KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 16, 2012

TFF, VODACOM HAKIJAELEWEKA

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) bado halijaingia mkataba mpya wa udhamini wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati yake na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom.
Uchunguzi uliofanywa na blogu ya liwazozito umebaini kuwa, pande hizo mbili bado hazijafikia makubaliano kuhusu marekebisho ya mkataba huo.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, mkataba wa sasa kati ya TFF na Vodacom unatarajiwa kumalizika Agosti 31 mwaka huu.
Kutosainiwa kwa mkataba mpya huenda kukasababisha michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyopangwa kuanza Septemba mbili mwaka huu kuchelewa kuanza.
Liwazozito imebaini kuwa, viongozi wa TFF wamegawanyika kuhusu udhamini wa ligi hiyo, baadhi wakati wakitaka Vodacom iendelee na wengine wakitaka udhamini mpya wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, viongozi wengi wa TFF wanataka TBL iwe mdhamini mpya wa ligi hiyo, hali iliyosababisha Vodacom isite kutia saini mkataba mpya.
Awali, TFF ilipanga kuingia mkataba mpya na Vodacom mwanzoni mwa mwezi huu na kisha kuupitisha kwa klabu za ligi kuu ili ziweze kutoa baraka zake.
Hata hivyo, viongozi wa klabu za ligi kuu hawajafurahishwa na mkataba huo na wametaka uboreshwe kabla ya kuanza kwa ligi kuu. Viongozi hao walilalamikia uchache wa zawadi na kucheleweshwa kwa pesa za nauli.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alikiri jana kuhusu kuchelewa kutiwa saini kwa mkataba huo, lakini alisema mambo yatakwenda vizuri.
"Ni kweli bado hatujasaini mkataba mpya, lakini kila kitu kinakwenda vizuri,kuna baadhi ya vitu vimekwama kidogo vinafanyiwa kazi na siku chache tutafanya kazi hiyo,"alisema katibu huyo.

No comments:

Post a Comment