KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 19, 2012

CAF yaitoza faini Jamhuri

Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), Amani Makungu



SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeitoza faini ya dola 5,000 za Marekani (sh milioni nane) timu ya Jamhuri ya Pemba kwa kosa la kuonyeshwa kadi nne za njano katika mechi moja.
Barua ya CAF iliyotumwa kwa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) wiki hii ilieleza kuwa, tukio hilo lilitokea Machi 4 mwaka huu wakati Jamhuri ilipomenyana na Hwangwe ya Zimbabwe.
Katika mechi hiyo iliyochezwa mjini Harare, Jamhuri ilichapwa mabao 4-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 7-0, kufuatia kuchapwa mabao 3-0 katika mechi ya awali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Haji Salum alithibitisha kupokea barua hiyo iliyoandikwa na CAF na kwamba tayari ameiwasilisha kwa uongozi wa Jamhuri.
Alipoulizwa sababu ya kuchelewa kwa barua hiyo iliyoandikwa Mei 31 mwaka huu, Kassim alisema haelewi ni kwa sababu gani. Alisema walipata barua hiyo Julai 13 mwaka huu.
Kassim alisema kwa mujibu wa kanuni mpya za mashindano yanayoandaliwa na CAF, timu inayopata kadi zaidi ya tatu katika mechi moja, itatozwa kiasi hicho cha faini.
Kwa mujibu wa Kassim, kosa hilo linahesabika kuwa ni la utovu wa nidhamu na fedha hizo zinapaswa kulipwa katika kipindi cha miezi miwili tangu kupokelewa kwa barua hiyo.
Meneja wa Jamhuri, Abdalla Abeid ‘Elisha’ alithibitisha kupokea barua hiyo, lakini aliilaumu ZFA kwa kuikalia na kuchelewa kuiwasilisha kwao kwa wakati.
Elisha alikiri pia kuwa, ugeni wa timu yao katika mashindano ya CAF uliwafanya washindwe kutambua uwepo wa kanuni hiyo na hivyo kushindwa kuchukua tahadhari mapema.
Kutokana na timu yake kutokuwa na uwezo wa kulipa faini hiyo, Elisha alisema wamewasilisha maombi ya kutaka wasaidiwe kwa kamati maalumu iliyoundwa kwa ajili ya kuzisaidia Jamhuri ya Mafunzo katika michuano ya kimataifa.
"Ni jambo la kusikitisha kwamba barua iliandikwa tangu Mei mwaka huu, lakini sisi tumeipata juzi na hali yetu inajulikana vyema. Tuombe Mungu atusaidie,”alisema.

No comments:

Post a Comment