KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 12, 2012

MATONYA; MAPENZI YA SASA NI KAMALI

BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mwimbaji nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Seif Shabani ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Mapenzi kamali.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Seif ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Matonya alisema, kibao chake hicho kimeshaanza kusikika na kuonyeshwa kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini.
Matonya alisema kibao chake hicho kinaelezea halisi hali ya mapenzi hivi sasa, ambayo yametawaliwa zaidi na pesa na kuyafanya yaonekane sawa na mchezo wa kamali.
Alisema baadhi ya matukio aliyoyasimulia katika wimbo huo yamekuwa yakitokea mara kwa mara kwenye jamii na mengine yaliwahi kumtokea yeye binafsi.
"Hivi sasa ni kama tunaishi maisha ya kimafia, tunaweka pesa mbele zaidi, sio kama zamani, ambapo tulikuwa na aibu. Sasa kila kitu kipo wazi, mapenzi yamekuwa kama kamali, unakula na kuliwa,"alisema.
Pamoja na kuibuka na kibao hicho kipya, Matonya alisema hatarajii tena kurekodi albamu kutokana na mauzo yake kuwa mabovu.
Alisema gharama za kurekodi nyimbo studio pamoja na kutengeneza mkanda wa video ni kubwa ikilinganishwa na malipo wanayoyapata wasanii kutokana na mauzo.
"Unaweza kutumia shilingi milioni tatu au nne kutengeneza albamu, lakini ukipeleka kwa wahindi, unapata nusu ya pesa hizo,"alisema.
"Hali hiyo imenifanya kwa sasa niamue kurekodi nyimbo moja moja hadi soko la albamu litakapokaa vizuri,"aliongeza Alipoulizwa sababu ya kuwa kimya kwa muda mrefu, Matonya alisema ni kutokana na kutingwa na shughuli nyingi za kibiashara.
Matonya alisema kwa muda mrefu sasa, amekuwa akisafiri sehemu mbalimbali barani Ulaya na katika nchi jirani ya Kenya kwa malengo ya kibiashara na hivyo kuwa bize.
Hata hivyo, alikiri kuwa ujenzi wa hoteli yake mpya mjini Tanga ndio unaomuumiza kichwa zaidi kwa vile bado haijakamilika na imemgharimu fedha nyingi.
"Hoteli hii imenigharimu fedha nyingi na ujenzi wake bado unaendelea, lakini hatua iliyobaki ni ndogo. Natarajia itakamilika hivi karibuni,"alisema.
Msanii huyo aliyewahi kutamba na kibao cha Anita, alichokiimba kwa kushirikiana na Judith Wambura 'Lady Jaydee' hakuwa tayari kusema ni lini hoteli hiyo itakamilika.
Matonya alianza kung'ara kimuziki mwaka 2003 baada ya kurekodi albamu yake ya kwanza na kumfanya awe mmoja wa wanamuziki wa kizazi kipya wanaoheshimika.
Alirekodi albamu yake ya pili mwaka 2006 inayojulikana kwa jina la Violeth, ambayo ilimwezesha kushinda tuzo za muziki za Kilimanjaro. Katika albamu hiyo, aliwashirikisha baadhi ya wasanii nyota kama vile Khamis Mwinjuma 'Mwana FA', Joslin na Sameer 'Mr. Blue'.
Msanii huyo aliamua kujiita Matonya kutokana na ugumu wa maisha aliokumbana nao wakati akiingia kwenye ulingowa muziki. Matonya ni jina, ombaomba maarufu aliyekuwa akivinjari katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam akitokea katika mji wa Dodoma.

No comments:

Post a Comment