KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, March 21, 2016

AFRICANS SPORTS YATUNGULIWA 1-0 NA PRISONS


 AFRICAN Sports imezidi kujiweka katika mazingira ya kushuka daraja baada ya kufungwa 1-0 nyumbani na Prisons ya Mbeya jioni ya leo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Bao pekee la Prisons leo limefungwa na beki James Mwasote sekunde ya 46 dakika ya kwanza aliyepiga kona iliyoingia moja kwa moja nyavuni, ingawa ilisindikizwa na Jumanne Elfadhil wakati tayari imekwishaingia langoni.
Kwa ushindi huo, Prisons inafikisha pointi 39 baada ya kucheza mechi 24 ingawa inaendelea kukamata nafasi ya tano, nyuma ya Mtibwa Sugar yenye pointi 39 pia na wastani mzuri wa mabao.
Kwa African Sports, inabaki na pointi zake 20 za mechi 24 na kuendelea kushika nafasi ya 15 katika ligi ya timu 16, mbele ya ndugu zao, Coastal Union wenye pointi 19 za mechi 24 pia.
Sports iliyopanda Ligi Kuu msimu huu baada ya zaidi ya miaka 20, sasa inahitaji kufanya kazi ya ziaba ili kubaki kwenye ligi hiyo, sawa na ndugu zao, Coastal na JKT Mgambo – ambao kwa pamoja wanashika nafasi tatu za mwisho.
Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho Uwanja wa Mkwakwani, kwa timu nyingine ya Tanga, JKT Mgambo kuikaribisha Toto Africans ya Mwanza.
Mgambo inashika nafasi ya 14 kwa pointi zake 20 za mechi 23, wakati Toto ni ya 12 ikiwa na pointi 23 za mechi 22.

No comments:

Post a Comment