilo’.
Wolper alisema tangu alipojitosa kwenye fani hiyo, watayarishaji na waongozaji wa filamu wamekuwa wakimkubali kutokana na uwezo wake mkubwa katika uigizaji.
Msanii huyo aliendelea kutetea msimamo wake kuhusu mavazi wanayotumia wasanii wa kike kwenye filamu kwamba hayana matatizo.
Alisema mara nyingi mavazi yanategemea sehemu husika hata kama mtu akiwa nyota, huwezi kwenda kanisani na kimini.
“Sehemu ambazo hazistahili kwa mavazi yaliyo tofauti, unatakiwa kuvaa vazi linalostahili na inafikia mahali lawama inawaangukia sana wasanii wakionekana kama ndivyo wavaavyo,”alisema.
Wolper alisema ni vigumu kwa mtu kwenda katika maonyesho ya muziki wa disco akiwa amevaa mavazi yasiyoendana na sehemu hiyo.
Hivi karibuni, Wolper alibadili dini na kuitwa Ilham baada ya kupata mchumba muislam aliyemtaja kwa jina la Dulla ‘Dallas’, ambaye alimnunulia gari sambamba na kumboreshea maisha.
Wolper ni mmoja wa wasanii wanaomiliki magari ya kifahari. Anamiliki magari mawili, Toyota Harrier Lexus lenye thamani ya sh. milioni 25 na Toyota Noah lenye thamani ya sh. milioni 18, ambalo analitumia kwenye kazi za filamu.

No comments:

Post a Comment