KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, March 28, 2016

CHAD YAIFANYIA KITU MBAYA TAIFA STARS



Timu ya Taifa ya Chad  ‘Les Sao’ imejiondoa katika michuano ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) itakayofanyika mwaka 2017 nchini Gabon.

Taarifa ya kujitoa kwa Chad imetolewa na Shirikisho la Mpira wa miguu barani Afrika (CAF) jana baada ya Les Sao kuandika barua ya kujitoka katika mashindano hayo ikiwa katika kundi G pamoja na timu za Tanzania, Nigeria na Misri.

Chad ilitarajiwa kucheza leo (Jumatatu) dhidi ya Tanzania katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, ikiwa ni mchezo wa marudiano wa kundi G baada ya kucheza mchezo wa awali jijini N’Djamena katika ya wiki.

Katika mchezo wa awali uliochezwa uwanja wa Idriss Mahamat Ouya, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 1- 0 , bao lililofungwa na nahodha Mbwana Samatta dakika ya 30 ya mchezo.

Kufuatia kujitoa kwa Chad, matokeo ya michezo yote iliyoihusisha timu hiyo yanafutwa, na msimamo wa kundi G kwa sasa unaongozwa na Misri yenye pointi 4, Nigeria pointi 2 na Tanzania pointi 1.

Kwa mujibu wa ibara ya 61 ya kanuni za mashindano kinasomeka kwamba: “kama timu itajitoa kwenye hatua ya kufuzu kwenye hatua ya makundi, matokeo yake yote yatafutwa (pointi, magoli ya kufunga na magoli ya kufungwa)”.

Maamuzi ya kamati ya utendaji ya CAF yaliyofanywa January 15, 2015 yalikuwa kwamba, kundi lolote litakalosalia na timu tatu kufuatia kujitoa kwa moja ya timu kwenye kundi hilo, timu itakayoongoza kundi hilo itafuzu moja kwa moja kwenye michuano hiyo.

Kutokana na timu ya Chad kujiondoa kwenye mashindano, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Chad limepigwa faini ya dola za kimarekani 20,000 pamoja na kufungiwa kushiriki michuano ijayo ya AFCON kwa mujibu wa ibara ya 59 ya kanuni za mashindano ambacho kinaeleza kwamba: “Shirikisho lolote likithibitisha kujiondoa baada ya mechi kuanza kuchezwa litawajibika kulipa faini ya dola za kimarekani 20,000. Pia haitaruhusiwa kushiriki mashindano yanayofuata.

Wakati huohuo, Misri watachuana dhidi ya Nigeria Jumanne  March 29, 2016 Alexandria, Misri.

No comments:

Post a Comment