KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, July 27, 2012

KEPTENI KOMBA AREJEA KUTOKA INDIA

Kepteni John Komba akiwa na mkewe Salome, nyumbani kwake Mbezi, Dar es Salaam.


MKURUGENZI wa Kundi la Tanzania One Theatre (TOT), ambaye pia ni Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba amerejea nchini kutoka India, ambako alikwenda kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kumtibu ugonjwa wa nyonga uliokuwa ukimsumbua upande wa mguu wake wa kulia.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, nyumbani kwake Mbezi kwa Komba, mjini Dar es Salaam, Komba alisema alirejea nchini juzi baada ya kupatiwa matibabu hayo kwenye hospitali ya Appolo iliyopo Hydrabad nchini India tangu mwanzoni mwa wezi huu.


Komba alisema, aliondoka nchini Julai 2, 2012 baada ya kupelekwa na serikali kwa maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete, Spika wa Bunge Anna Makinda na Katibu wa Bunge John Kashilila na kwamba alikwenda baada ya kukosa matibabu hapa nchini kwa sababu ya mgomo wa madaktari.


"Siku napelekwa Muhimbili tu, tayari madaktari walikuwa wameanza siku ya kwanza ya mgomo wao, nikawa sina namna ila kuujulisha uongozi wa Bunge na kisha nikamuomba Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, naye kwa mamlaka yake akanisaidia haraka kama ambavyo huwasaidia wengine kwenda kutibiwa nje", alisema Komba.


Alisema uzito ulichangia sana kusababisha mifupa kusagana kwenye nyonga upande wa mguu wa kulia, ambapo hadi anakwenda India, alikuwa na uzindo wa kilo 138 wakati wastani wa uzito aliotakiwa kuwa nao kulingana na ukubwa wa mwili wake ni kilo 90 au 100 tu.


Komba alisema baada ya matibabu, amerejea nchini akiwa na uzito wa kilo 128, ambao hata hivyo ametakiwa kuudhibiti na kuupunguza katika siku ambazo atalazimika kupumzika nyumbani kabla ya kuanza kazi Septemba mwaka huu kama alivyoelekezwa na madaktari.

Akizungumzia upasuaji ulivyoendeshwa, Komba alisema ulichukua saa tano na kukamilika bila matatizo. Alisema katika upasuaji huo, sehemu iliyopasuliwa ni ya ukubwa wa futi moja.

Hata hivyo, alisema baada ya upasuaji huo, hakuweza kurejea katika wodi ya kawaida kwa sababu magonjwa kadhaa yaliibuka, ikiwemo homa kali na presha hivyo akalazimika kulazwa katika wodi ya wagonjwa waliopo kwenye uangalizi maalum (ICU) kwa siku tano.

"Sasa nimerejea nikiwa mzima, kwa sasa natumia fimbo hii, ili kuwezesha uzito usielemee upande wa kulia nilikopanyiwa upasuaji, lakini sijambo kabisa," alisema Komba.

Komba alilaani baadhi ya vyombo vya habari, ambavyo viliripoti kwamba katika kuugua kwake alikuwa mahututi na kwamba alikuwa anaugua figo.

"Jamani ninyi waandishi wa habari, jizoesheni kuandika habari zilizokamilika siyo kurashia-rashia tu na kuzusha uongo. Mfano gazeti moja liliandika eti naugua figo, nipo mahututi wakati si kweli kabisa, ilikuwa jambo rahisi tu, kuja hapa nyumbani na kuniuliza au kuuliza mke wangu lingepata kwa uhakika ninachoumwa", alisema Komba.

No comments:

Post a Comment