KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, July 22, 2012

Mtoto wa kufikia wa Usher Raymond afariki duni

Usher Raymond akiwa na Kyle Glover wakati wa uhai wake na mkewe wa zamani, Tameka Foster


ATLANTA, Marekani
MTOTO wa kiume wa mwanamuziki Usher Raymond, Kyle Glover amefariki dunia baada ya madaktari kuondoa chombo cha kumsaidia kupumua.
Glover (11) alifariki dunia juzi asubuhi katika hospitali ya Egleston mjini Atlanta, ambako alikuwa amelazwa baada ya kupata ajali ya boti Julai 6 mwaka huu.
Mtoto huyo wa Usher alipata majeraha makubwa kichwani na imeelezwa kuwa, ubongo wake ulikuwa haufanyikazi.
Glover, ambaye ni mtoto wa mke wa zamani wa Usher, Tameka Foster, alipata ajali hiyo katika Ziwa Lanier wakati yeye na watoto wenzake walipokuwa wakicheza mchezo wa kuendesha boti ndogo.
Madaktari waliokuwa wakimtibu mtoto huyo waliamua kuzima mashine za kumsaidia kupumua baada ya kubaini kwamba asingeweza kupona.
Imeelezwa kuwa, Tameka alikuwa kwenye wakati mgumu wa kukubali uamuzi huo wa madaktari na alichanganyikiwa.
Glover alijeruhiwa vibaya kichwani wakati boti aliyokuwa akiendesha ilipogongana na boti nyingine kwenye ziwa hilo.
Kwa mujibu wa taarifa, mtoto wa familia ya karibu na Usher alipoteza mwelekeo wakati akiendesha botu yake na kugongana na iliyokuwa ikiendeshwa na Glover.
Wakati wa ajali hiyo, Glover alikuwa pamoja na mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15 na wote walikimbizwa kwenye hospitali ya Egleston.
Wanamuziki mbali mbali maarufu wa Marekani wamemtumia salamu za rambirambi Usher kutokana na kifo hicho cha mwanaye, akiwemo Justin Bieber.
Bieber alieleza kupitia mtandao wa twitter: “Kalale pema Kile” wakati mwanamuziki Russell Simmons aliandika: “Natuma salamu za rambirambi kwa Tameka, Ryan, Usher na familia yao.”
Wiki iliyopita, familia ya Glover iliwaomba watu mbalimbali kumuombea dua mtoto huyo ili aweze kupona kufuatia ajali hiyo mbaya.
Usher na Tameka walitengana mwaka 2009, ikiwa ni miaka miwili tu tangu walipofunga ndoa na walikuwa katika mzozo wa kugombea malezi ya watoto wao, Usher Raymond V (4) na Navidy (3).
Hata hivyo, waliamua kuweka kando tofauti zao baada ya ajali hiyo. Baba wa Glover ni Ryan Glover, ambaye ni mume wa zamani wa Tameka.

No comments:

Post a Comment