KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 12, 2012

CECAFA yachafua hewa ZFA

CHAMA cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kimepinga uamuzi wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kumjumuisha Katibu Mtendaji wa zamani wa chama hicho, Mzee Zam Ali kwenye orodha ya wajumbe wake wa kamati ya utendaji.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya ZFA kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye hoteli ya Ocean View mjini hapa chini ya rais wake mpya, Amani Makungu. ZFA ilikuwa imeandika barua CECAFA ikiutambulisha uongozi wake mpya chini ya Makungu, Makamu Mwenyekiti, Masoud Attai na Katibu Mtendaji, Kassim Haji Salum.
Lakini katika majibu yake kwa ZFA, baraza hilo lilikubali kuwatambua Makungu na Attai na kutomtambua Kassim kama katibu mtendaji. Badala yake, baraza hilo lilimtaja Zam kuwa ndiye katibu mtendaji halali.
Habari kutoka ndani ya ZFA zimeeleza kuwa, uamuzi huo wa CECAFA ulipingwa vikali na wajumbe wa kamati ya utendaji ya chama hicho, ambao waliweka msimamo kuwa hawapo tayari kupangiwa viongozi na baraza hilo.
Zam alikuwa katibu mtendaji wa ZFA kwa miaka mingi, lakini alistaafu kazi mwaka jana.
Kufuatia kustaafu kwa Zam, nafasi yake ilichukuliwa na Kassim, ambaye alikuwa akishika wadhifa huo kwa upande wa Pemba.
Mbali na Zam, ZFA pia imepata rais mpya, Makungu baada ya Ali Ferej Tamim kujiuzulu mwezi uliopita.
Mmoja wa viongozi wa juu wa ZFA alithibitisha kutokea kwa utata huo, lakini hakutaka kuzungumza kwa undani zaidi kuhusu suala hilo.
“Tumeshaandika barua CECAFA kueleza msimamo wetu kwa hiyo bado tunasubiri majibu. Lakini msimamo wetu ni kwamba hatuwezi kupangiwa viongozi na baraza hilo kwa sababu Mzee Zam Ali alishastaafu wadhifa huo,” kilisema chanzo cha habari.

No comments:

Post a Comment