KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, August 14, 2012

Taifa Stars yatua salama Gaborone

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kikiwa na wachezaji 17 kimewasili leo asubuhi jijini Gaborone tayari kwa mechi ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya wenyeji Botswana 'Zebras' itakayochezwa kesho (Agosti 15 mwaka huu).

Stars ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sir Seretse Khama saa 5.45 asubuhi kwa saa za hapa ambapo nyumbani ni 6.45 na kupokewa na viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Botswana (BFA) na Watanzania wanaoishi hapa Botswana.

Baadhi ya wachezaji walioko kwenye kikosi hicho ni Frank Domayo, Ramadhan Singano na Simon Msuva ambao walijiunga na Stars saa chache baada ya kurejea kutoka Nigeria ambapo walikuwa na timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) ambayo Jumapili ilicheza mechi ya mashindano ya Afrika dhidi ya Nigeria (Flying Eagles).

Wachezaji wengine kwenye kikosi kilichoko Botswana ni Aggrey Morris, Amir Maftah, Athuman Idd, Erasto Nyoni, Haruna Moshi, Juma Kaseja, Kelvin Yondani, Mrisho Ngassa, Mwadini Ally, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Chombo, Salum Abubakar, Said Bahanuzi na Shabani Nditi.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefikia kwenye hoteli ya Oasis ambayo pia ndipo Zebras imepiga kambi kwa ajili ya mechi hiyo.

Mechi itaanza kesho saa 1 kamili usiku kwa saa za hapa na itafanyika kwenye Uwanja wa Molepolole Sports Complex. Uwanja wa Taifa wa Botswana hivi sasa uko kwenye matengenezo.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema mechi hiyo ni muhimu kwa vile timu yake bado inakabiliwa na mechi za Kombe la Dunia Kanda ya Afrika, na michuano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) inayotarajia kuanza baadaye mwaka huu.

No comments:

Post a Comment