KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, March 27, 2016

TASWA YAPATA WADAU WATAKAOSAIDIA KUDHAMINI MAFUNZO KWA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO



KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) ilikutana hivi karibuni na kujadili masuala mbalimbali.

A; Mafunzo

TASWA imepata wadau watakaosaidia kudhamini mafunzo kwa waandishi wa habari za michezo 60 chipukizi na wale wa kada ya kati.

Mada mbalimbali zitatolewa zikihusisha wataalamu wa uandishi wa habari za michezo, wahariri wazoefu na baadhi ya wataalamu wa michezo mbalimbali.

Pia itatolewa mada ya masuala ya ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano na namna ya kuripoti habari za michezo.

Mafunzo haya yatafanyika Mei 21-23 mwaka huu jijini Dar es Salaam, ambapo TASWA inaendelea na juhudi za kusaka wadau wengine ili mafunzo hayo yatatanguliwe na mkutano wa siku moja kwa wahariri wa habari za michezo na baadhi ya waandishi wazoefu wa habari za michezo.

Utaratibu wa kupata washiriki hao utafanyika kwa kutumia wahariri wa habari za michezo wa vyombo mbalimbali kwa kadri mahitaji yatakavyoruhusu.

TASWA inawashukuru wadau hao ambao tutawatangaza baada ya taratibu za udhamini wao kukamilika na tunaomba wengine waendelee kutuunga mkono katika hili.

B: Media Day

Kwa miaka miwili sasa, bonanza la wanahabari ‘Media Day’ limeshindwa kufanyika kutokana na sababu mbalimbali, hivyo imeundwa kamati ndogo kwa ajili ya jambo hilo na inaendelea vyema na maandalizi na muda si mrefu majibu mazuri yatatangazwa.

C: Vitambulisho

Tulisitisha kwa muda kutoa vitambulisho kwa wanachama ili kuboresha utaratibu na kutoa vyenye ubora zaidi, hilo tayari limekamilika na mtatangaziwa utaratibu mzuri na wale wote ambao hawana watapata vitambulisho vyao.

Nawasilisha,

Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
26/03/2016

No comments:

Post a Comment