KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, July 22, 2012

WENGER AITOLEA NJE MAN UTD, AGOMA KUMUUZA VAN PERSIE KWA DAU DOGO

LONDON, England
KLABU ya Arsenal imegoma kumuuza mshambuliaji wake nyota, Robin van Persie kwa kitita cha pauni milioni 20 kwa klabu ya Manchester United.
Kocha Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger alisema juzi kuwa, watakuwa tayari kumuuza mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi iwapo klabu yoyote inayomuhitaji itatoa kitita cha zaidi ya pauni milioni 25 na 30.
“Van Persie ni mmoja wa washambuliaji bora duniani, kama si bora, na lengo langu ni kumbakisha katika klabu. Nitafanya kile ambacho ni bora kwa maslahi ya Arsenal,”alisema kocha huyo raia wa Ufaransa.
Msimamo huo wa Wenger huenda ukatoa mwanya kwa klabu ya Manchester City, ambayo nayo inamuwinda nyota huyo, kuongeza dau la kumsajili.
Awali, Manchester United ilikuwa tayari kumsajili Mholanzi huyo kwa kitita cha pauni milioni 15 kabla ya kuongeza dau na kufika pauni milioni 20.
Mbali na Manchester United na Manchester City, mshambuliaji huyo pia anawaniwa kwa udi na uvumba na klabu ya Juventus ya Italia.
Manchester City inataka kumuuza mmoja kati ya wachezaji wake, Edin Dzeko au Carlos Tevez ili iweze kupata pesa za kutosha kumsajili Van Persie.
Kocha Mkuu wa Manchester City, Roberto Mancini anaamini kuwa, ni klabu yake pekee yenye uwezo wa kutoa pesa inazihitaji Arsenal kwa ajili ya kumuuza nyota huyo.
Manchester United imekuwa ikimpa Van Persie thamani ndogo kutokana na kuwa na umri wa miaka 29 na pia yupo kwenye mwaka wa mwisho katika mkataba wake na Arsenal.
Tayari Van Persie ameshaeleza azma yake ya kutaka kuihama klabu hiyo, akiwa anataka kufuata nyayo za Cesc Fabregas aliyejiunga na Barcelona ya Hispania msimu uliopita.
Hivi karibuni, Van Persie aligoma kuongeza mkataba mpya wa kuichezea Arsenal, hali iliyodhihirisha wazi kuhusu msimamo wake wa kutaka kuhama.
Kocha Wenger amemwacha mchezaji huyo katika ziara ya barani Asia kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi na kusisitiza kuwa, hatamuuza kwa dau dogo.
Wenger alisema juzi kuwa, yupo tayari kumbakisha Van Persie katika klabu yake hadi mkataba wake utakapomalizika iwapo hakutakuwa na klabu itakayoweza kulipa dau analolitaka.
Kocha huyo alisema anaamini Van Persie ataendelea kuitumikia Arsenal kwa moyo wote kwa sababu anapenda kucheza soka na hiyo ndiyo heshima pekee anayoweza kuipata akiwa mchezaji.
Bodi ya wakurugenzi ya Arsenal huenda ikafunga mjadala kuhusu uhamisho wa nyota huyo, lakini kwa kutegemea maamuzi ya Wenger.
Wenger hakufurahishwa na maamuzi ya bodi hiyo katika usajili wa wachezaji wapya msimu uliopita na ndio sababu ameamua kumuuza kwa pesa nyingi ili apate pesa za kununua nyota wengine wapya.
Kocha Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amethibitisha kuwasilisha ofa ya kumsajili nyota huyo kwa klabu ya Arsenal.
Hata hivyo, kocha huyo hakuwa tayari kueleza iwapo wataongeza dau kwa ajili ya kumnasa nyota huyo baada ya pesa walizotenga awali kukataliwa.
Van Persie ameifungia Arsenal mabao 41 katika mechi 53 msimu uliopita na alichaguliwa kuwa mchezaji nyota wa mwaka wa Chama cha Wanaska wa Kulipwa wa England.
Arsenal inatarajiwa kucheza mechi za kirafiki katika nchi za Malaysia, China na Hong Kong katika kipindi cha wiki mbili zijazo.
Hata hivyo, Van Persie atabaki England wakati timu yake itakapokuwa katika ziara hiyo, akifanya mazoezi ya viungo kwenye kituo cha mazoezi cha klabu hiyo.

No comments:

Post a Comment