KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 12, 2012

DOGO JANJA; SINA KINYONGO NA MADEE



MSANII chipukizi wa muziki wa kizazi kipya nchini, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ amesema hana kinyongo wala matatizo na mlezi wake wa zamani, msanii Ahmed Ally ‘Madee’ wa kundi la Tip Top Connection.
Akihojiwa katika kipindi cha Friday Night Live kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Channel Five mwishoni mwa wiki iliyopita, Dogo Janja alisema ameamua kusamehe yote yaliyotokea kati yake na Madee.
“Yeye ndiye aliyenilea hadi kufikia hapa nilipo, namheshimu, amenitoa mbali, sina kinyongo naye,”alisema.
Hata hivyo, Dogo Janja alikiri kuwa, vitendo alivyokuwa akifanyiwa na Madee kabla ya kurejea Arusha, havikuwa vya kiungwana.
“Nilipoondoka kurudi Arusha, hakuwahi kunipigia simu kuniuliza kama nimefika salama. Hakuwa mtu mwema kwangu,”alisema Dogo Janja.
“Lakini namshukuru Mungu kwamba ndiye aliyenifikisha hapa nilipo na kunifanya nijulikane. Kila ninapopita mahali, watu wanajua kwamba yule ni Dogo Janja,”aliongeza.
Dogo Janja alisema kwa sasa ameamua kujiunga na kundi la Mtanashati linalomilikiwa na mfanyabiashara Ustaadh Juma Namusoma.
Alisema tayari ameshatunga kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Ya moyoni, ambacho kazi ya kukirekodi inatarajiwa kumalizika hivi karibuni.
Alisema kibao hicho kinaelezea matukio mbalimbali yaliyowahi kumkuta wakati akiwa chini ya kundi la Tip Top Connection na ulezi wa Madee.
“Lengo la wimbo huu si kuzungumzia mambo mabaya. Nasimulia mambo yaliyonisibu, simlengi mtu. Kwa sasa nimeamua kuangalia ninakokwenda,”alisema.
Madee alikaririwa hivi karibuni akidai kuwa, aliamua kumrejesha Dogo Janja kwao kutokana na kulewa sifa na pia kuwa mtoro shuleni.
Hata hivyo, Dogo Janja alikanusha madai hayo kwa kusema, alikuwa akipata mateso mazito alipokuwa chini ya Madee, ikiwa ni pamoja na kufanyishwa kazi nyingi na kuambulia malipo kiduchu.

No comments:

Post a Comment