KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 3, 2016

PHIRI ATANGAZA KIKOSI CHA MBEYA CITY KITAKACHOIVAA SIMBA JUMAPILI


Kocha Mkuu wa Mbeya City Fc, Kinnah Phiri ametangaza majina ya nyota 18 watakaoivaa Simba Sports Club  kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliopangwa kuchezwa  Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam

Mapema leo Phiri ameuambia  mtandao huu kuwa anatua jijini Dar na kikosi cha nyota hao ambao aliwaandaa maalumu kwa mchezo huo wa mwishoni mwa juma akiwa na imani kubwa kuwa wataiwezesha City kuibuka na ushindi kutokana na  ‘kuiva’  vizuri kimazoezi na mafunzo waliyoyapata katika wiki nzima ya maandalizi  kupitia  mifumo mbalimbali aliyokuwa akiifundisha .

“Nina imani nao,wamefanya vizuri sana kwenye mazoezi ya wiki hii, sina shaka na wao kutupatia matokeo kwa sababu wako sawa tayari kwa mchezo,tutacheza kwenye mfumo mpya ambao haujawahi kuonekana tukicheza, hii ni kwa sababu tumedhamiria kupata ushindi kama ambavyo timu imekuwa ikifanya kila inapokutana na Simba”, alisema.

Miongoni mwa nyota walio kwenye orodha ya kuivaa Simba siku hiyo ya jumapili ni pamoja na mlinzi Hassan Mwasapili, mlinda lango Haningtony Kalyesubula pia wamo Temi Felix, Haruna Shamte,Yohana Moriss,Kenny Ally,Geoffrey Mlawa,Issa Nelson na wakali wengine 10 ambao wamepewa majukumu kadhaa kuhakikisha  City inaandikisha pointi tatu muhimu mbele ya timu hiyo ya Msimbazi.

Huu utakuwa ni mchezo wa sita kwa timu hizi kukutana katika michuano hii ya ligi kuu ya vodacom  huku City ikifanikiwa kushinda mara mara mbili sare mbili na Simba ikishinda mara moja katika michezo mitano iliyozikatanisha timu hizi hapo awali.

Kiungo mshambuliaji wa City, Ramadhani Chombo Redondo amesema  mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania dhidi ya Simba uliopangwa kuchezwa jumapili hii kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar utakuwa mgumu kutokana na mazingira ya timu zote mbili.

Akizungumza  na mbeyacityfc.com mapema leo, Chombo amesema kuwa City inakwenda Dar kucheza mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa uliopita kama ilivyo kwa simba, jambo ambalo linaufanya mchezo huo kuwa mgumu kutokana na uhitaji wa matokeo kwa timu zote.

“Ni wazi utakuwa mgumu, hii ni kwa sababu kila timu inahitaji matokeo baada ya kupoteza mchezo uliopita,Simba na timu nzuri na wako kwenye nafasi nzuri pia lakini wasitegeme kupata ushindi kw sababu sisi tunauhitaji zaidi yao” alisema.

Aidha Chombo aliweka wazi kuwa City ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo hasa ukizingatia  kuwa imekuwa na historia nzuri kila inapokutana na Simba kwenye uwanja wa Taifa.

“City imeshinda mara  kadhaa mbele ya Simba,hili ni jambo nzuri kisaikolojia kwa sababu linaleta kujiamini,imani yangu kubwa dakika 90 za jumapili zitakuwa upande wetu” alisema.

Kuhusu ligi kuu ya Vodacom inayoendelea sasa Redondo aliweka wazi kuwa imekuwa ngumu na yenye changamoto nyingi sana,hasa ukizingatia kuwa timu nyingi zilijiandaa vizuri toka mwanzo wa msimu ingawa pia suala la kusima simama au kupanguliwa kwa ratiba linapunguza msisimko wake.

No comments:

Post a Comment