KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 16, 2012

ANNA MWAOLE: LENGO LANGU NI KUMILIKI BENDI

Anna Mwaole akiimba wakati alipokuwa katika bendi ya Super Kamanyola ya mjini Mwanza

Anna Mwaole (kushoto) wa Super Kamanyola na Nyota Waziri wa The Kilimanjaro wakiimba wakati wa onyesho la pamoja la bendi hizo.


BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mwanamuziki nyota wa kike nchini, Anna Mwaole ameibuka na albamu yake mpya na ya kwanza inayokwenda kwa jina la Shoka la Bucha.
Anna, ambaye amewahi kuimbia bendi 17 za hapa nchini, amerekodi nyimbo tano kati ya sita zilizomo kwenye albamu hiyo katika studio ya Reflect iliyopo mjini Mwanza.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Anna alisema amerekodi albamu hiyo kwa msaada wa mfadhili wake, ambaye hakuwa tayari kumtaja.
Anna alisema ameamua kutoa albamu kwa lengo la kujiongezea mapato baada ya kuwa amefanyakazi kwa miaka mingi katika bendi mbali mbali bila ya kupata manufaa makubwa kimaisha.
Mbali ya kibao cha Shoka la Bucha kilichobeba jina la albamu hiyo, alizitaja nyimbo zingine kuwa ni Acha waseme, Sio kama naona wivu, Mageuzi kwa watanzania, Sitaki sitaki visa vyako remix, Penzi la kweli na wimbo mmoja wa kihehe.
Anna alisema wimbo wa Penzi la kweli ameuimba kwa kushirikiana na kiongozi wa bendi ya Talent, Hussein Jumbe wakati kibao cha Sitaki sitaki visa vyako amekirudia baada ya awali kukirekodi na bendi ya Sambulumaa.
Mwanamama huyo, ambaye alirejea mjini Dar es Salaam hivi karibuni akitokea bendi ya Super Kamanyola yenye maskani yake mjini Mwanza, alisema amepitia kwenye bendi nyingi kwa sababu amekuwa akikubalika kiuimbaji.
“Siku zote kitu kizuri hakiwezi kukaa mahali pamoja kwa muda mrefu kwa sababu kizuri kinajiuza,” alisema mwanamama huyo, ambaye alianza kujifunza muziki katika bendi ya Maquiz Original mwaka 1989.
Anna amekiri kuwa, muziki wa Tanzania kwa sasa umekuwa na maendeleo makubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita kwa sababu wanamuziki wananufaika kimaisha.
Alisema katika miaka ya nyuma, kulikuwepo na watunzi wengi wazuri wa nyimbo, lakini hawakuweza kunufaika na vipaji vyao kutokana na kuwepo kwa usimamizi mbovu katika fani hiyo.
“Hivi sasa wanamuziki wamekuwa wakifaidika na vipaji vyao na wamekuwa wakiendesha maisha yao vizuri kutokana na muziki, tofauti na miaka ya nyuma,”alisema.
Alipoulizwa sababu ya vijana wengi wa kike kushindwa kupiga muziki wa bendi laivu, Anna alisema ni kutokana na woga na kutojiamini.
Alisema tatizo kubwa, ambalo limekuwa likiwakabili wanawake katika bendi za muziki ni kuwepo kwa vikwazo vingi, vinavyowafanya wakate tamaa mapema.
“Vikwazo kwa wanawake katika bendi za muziki ni vingi. Unahitajika kuwa mvumilivu sana,”alisema Anna.
”Na Muziki wa dansi ni mgumu sio kama bongo fleva. Ndio sababu watoto wa kike akijaribu kidogo na kushindwa, anakata tamaa,”aliongeza.
Pamoja na kuwepo kwa mafanikio katika fani ya muziki, Anna ameeleza kukerwa na tabia ya wacheza shoo wa kike kucheza stejini wakiwa nusu uchi.
Anna alisema tabia hiyo si tu kwamba imekuwa ikiwadhalilisha wanawake, bali pia inakiuka utamaduni na maadili ya kitanzania
”Hivi ukicheza nusu uchi ndio unapendeza na kuvutia mashabiki? Hivi hawa mabinti wanaofanya hivi hawana wazazi?”
”Kwa nini wamiliki wa bendi za aina hii wanawaruhusu wacheza shoo wao kucheza nusu uchi? Kwa nini wanawalazimisha wavae hivyo?
”Nimewahi kutukanwa sana kwa njia ya simu kutokana na msimamo wangu huu, lakini siwezi kuacha kuikemea tabia hii, nitaendelea kusema. Waache kucheza nusu uchi kwa sababu wanajidhalilisha,”alisema mwanamama huyu.
”Kucheza nusu uchi siyo utamaduni wetu. Na kwa nini tuige utamaduni wa wenzetu? Mbona wacheza shoo wa kiume wanavaa smarti stejini?” Alihoji.
Anna alisema tangu ameanza muziki, hajawahi kuvaa mavazi ya aina hiyo na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa wanamuziki wa zamani kama vile marehemu Rahma Sharri, Nana Njige, Kida Waziri, Nyota Waziri, Asia Daruweshi na wengineo.
Mwanadada huyo ametoa mwito kwa wanamuziki nchini kuwa na wivu wa kimaendeleo badala ya wivu wa kurudishana nyuma kwa sababu ya chuki.
Kwa mujibu wa Anna, lengo lake kubwa ni kumiliki bendi yake mwenyewe ili aweze kutoa ajira kwa vijana, hasa wa kike. Pia alisema anapenda kutoa mafunzo ya uimbaji kwa watoto wa kike wenye vipaji na mapenzi ya fani hiyo.
Anna alianza muziki katika bendi ya Maquiz Original chini ya usimamizi wa Issa Nundu na Mobali Jumbe kabla ya kujiunga na Polisi Jazz, ambako alipatiwa mafunzo ya uaskari mwaka 1992.
Baadaye alijiunga na Bantu Group na kushiriki kurekodi wimbo wa Tupunguze matumizi yasiyo ya lazima kabla ya kujiunga na ChocChoc Bayetu iliyokuwa ikiongozwa na Mbombo wa Mbomboka.
Mwaka huo huo, alijiunga na bendi ya Legho Stars iliyokuwa ikiongozwa na marehemu Joseph Mulenga na kutunga wimbo wa Kujenga ni vigumu, kubomoa ni rahisi kabla ya kutua Sambulumaa mwaka 1993 ilipokuwa chini ya King Kikii.
Mwaka huo huo, alijiunga na bendi ya Tanza Muzika iliyokuwa ikiongozwa na Makassy Junior kabla ya kutua Super Matimila ilipokuwa chini ya Dokta Remmy, ambako alidumu kwa miezi sita.
Mwaka uliofuata alijiunga na bendi ya Magereza Jazz, ambayo alidumu nayo kwa miaka miwili na kurekodi wimbo wa Samahani baba watoto kabla ya kutua Vijana Jazz mwaka 2000 na kudumu nayo hadi 2002.
Anna alijiunga na kikundi cha Muungano Cultural Troup mwaka 2003 na kushiriki kurekodi albamu ya Hatutaki ukewenza ya bendi ya muziki wa dansi ya kikundi hicho. Pia alirekodi wimbo wa taarab unaojulikana kwa jina la Hata mkisema uliotungwa na Mustafa Ramadhani.
Mwaka mmoja baadaye alikabidhiwa vyombo vya bendi ya Lolita na kuwa kiongozi, lakini ilisambaratika baada ya miaka miwili kufuatia mmiliki wake kuamua kuvifungia vyombo vyake.
Kuanzia mwaka 2006 hadi 2007 alikuwa katika bendi ya Wazee Sugu kabla ya kwenda Zanzibar na kupiga muziki kwenye hoteli za kitalii kwa mwaka mmoja. Mwaka 2009 alijiunga na Bana Maquiz inayoongozwa na Tshimanga Kalala Assosa kabla ya kwenda Mwanza, ambako alijiunga na Super Kamanyola hadi mwezi uliopita alipoamua kurudi Dar es Salaam kwa lengo la kupumzika.

No comments:

Post a Comment