KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 12, 2012

Cheo cha Ofisa Habari chafutwa ZFA

CHAMA cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kimemuondoa msemaji na ofisa wake wa habari, Munir Zakaria kwa madai kuwa, cheo hicho kimefutwa.
Uamuzi wa kufutwa kwa cheo hicho ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya chama hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye hoteli ya Ocean View mjini hapa.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na rais mpya wa ZFA, Amani Makungu, wajumbe walifikia uamuzi wa kukifuta cheo hicho kwa vile hakimo kwenye katiba.
Katibu Mtendaji wa ZFA, Kassim Haji Salum alisema juzi mjini hapa kuwa, uteuzi wa ofisa habari ulifanyika kimakosa katika uongozi uliopita kwa vile cheo hicho hakimo kwenye katiba.
Salum alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, msemaji mkuu wa masuala mbalimbali yanayoihusu ZFA ni rais wake kwa kushirikiana na katibu mkuu.
"Kwa mujibu wa katiba yetu, rais anazo nafasi nne za kufanya uteuzi wa watu wa kumsaidia kazi, lakini hakuna nafasi ya ofisa habari. Kazi ya kukisemea chama ni ya rais kwa kushirikiana na katibu mkuu", alifafanua.
Hata hivyo, Salum alisema Zakaria ataendelea kuwa mjumbe wa kawaida wa kamati ya utendaji ya ZFA kwa vile uteuzi wake ulifuata katiba.
“Kwa sasa tumeamua kufanya kazi zetu kikatiba zaidi na kufutwa kwa cheo cha ofisa habari ni utekelezaji wa mkakati wetu huo,”alisema.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, kuondolewa kwa Zakaria katika nafasi hiyo kulitokana na kauli yake kwa vyombo vya habari kwamba, iwapo Simba na Azam zitafuzu kucheza fainali ya michuano ya Kombe la Urafiki, mechi hiyo itachezwa Dar es Salaam badala ya Zanzibar.
Imedaiwa kuwa, Zakaria alitoa kauli hiyo bila kupata idhini kutoka kwa viongozi wa chama hicho pamoja na waandaaji wa mashindano hayo.
Kauli hiyo iliwakera wadau wa michezo visiwani Zanzibar, ambao wamekuwa wakihoji iweje fainali hiyo ihamishiwe Dar es Salaam katika hatua ya mwisho wakati mechi zote za mwanzo zilichezwa kwenye Uwanja wa Amaan.
Katika hatua nyingine, ZFA imemteua Suleiman Mahmoud Jabir kuwa mkurugenzi mpya wa ufundi wa chama hicho wakati Abdalla Juma Mohamed ameteuliwa kuwa mwanasheria wa chama.
Salum alisema juzi kuwa, kazi za mkurugenzi huyo wa ufundi ni kupanga programu za maendeleo ya soka kwa timu za madaraja yote na pia mitaala ya mafunzo ya soka kwa waamuzi, makocha na viongozi wa klabu.

No comments:

Post a Comment