KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 16, 2012

BAYI: SIJIUZULU NG'O

KATIBU Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi amesema kamwe hawezi kujiuzulu kutokana na kuvurunda kwa Tanzania katika Michezo ya Olimpiki.
Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, Bayi alisema wanaopaswa kulaumiwa kutokana na kuvurunda huko ni viongozi wa vyama vya michezo.
Bayi alisema kamati yake haipaswi kubebeshwa lawama kwa vile siyo inayowaandaa wanamichezo kwa ajili ya kushiriki katika michezo hiyo.
Alisema jukumu la kuwaandaa wanamichezo ni la vyama husika, hivyo ndivyo vinavyopaswa kubebeshwa lawama kwa vile havikuwaandaa kiushindani.
Katibu Mkuu huyo wa TOC alisema jukumu la kamati yake lilikuwa kuwaweka kambini wanamichezo wote mwezi mmoja kabla ya kushiriki kwenye michezo hiyo.
“Watu wengi wanadhani TOC ndiyo inayopaswa kuziandaa timu, hii si kweli hata kidogo. Jukumu hilo ni la vyama husika, sisi tunawaweka wachezaji kambini mwezi mmoja wa mwisho,”alisema.
Katika michezo hiyo iliyomalizika hivi karibuni mjini London, Uingereza, Tanzania ilirudi mikono mitupu baada ya wanamichezo wake saba kushindwa kuambulia medali.
Tanzania ilishiriki katika michezo ya ngumi za ridhaa, kuogelea na riadha.
Kuvurunda kwa Tanzania katika michezo hiyo kuliwafanya wanamichezo wengi wawatake viongozi wa TOC, akiwemo Bayi wajiuzulu.

No comments:

Post a Comment