KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 25, 2012

SIMBA YAITISHA MKUTANO MKUU AGOSTI 5

UONGOZI wa klabu ya Simba umeitisha mkutano mkuu wa
wanachama uliopangwa kufanyika Agosti 5 mwaka huu kwenye
ukumbi wa bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay mjini Dar es
Salaam.
Simba imeitisha mkutano huo siku moja baada ya kutupwa nje ya
mashindano ya Kombe la Kagame katika hatua ya robo fainali
baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Azam.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es
Salaam jana kuwa, mkutano huo unatarajiwa kujadili masuala
mbali mbali yanayoihusu klabu hiyo.
Alizitaja baadhi ya ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo
kuwa ni pamoja na ripoti ya mapato na matumizi na maandalizi
ya michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara na klabu bingwa Afrika.
Ili kufanikisha kufanyika kwa mkutano huo, Kamwaga alisema
klabu yake jana ilipokea msaada wa sh. milioni 20 kutoka kwa
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Hundi ya pesa hizo ilikabidhiwa kwa Makamu Mwenyekiti wa
Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Meneja wa Bia ya
Kilimanjaro, George Kavishe katika hafla iliyofanyika makao makuu
ya kampuni hiyo, Ilala, Dar es Salaam.
Kamwaga alisema wakati wa mkutano huo, watazindua Wiki ya
Simba na Jamii, ambayo itawahusu wachezaji, viongozi na
makocha kufanya ziara katika hospitali mbali mbali pamoja na
kutoa misaada kwa wagonjwa na watoto yatima.
Kwa mujibu wa Kamwaga, Simba pia imeandaa tamasha la kila
mwaka la klabu hiyo linalotarajiwa kufanyika Agosti 8 mwaka huu
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Maandalizi ya tamasha hilo (Simba Day) yameshaanza na
yanaendelea vizuri na kwa sasa kocha wetu yupo kwenye harakati
za kuboresha timu,”alisema Kamwaga.
Kwa upande wake, Kavishe aliahidi kuwa, siku hiyo
watawakabidhi viongozi wa Simba basi jipya litakalokuwa
likitumiwa na wachezaji kwa ajili ya kusafiri mikoani.

No comments:

Post a Comment