KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, October 29, 2017

SIMBA, YANGA ZASHINDWA KUTAMBIANA


Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania mzunguko wa nane imeendelea tena kwa mchezo mmoja uliowakutanisha watani wa Jadi nchini Simba na Yanga ambapo timu hizo zimetoshana nguvu ya kugawana alama moja moja baada ya kufungana goli 1-1 kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Wakicheza kwa kujiamini vijana wa Lwandamina walionekana kutengeneza nafasi nyingi za kufunga kuliko vinara wa Ligi Simba huku timu zote zikicheza kwa kuogopana hali ambayo ilipelekea timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko mbalimbali hata hivyo hayakuweza kuwa na manufaa kwa pande zote kwani Yanga waliingia wakiwa na hofu ya kukosa baadhi ya nyota wake muhimu ambao wapo katika majeruhi Thabani Kamusoko,Donald Ngoma na Amis Tambwe.

Simba walikuwa wa kwanza kuapata goli kupitia kwa winga matata Shiza Ramadhani Kichuya dakika ya 57 baada ya krosi ya Emanuel Okwi kupanguliwa na golikipa wa Yanga na uzembe wa Papy Kabamba Tshishimbi ulioweza kumuacha Kichuya aliyemtungua Youthe Rostand.

Baada ya kuingia kwa goli hilo Yanga walijipanga na kuendeleza mashambulizi kwa Simba na dakika ya 60 wachezaji Ajibu na Mwashiuya waligogeana na kutoa pasi kwa Mshambuliaji matata ambaye alikuwa mwiba kwa wekundu wa Msimbazi,Obrey Chirwa na kuisawazishia Yanga.

Hadi mwamuzi wa Kimataifa Heri Sasii anapuliza kipyenga cha mwisho Yanga na Simba wamegawana pointi moja moja na kwa matokeo hayo Simba wanarudi katika nafasi yao ya kwanza kwa kufikisha pointi 16 sawa na Yanga na Azam huku yeye akiwa na uwiano mzuri wa magoli ya kufungwa na kufunga.

Tuesday, October 24, 2017

TAIFA STARS KUJIPIMA UBAVU NA BENIN UGENINI


KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Mayanga amewarejesha kikosini kiungo Farid Mussa na mshambuliaji, Elias Maguri kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa mapema mwezi ujao.
Baada ya kucheza nyumbani mfululizo mechi za kirafiki za kimataifa, Taifa Stars sasa itatoka mwezi ujao kwenda Benin kucheza na wenyeji Novemba 11, mwaka huu.
Mayanga ameita kikosi cha wachezaji 24, ambacho kitaingia kambini Novemba 5 mjini Dar es Salaam kabla ya kusafiri Novemba 9 kwenda Benin tayari kwa mchezo huo. 
Elias Maguri (kushoto) akiwa na Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro'
Na ndani yake amewaorodhesha Maguri aliyekuwa anacheza Oman na Farid Mussa anayecheza Tenerife B ya Hispania, ambao wote hakuwaita kwenye mchezo uliopita dhidi ya Malawi, uliomalizika kwa sare ya 1-1 Oktoba 7, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kikosi kamili cha Taifa Stars kilichotajwa leo kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Simba SC), Peter Manyika (Singida United) na Ramadhani Kabwili, mabeki Boniphace Maganga (Mbao FC), Abdi Banda (Baroka FC/Afruka Kusini), Gardiel Michael (Yanga), Kevin Yondan (Yanga), Nurdin Chona (Prisons), Erasto Nyoni (Simba) na Dickson Job (Mtibwa Sugar).
Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Hamisi Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Muzamil Yassin (Simba), Raphael Daudi (Yanga), Simon Msuva (Yanga), Shiza Kichuya (Simba), Ibrahim Hajib (Yanga), Mohammed Issa (Mtibwa), Farid Mussa (Tenerife/Hispania) na Abdul Mohammed (Tusker/Kenya) na washambuliaji Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Mbaraka Yussuf (Azam FC), Elias Maguri (Huru) na Yohanna Nkomola (Huru). 

KUZIONA SIMBA, YANGA BUKU KUMI, MECHI KUCHEZWA SHAMBA LA BIBI


KIINGILIO cha chini katika mchezo wa mahasimu wa jadi, Simba na Yanga utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Oktoba 28, kitakuwa ni Sh 10,000.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam kwamba kiingilio hicho kitahusu majukwaa ya mzunguko ya Uwanja huo, wakati jukwaa kuu watu watalipa Sh. 20,000.
Kidau amesema kwamba utaratibu maalum umewekwa kuhakikisha idadi inayotakiwa ya watu 22,000 ndiyo wanaoingia uwanjani kwa kuhakikisha haziuzwi tiketi zaidi.
Aidha, kiungo huyo wa zamani wa Simba SC, amesema kwamba imelazimika mchezo huo kufanyika Uwanja wa Uhuru kwa sababu Uwanja mkubwa wa Taifa upo kwenye ukarabati.
Kidau pia amesema kwamba Alhamisi wiki hii Kamati mpya ya Uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) ya TFF itafanya kikao chake cha kwanza mjini Dar es Salaam, kubwa likiwa ni maandalizi ya mchezo huo.
Lakini pia, Kidau amesema kwamba ajenda nyingine katika kikao hicho ni kuteua Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, na Kamati nyingine mbalimbali.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau amesema kiingilio cha chini Simba na Yanga ni Sh. 10,000

YANGA YATOA DOZI YA 4G KWA STAND UNITED



YANGA SC wameonyesha wapo tayari kutetea ubingwa, baada ya leo kuwafumua mabao 4-0 wenyeji Stand United kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Shujaa wa Yanga  alikuwa mshambuliaji mpya, Ibrahim Hajib Migomba aliyefunga mabao mawili na kuseti moja, lililofunga na Obrey Chirwa wakati bao lingine la wana Jangwani hao limefungwa na kiungo Pius Buswita.
Kwa matokeo hayo, Yanga inafikisha pointi 15 baada ya kucheza mechi saba na kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakizidiwa kwa wastani wa mabao tu ya kufunga na kufungwa na Simba SC wenye pointi 15 pia sawa na Mtibwa Sugar walio nafasi ya tatu.

Sunday, October 22, 2017

SIMBA YAIPA KISAGO MJI NJOMBE



SIMBA jana iliendelea kuchanja mbuga katika kuwania ubingwa wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuicharaza Mji Njombe mabao 4-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, mabao ya Simba yalifungwa na Muzamir Yassin, aliyetupia mabao mawili, Emmanuel Okwi na Laudit Mavugo.

Kwa matokeo hayo, Simba bado ipo kileleni mwa ligi hiyo, ikiwa na pointi 15, sawa na Mtibwa Sugar, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo wakati Yanga itakapomenyana na Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.


Saturday, October 21, 2017

DAKTARI ASEMA ALIMKUTA KANUMBA AKIWA AMESHAKUFA




DAKTARI wa familia ya msanii maarufu wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba, Dkt, Paplas Kagaia, ameileza mahakama Kuu ya Tanzania kanda Dar es Salaam Kanumba alifariki toka nyumbani baada ya kumpima na kukuta mapigo yake ya moyo hayakuwepo.
Dk, Paplas amedai hayo leo Oktoba 20, 2017 huu wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Sam Rumanyika.
Amedai kuwa, baada ya mdogo wa marehemu kumfuata hospitali kwake na kumwambia kuwa Kanumba amefariki, alichukua kipino cha sukari na shindikizo la Damu(pressure) na kwenda moja moja nyumbani kwake Sinza ambako baada ya kufika nyumbani kwake alimpima sukari na kukuta io kawaida lakini alipompima pressure haikuwepo kabisa.

Daktari Huyo mwenye elimu ya stashada ya juu (Advance diploma) aliyejipatia Elimu yake chuo cha uuguzi cha jeshi cha Lugalo amedai kuwa, alikuwa daktari wa familia ya Kanumba kwa zaidi ya miaka mitano na anamiliki Hospitali yake binafsi ya St. Anna iliyopo Manzese jijini Dar es Salaam alikuwa akimtibu Kanumba magonjwa ya kawaida na hakuwahi kugundua tatizo lake lolote.

Mahojiano kati ya Dr Paplas na Wakili wa serikali Batlida Mushi yalikuwa kama ifuatavyo;

Wakili: Ulipata wapi taarifa kama ya kuugua kwa Kanumba?
Shahidi: Nikiwa naudumia wagonjwa kama kawaida nilipigiwa simu na Seth akiniomba niende kumuona Kanumba amedondoka, nikamwambia muda ule ulikuwa ni usiku sana aende kumchukua.

Wakili: kwani nini Seth akupigie wewe simu?
Shahidi: Nilikiwa daktari wa familia yao kwa miaka kama mitano hadi sita.

Wakili: Baada ya kukupigia simu, ulifanya nini?
Shahidi: Nilichukua vifaa vya mashine ya sukari na BP, niliingia chumbani kwake nikifuatana na Seth nilipofika nilikuta Kanumba amelala chini chali, nikampima sukari ilikuwa normal nikampima pressure mapigo ya moyo hayakuwepo kabisa.
Wakili:Baada ya kujua mapigo ya moyo hayapo ulifanya ulichukua hatua gani?
Shahidi: Nilimwambia Sethi Fanya umvalishe nguo wafanye utaratibu wa kumpeleka hospitali kubwa ya Muhimbili akafanyiwe Vipimo.

Wakili: Baada ya hapo ulifanya nini?
Shahidi: Baada ya kumvalisha nguo kwa kisaidiana na kijana mmoja wa jirani na mama mwenye nyumba tulimpeleka Muhimbili kitengo cha emergency.
Wakili: Mlipofika Muhimbili kitengo cha Emergency ulifanya nini?
Shahidi: Nilimuomba Dk tuliyemkuta pale ampime Kanumba na alipompima alisema kuwa ameshafariki.

Wakili: Wakati huo anapimwa mlikuwa mahali gani?
Shahidi: Alimpima pale pale nje hata ndani hatukuingia, alitushauri tufuate taratibu za polisi, alituambia twende Kituo cha polisi cha Slender Bridge tukachukue PF3.

Wakili: Mlipokuwa Polisi nini kiliendelea?
Shahidi: Tulipewa askari ili watusaidie kupeleka maiti Mochuari kisha tukaambiwa twende Kituo Osterbay Polisi tukatoe Maelezo.

Wakili: Unamfahamu Lulu?
Shahidi: Ndiyo
Wakili: Unamfahamuje?
Shahidi: Nimemfahamu kwa kupitia Kanumba.

Wakili: Unamfahamu kama nani?
Shahidi: Alikuwa mpenzi wake Marehemu Kanumba.
Wakili: Je Aprili 7 mwaka 2012 baada ya wewe kwenda Polisi Osterbay ulimuona?
Shahidi: Hapana sikumuona.

Wakili: ulimuonea wapi?
Shahidi: Nilimuona usiku kwenye saa 11 alikuwa Sinza sehemu moja inaitwa Bamaga, baada ya yeye kunipigia simu.

Baada ya kumaliz kutoa ushahidi wake kwa upande wa mashtaka wakili wa utetezi, Peter Kibatala naye alipata nafasi ya kumuhoji shahidi huyo ambapo mahojiano yao yalikuwa hivi;
Wakili Kibatara: Kwa nini ulipofika eneo la tukio ulimpima Sukari?
Shahidi: mtu akianguka ghafla Mara nyingi sukari inaweza kuwa imeshuka
Wakili Kibatala, kabla ya Octoba 7 uliwahi kumfanyia uchunguzi marehemu kuhusu sukari.
Shahidi: Hapana
Wakili: Uliwahi kumfanyia vipimo kama anauvimbe kichwani
Shahidi: hapana.
Wakili: je ulimkuta na jeraha lolote?
Shahidi hapana.
Wakili Kibatara: Ni sahihi kuwa mshtakiwa alikuwa anakupigia simu Mara kwa Mara?
Shahidi: Ni sahihi kweli alikuwa akinipigia hata kabla hajaenda hospitali.

Wakili Kibatara:Ni sahihi kwamba mshtakiwa alikuwa anakupigia simu Mara kwa Mara akifikiria kuwa marehemu alikuwa amezimia tu?
Shahidi; Ndiyo ila alikuwa na hofu kama marehemu amekufa.

Wakili Kibatara: Ni sahihi kuwa mshtakiwa alikuwa anaogopa kuonana na wewe kwa sababu alidhani uko na marehemu na ulikuwa na mtego tu wa kumkamata ili andeleze tabia yake ya wivu uliopindukia?
Shahidi: hapana.
Wakili Kibatala: umesema, mlikutana na mshtakiwa Bamaga, kwa nini mshtakiwa alikubali kuonanana wewe Bamaga?, Ni ushawishi gani ulimwambia hadi akakubali kuja?
Shahidi: alikubali tukutane Bamaga alikuwa hajui kwamba Kanumba ameshafariki, yeye ndio alinipigia simu akasema si umesema Kanumba hajafa nikamwambia ndio akasema tukutane Sinza nikasema tukutane Bamaga.

Naye shahidi wa tatu, mrakibu msaidizi wa Polisi PF 16519 ASP Ester Zefania akitoa ushahidi wake huku akiongozwa na wakili wa Serikali,  Ayoub Abood amedai, Oktoba 7, 2012 akiwa kituoni Osterbay alipewa maelekezo na Mkuu wa upelelezi Wa mkoa Wa Kinondoni Camilius wambura kwenda Sinza kwa Kanumba kufuatilia taarifa alizopata za kifo cha Kanumba.

Amedai aliondoka na askari watatu pamoja na msanii Ray ambaye aliwaongoza hadi kwa Sinza kwa marehemu ambako alikuta watu wengi wengine wakilia kuashiria hali ya msiba mahojiani yake na Wakili Abood yalikuwa hivi;
Wakili: Baada ya kufika hapo nyumbani ulifanya nini?
Shahidi : Nilijitambulisha wa watu waliokuwepo pale kuwa Mimi ni askari kutoka kituo cha polisi cha Osterbay, nikaitiwa mdogo wake Kanumba Seth, ambapo nilipomuuliza nini kilitokea alinielezea kwa kifupi.
Baada ya hapo mimi pamoja na askari 2 pamoja na Ray tulioingia chumbani kwa marehemu kwa ajali ya uchunguzi.

Wakili : Baada ya kuingia humo chumbani ulikuta hali gani? na  mliweza kuona kitu gani katika chumba hicho?
Shahidi:Kitanda kilikuwa kimevurugwa, pembeni yake kulikuwa na stuli juu yake ilikuwa na chupa ya soda aina ya Sprite, glass iliyokuwa na kinywaji nusu na chupa ya whisky ya Jackie Daniel, pia pembeni chini ya tendegu za kitanda kulikuwa na panga na pembeni yake kulionekana michirizi ya mburuzo wenye rangi kama nyeusi isiyokolea.

Wakili: Baada ya hapo nini kilitokea?
Shahidi: Nilimpigia simu kamanda Wambura na kumpatia taarifa ambaye aliniambia angetuma timu ya wapelelezi wa matukio kutoka mkoani na eneo la tukio libaki vilevile.

Wakili: Baada ya kufika wakuu wa upelelezi ulifanya nini?
Shahidi: Nilindoka nikarudi kituoni.

Wakili: Baada ya kufika kituoni ulimkuta nani?
Shahidi; Nilimkuta kamanda Wambura ambaye alinipa (task) jukumu la kumtafuta Lulu apelekwe kituoni hapo kwani kwa taarifa alizokuwa nazo atakuwa anafahamu nini kilimpata Kanumba.

Wakili: Alikupa Huyo Daktari kwa ajili gani?
Shahidi; Alinipa Daktari Paplas ili tusaidiane nae kumpata Lulu kwani ndio alikuwa akiongea naye  Mara nyingi ambapo alimpigia simu na kukubaliana kukutana nae bamaga ndipo waliweza kumkamata.
Wakili Kibatala nae alimhoji mrakibu msaidizi wa Polisi PF 16519 ASP Ester Zefania mahojiano yao yalikuwa hivi;

Wakili Kibatala: Mlipomkamata Lulu mlimpeleka hospitali?
Shahidi; NdioWakili Kibatala: Mlimpeleka Lulu hospitali kutibiwa nini?
Shahidi: sifahamu, sikuingi kwa kwenye chumba cha daktari.Wakili Kibatala: Ni sahihi kwamba sababu ya kupelekwa Lulu kwa daktari kuwa alipigwa na ubapa wa panga mapajani na alikuwa na maumivu
Shahidi; Sifahamu.

Kesi hiyo itaendelea Oktoba 23, 2017( Jumatatu) na shahidi wa nne atatoa ushahidi wake.

LIGI KUU BARA USHINDANI KILA KONA

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), inatarajiwa kuendelea kesho Ijumaa Oktoba 20, 2017 kwa mchezo mmoja utakaokutanisha timu za Mwadui na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mwadui mkoani Shinyanga.

Timu hizo zinakutana katika Raundi ya Saba katika duru hili la kwanza la VPL ambalo mbali ya Kampuni ya Simu ya Vodacom - wadhamini wakuu, wadhamini wengine ni Kituo cha Televisheni cha Azam (Azam Tv) na Benki ya KCB ambayo huduma zake za kibenki zinazidi kushamiri nchini.

Wadhamini hao wanachagiza ligi hiyo ambayo itaendelea Jumamosi Oktoba 21 kwa michezo sita  itakayofanyika kwenye viwanja tofauti huku mechi nyingi zikipata fursa ya kuonyeshwa kwenye chaneli mbalimbali za Azam Tv kupitia king’amuzi cha Azam.

Michezo ya Jumamosi itakutanisha timu za Mbao na Azam kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wakati Lipuli itakuwa mwenyeji wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa ilihali Ruvu Shooting watakuwa wageni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Jumamosi hiyo hiyo Simba yenye mabadiliko kidogo kwenye benchi la Ufundi, itawaalika Njombe Mji kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku Ndanda ikicheza na Singida United kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Wakati Jumamosi hiyohiyo tena, Mtibwa Sugar wakicheza na Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro, Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja tu - ambao ni kati ya Stand United na mabingwa watetezi, Young Africans ya Dar es Salaam - mchezo utakaopigwa Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

LIGI DARAJA LA KWANZA KUENDELEA WIKIENDI HII
Raundi ya Sita ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL), itaendelea  kesho Ijumaa Oktoba 20, 2017 kwa mechi za makundi yote matatu.

Katika Kundi ‘A’, Mvuvumwa FC ya Kigoma, watacheza na Mgambo JKT katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Mvuvumwa anatumia Kanuni ya 6 (1) na (2) kuhamishia mechi zake za nyumbani Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kutoka Uwanja wa Tanganyika, Kigoma.

Mechi nyingine kwenye kundi hilo itafanyika Jumapili Oktoba 22, mwaka huu kwa michezo mitatu.

Mechi hizo ni kati ya  Kiluvya United  na Mshikamano  kwenye Uwanja wa Filbert Bayi, ilihali African Lyon  itacheza na Ashanti United  kwenye Uwanja wa Uhuru wakati Friends Rangers itapambana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam, Dar es Salaam.

Katika Kundi ‘B’ siku hiyo ya Ijumaa Oktoba 20, mwaka huu Polisi Dar itacheza na Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Azam wakati michezo mingine katika kundi hilo ikichezwa Jumamosi na  Jumapili.

Jumamosi Mbeya Kwanza itacheza na JKT Mlale Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani na Jumapili Polisi Tanzania watawakaribisha KMC kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Ushirika Moshi, huku Mawenzi Market ya Morogoro wakiwaalika Mufindi United kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Katika Kundi ‘C’ kutakuwa na mchezo mmoja siku ya Ijumaa Oktoba 20, 2017 Pamba SC ya Mwanza itacheza na Alliance Schools nayo ya Mwanza kwenye Uwanja wa Nyamagana huko Mwanza na michezo mingine itafanyika Jumamosi na Jumapili.

Michezo ya Jumamosi  itazikutanisha Biashara Mara dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Karume Mara,Transit Camp itakuwa mwenyeji wa Dodoma FC kwenye Uwanja wa Kambarage Mjini Shinyanga,wakati mchezo mwingine wa Kundi C, Toto Africans ya Mwanza itacheza  na Rhino Rangers ya Tabora katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

WANAWAKE 28 WAHITIMU KOZI YA UKOCHA TFF

Makocha 28 wanawake kutoka vyuo mbalimbali vya Maendeleo ya Jamii nchini leo Oktoba 17, 2017 wamehitimu kozi fupi ya ukocha katika kozi iliyoratibiwa kwa pamoja kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Taasisi ya Karibu Tanzania (KTO).

Kozi hiyo ya siku mbili ambayo ni ya pili kufanyika kwa makocha hao, iliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume - Makao Makuu ya TFF ilikuwa chini ya mkufunzi wa TFF, Raymond Gweba.

Akizungumza kwenye ufungaji wa kozi hiyo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo amesema Serikali inafahamu kuwa inatakiwa kuwekeza kwenye soka la wanawake kuanzia upande wa vijana na ndio maana inatengeneza mazingira na sera zitakazowezesha mafanikio hayo.

Singo amesema nchi mbalimbali wana maendeleo makubwa katika mpira wa miguu kwa wanawake na sasa wakati wa Tanzania kuwekeza katika upande huo kuanzia kwa watoto na makocha.

Kadhalika, Singo amewataka wahitimu kuchukuwa mafunzo hayo kwa uzito mkubwa kwa sababu mpira wa miguu ya ajira na elimu hiyo itaongeza kitu kikubwa kwao.

Naye, Mwenyekiti wa Chama Mpira wa la Wanawake (TWFA), Amina Karuma amesema lengo la chama chake na TFF kuhakikisha soka linachezwa nchi nzima linaelekea kutimia.

Amewataka wahitimu hao wa kozi hiyo fupi kuvitumia vyeti walivyovipata kuendeleza soka la wanawake na kufanyia kazi yale yote waliyofundishwa.

Pia ameiomba Serikali kuwaunga mkono katika maendeleo ya soka la wanawake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ufundi wa TFF Salum Madadi amesema kufundisha watoto kuna changamoto nyingi, lakini makocha hao wamefundishwa maarifa ya jinsi ya kukabiliana nazo.

Amesema maarifa hayo sio makocha wote wanaweza kuyapata lakini wameona umuhimu mkubwa kwa wahitimu hao kuweza kuyapata ili kwenda kuibua vipaji kuanzia chini.

Wahitimu wa kozi hiyo wamepatiwa vyeti vya ushiriki na vifaa vya michezo ikiwemo koni na mipira.

Friday, October 13, 2017

TFF YATAWATOA MAKOCHA KATIKA MABENCHI



Bodi ya Ligi (TPLB) ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, limewapiga marufuku makocha watano wa timu za Ligi Daraja la Kwanza kukaa katika mabenchi ya timu hizo kwa sababu ya kukosa sifa.


Makocha hao ni Mathias Wandiba wa Pamba FC ya Mwanza, Salum Waziri wa JKT Mgambo ya Tanga, Adam Kipatacho wa African Lyon ya Dar es Salaam, Omba Thabit wa Mvuvumwa FC ya Kigoma na Ngelo Manjamba wa Polisi Dar.


Makocha hao wamekuwa kwenye mabenchi ya timu wakifanya kazi kama makocha wakuu katika mechi nne mfululizo za Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2017/2018 inayoendelea hivi sasa.


Kwa mujibu wa kanuni ya 72 (3) (5) ya Ligi Daraja la Kwanza, Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na Leseni ya chini kuanzia daraja C ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) wakati Kocha Msaidizi anatakiwa kuwa na  sifa isiyopungua ngazi ya Kati cha Ukocha (Intermediate).


Tayari Idara ya Ufundi ya TFF imefafanua wazi kuwa makocha hao hawana Leseni C ya CAF hivyo hawastahili kukaa kwenye mabenchi ya timu zao kama makocha wakuu.


Vitendo vinavyofanywa na timu husika ni ukiukwaji wa kanuni, na ni matarajio ya TFF kuwa viongozi wa timu hizo watasitisha mara moja kwa makocha hao kukaa kwenye mabenchi ili kuepika adhabu.


TFF tunachukua nafasi hii kuzikumbusha klabu husika  kwamba kuanzia msimu ujao 2018/2019 kuwa sifa ya Kocha Mkuu wa kila timu ya Daraja la Kwanza ni Leseni B ya CAF.


PATASHIKA LIGI VPL, FDL, SDL WIKIENDI HII


Baada ya kupisha wiki ya FIFA kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa ukihusisha Taifa Stars ya Tanzania na Miale ya Moto kutoka Malawi iliyotoshana nguvu ya bao 1-1, uhondo wa mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili, umerejea.


Kwa upande wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea wikiendi hii ambako kesho Oktoba 13, 2017 kutakuwa na mchezo mmoja tu utakaokutanisha timu za Mbao FC na Mbeya City kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Dar es Salaam.


Timu hizo ziko katika nafasi za katikati katika msimamo wa VPL, lakini ushindani unatarajiwa kuwa kwa timu za Simba SC, Mtibwa FC na Azam ambazo kila moja ina pointi 11 na ziko kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa tu.


Katika michezo ya Jumamosi Oktoba 14, 2017 Azam FC itakuwa mgeni wa Mwadui FC kwenye Uwanja wa Mwadui wakati Kagera Sugar itawaalika mabingwa watetezi, Young Africans kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.


Ndanda itakuwa nyumbani kucheza na majirani zao Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara wakati Singida United itasafiri hadi Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi kucheza na wenyeji Ruvu Shooting ya Pwani.


Majirani wengine, Njombe Mji na Lipuli ya Iringa watacheza kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe ilihali michezo mingine ya Ligi hiyo ikifanyika Jumapili Oktoba 15, ambako Simba itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati Tanzania Prisons itacheza na Stand United kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.


Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo itaendelea ambako kesho kutakuwa na mchezo kati ya African Lyon na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Timu hizo ni za Kundi A.


Mechi nyingine kwenye kundi hilo itafanyika Jumamosi ambako Ashanti United itacheza na Mvuvumwa ya Kigoma kwenye Uwanja wa Uhuru ilihali Jumatatu Oktoba 16, Kiluvya itacheza na Friends Rangers kwenye Uwanja wa Uhuru huku Mgambo JKT ikishikamana na Mshikamano kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.


Kundi B kwa mujibu wa ratiba ni kwamba kesho Ijumaa JKT Mlale itacheza na Polisi Dar kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea huku michezo mingine katika kundi hilo ikicheza Jumapili kwa michezo mitatu.


Siku hiyo Mbeya Kwanza itacheza na Mawenzi Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani, Coastal na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mufindi United itacheza na KMC Uwanja wa Samora mkoani Iringa.


Kundi C litakuwa na mchezo mmoja siku ya Jumamosi  Oktoba 14, 2017 ambako Toto African itakipiga na Pamba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na michezo mingine mitatu itafanyika siku ya Jumapili Oktoba 15, mwaka huu.


Michezo ya Jumapili itakuwa ni kati ya Dodoma FC dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma; Rhino Rangers itacheza Biashara United wakati mchezo wa Alliance Schools na Transit Camp utachezwa kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.


Ligi Daraja la Pili (SDL), Jumapili Oktoba 15, 2017 Kundi A kutakuwa mchezo kati ya Villa Squad na Abajalo FC Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam.


Jumamosi kutakuwa na michezo miwili ya Kundi B ambako African Sports itacheza na Pepsi kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga huku Arusha FC itacheza na Kitayose kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.


Jumapili Oktoba 15, 2017 katika kundi B hilo la B kutakuwa na mchezo mmoja kati ya Madini na Kilimanjaro Heroes kwenye Uwanja wa Nyerere mkoani Arusha.


Kundi C kutakuwa na michezo yote mitatu ya raundi ya tatu ambako Ihefu itacheza na Green Warriors kwenye Uwanja wa Highland; Mkamba Rangers itacheza na The Mighty Elephant kwenye Uwanja wa Mkamba huko Morogoro ilihali Boma FC dhidi ya Burkinafaso zitacheza Uwanja wa Mwakangale, Mbeya.


Kundi D pia kutakuwa na mechi zote tatu Oktoba 14, 2017 ambako Nyanza itacheza na Mashujaa kwenye Uwanja wa Nyerere; Area ‘C’ United itacheza na Milambo Uwanja wa Jamhuri Dodoma wakati JKT Msange itacheza na Bulyanhulu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.


NI ZAMU YA WAAMUZI DARAJA I NA II


Baada ya mtihani wa utimamu wa mwili kwa waamuzi wenye beji za FIFA na wale wa Daraja la Kwanza kufanyika Agosti, 2017, sasa ni zamu ya waamuzi wa madaraja ya Tatu na Pili.


Waamuzi wa madaraja ya Tatu na Pili kuanzia leo Alhamisi Oktoba 12, 2017 wameanza vipimo kabla ya  mitihani ya utimamu wa mwili katika vituo viwili vya Dar es Salaam na Mwanza. 


Kwa wale watakaopata matokeo mazuri, watapata fursa ya kupandisha madaraja kwa mujibu wa utaratibu.


Zoezi hilo litajumuisha pia wale waamuzi wa Daraja la Kwanza walioshindwa mitihani hiyo mwezi Agosti, mwaka huu. Hivyo nao wanaruhusiwa kwenda kufanya mitihani tena.


Kituo cha Dar es Salaam kitakuwa na waamuzi wa mikoa ya Dar es Salaam yenyewe, Pwani, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya, Rukwa na Songwe.


Kituo cha Mwanza kitakuwa na waamuzi wa mikoa ya Mwanza yenyewe, Mara, Kagera, Simiyu, Geita, Kigoma, Arusha, Shinyanga, Tabora, Dodoma, Singida, Manyara na Katavi.


Waamuzi wote waende kwenye vituo vyao walivyopangiwa kama ilivyoelekezwa Oktoba 12, 2017 - ni siku ya kupima afya kabla ya kuanza kwa mitihani mingine ukiwamo wa utimamu wa mwili hapo kesho.

BEKI SINGIDA UTD MCHEZAJI BORA SEPTEMBA, 2017



Mchezaji wa timu ya Singida United, Shafik Batambuze  amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2017/2018.


Batambuze anayecheza nafasi ya ulinzi wa pembeni, alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Ibrahim Ajibu wa Yanga na kiungo Mohammed Issa wa Mtibwa Sugar, alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam.


Uchambuzi huo kwa mujibu wa utaratibu hufanywa na kikao cha Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.



Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa Singida United kupata pointi 10 katika michezo minne, ambayo timu yake ilicheza kwa mwezi huo, matokeo ambayo yaliiwezesha Singida United kutoka nafasi ya 10 katika msimamo na kupanda hadi nafasi ya nne kwa mwezi huo wa Septemba. Singida United ndiyo timu iliyokusanya alama nyingi kwa mwezi huo ukilinganisha na timu nyingine 15 zinazoshiriki VPL.


Singida United iliifunga Mbao FC mabao 2-1 Uwanja wa Jamhuri Dodoma,  ikaifunga Stand United bao 1-0 Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, iliifunga Kagera Sugar Uwanja wa Jamhuri Dodoma na ilitoka sare ya bao 1-1 na Azam FC uwanja huo huo. Michezo yote hiyo Batambuze alicheza dakika zote 90 kwa kila mchezo, ambayo ni sawa na kucheza dakika 360.


Kwa upande wa Ibrahim Ajibu alitoa mchango mkubwa kwa Yanga uliowezesha kupata pointi nane kwa mwezi huo, baada ya kushinda michezo miwili na kutoka sare miwili, ambapo pia Mohammed Issa aliisaidia timu yake kupata pointi nane katika michezo minne iliyocheza mwezi huo, ikishinda miwili na kutoka sare miwili.


Kampuni ya Vodacom, ambao ndiyo wadhamini wa ligi hiyo ina utaratibu wa kuwazawadia wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2016/2017 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali. Batambuze atazawadiwa Sh milioni moja kwa kuibuka Mchezaji Bora wa mwezi.

MALALAMIKO YA PEPSI YAMEKATALIWA



Malalamiko ya Pepsi dhidi ya Madini kuwa timu hiyo ilimtumia mchezaji Shabani Imamu kwenye mechi yao ya Ligi Daraja la Pili (SDL) iliyochezwa Septemba 30 mwaka huu Uwanja wa  Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini wakati akiwa na adhabu ya kutumikia kadi nyekundu yamekataliwa.

Kamati imebaini kuwa mchezaji huyo alishatumikia adhabu ya kukosa mechi moja wakati wa mchezo wa SDL kati ya Madini na JKT Oljoro uliochezwa Februari 6 mwaka huu.

Mchezaji huyo alioneshwa kadi ya pili ya njano msimu uliopita kwenye mechi kati ya Madini na AFC iliyofanyika Januari 31 mwaka huu, na kukosa mechi moja iliyofuata kati ya Madini na JKT Oljoro ya Februari 6 mwaka huu, hivyo kuwa halali kwenye mechi ya Pepsi na Madini iliyochezwa Septemba 30 mwaka huu.

Kocha Msaidizi wa Area C United, Omarooh Omari amesimamishwa kukaa kwenye benchi la timu yake wakati akisubiri suala lake la kumpiga kiwiko mchezaji wa Nyanza FC kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.


Alimpiga kiwiko mchezaji wa Nyanza, Rajab Adam alipokuwa akikimbilia mpira uliopita karibu yake. Pia dakika ya 78 alianzisha tena vurugu na Mwamuzi kumtoa kwenye benchi la ufundi lakini aligoma kutoka hadi alipotolewa na askari polisi.


Alifanya vitendo hivyo vya utovu mkubwa wa nidhamu wakati wa mechi kati ya Ligi Daraja la Pili kati ya timu yake na Nyanza iliyochezwa Oktoba 1 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyerere uliopo Mbulu mkoani Manyara.

Uamuzi wa kumsimamisha umefanywa kwa kutumia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Pili.



KUSIMAMISHWA MCHEZAJI JOHN BARAKA WA AREA C



Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake kilichopita ilipitia taarifa na matukio mbalimbali ya Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili msimu wa 2017/2018 zinazoendelea hivi sasa.



Katika taarifa hizo imebainika kuwa mchezaji wako John Baraka jezi namba 2 alioneshwa kadi nyekundu baada ya mchezo kumalizika kwa kumpiga ngumi mwamuzi ngumi ya mgongoni.



Alifanya kitendo hicho kwenye mechi namba 1 ya Kundi D la Ligi Daraja la Pili kati ya timu yako na Nyanza FC iliyofanyika Oktoba 1 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyerere uliopo Mbulu mkoani Pwani.



Kwa vile suala lake ni la kinidhamu, na kwa kutumia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Kwanza, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imemsimamisha kucheza mechi za SDL hadi suala lake litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).



Mchezaji wako atafahamishwa siku ambayo kikao cha Kamati ya Nidhamu kitafanyika kusikiliza shauri dhidi yake ambapo pia atapata fursa ya kuwasilisha utetezi wake kama upo.



ONYO KALI KWA MKAMBA RANGERS


Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake kilichopita ilipitia taarifa na matukio mbalimbali ya Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili msimu wa 2017/2018 zinazoendelea hivi sasa.


Katika taarifa hizo imebainika kuwa timu yako haikuhudhuria katika kikao cha maandalizi (pre match meeting), na pia ilichelewa kufika uwanjani wakati wa mechi namba 3 ya Kundi C dhidi ya Boma FC iliyochezwa Septemba 30 mwaka huu Uwanja wa Mwakangale uliopo Kyela mkoani Mbeya.


Kitendo hicho ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(2a) na Kanuni ya 14(9) za Ligi Daraja la Pili. Kwa vile ni kosa la kwanza kwa timu yako msimu huu, Kamati imeipa klabu yako Onyo Kali kwa kuamini kuwa kosa hilo la kikanuni halitajitokeza tena. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) na 14 (48) za Ligi Daraja la Pili.


Unakumbushwa kuwa Ligi Daraja la Pili inaendeshwa kwa kuzingatia Kanuni husika, na ni matarajio yangu kuwa ukiwa mtendaji mkuu wa klabu utakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kanuni hizo zinafuatwa kikamilifu.



ONYO KALI KWA KLABU YA REHA



Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake kilichopita ilipitia taarifa na matukio mbalimbali ya Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili msimu wa 2017/2018 zinazoendelea hivi sasa.



Katika taarifa hizo imebainika kuwa timu yako iliwakilishwa na viongozi watatu tu katika kikao cha maandalizi (pre match meeting) wakati wa mechi namba 3 ya Kundi A dhidi ya Namungo FC iliyochezwa Septemba 30 mwaka huu Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.



Kitendo hicho ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Pili. Kwa vile ni kosa la kwanza kwa timu yako msimu huu, Kamati imeipa klabu yako Onyo Kali kwa kuamini kuwa kosa hilo la kikanuni halitajitokeza tena. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.



Unakumbushwa kuwa Ligi Daraja la Pili inaendeshwa kwa kuzingatia Kanuni husika, na ni matarajio yangu kuwa ukiwa mtendaji mkuu wa klabu yako utakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kanuni hizo zinafuatwa kikamilifu.



ONYO KALI BULYANHULU FOOTBALL CLUB


Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake kilichopita ilipitia taarifa na matukio mbalimbali ya Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili msimu wa 2017/2018 zinazoendelea hivi sasa.


Katika taarifa hizo imebainika kuwa timu yako haikuhudhuria katika kikao cha maandalizi (pre match meeting) wakati wa mechi namba 3 ya Kundi D dhidi ya Milambo FC iliyochezwa Oktoba 1 mwaka huu Uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga.


Kitendo hicho ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(2a) ya Ligi Daraja la Pili. Kwa vile ni kosa la kwanza kwa timu yako msimu huu, Kamati imeipa klabu yako Onyo Kali kwa kuamini kuwa kosa hilo la kikanuni halitajitokeza tena. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.


Unakumbushwa kuwa Ligi Daraja la Pili inaendeshwa kwa kuzingatia Kanuni husika, na ni matarajio yangu kuwa ukiwa mtendaji mkuu wa klabu utakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kanuni hizo zinafuatwa kikamilifu.

KOCHA TOTO AFRICANS AZUIWA KUKAA BENCHI



Kocha wa Toto Africans, Almasi Moshi amezuiwa kukaa kwenye benchi la timu yake kutokana na kutokidhi matakwa ya Kanuni ya 72(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu benchi la ufundi.
 

Kwa mujibu wa Kanuni hiyo, Kocha Mkuu wa timu ya Ligi Daraja la Kwanza anatakiwa kuwa na Leseni ya chini kuanzia Daraja C ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).


Klabu ya Mvuvumwa FC imepigwa faini ya sh 100,000 (laki moja) kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi (pre match meeting) ikiwa na maofisa wawili tu badala ya wanne wakati wa mechi namba 5 ya Kundi A la Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Kiluvya United iliyochezwa Septemba 22 mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.


Adhabu dhidi ya klabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo, na kitendo chao cha kuwa pungufu kwenye pre match meeting ni kukiuka Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.


Nayo Toto Africans imepigwa faini ya sh 100,000 (laki moja) kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi (pre match meeting) ikiwa na maofisa watatu badala ya wanne wakati wa mechi namba 10 ya Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Transit Camp FC iliyochezwa Septemba 29 mwaka huu katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.


Adhabu dhidi ya klabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo, na kitendo chao cha kuwa pungufu kwenye pre match meeting ni kukiuka Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.


JKT Oljoro imepigwa faini ya s 100,000 (laki moja) kwa timu hiyo kufika uwanjani ikiwa imechelewa kinyume na Kanuni ya 14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza. Ilifanya kosa hilo kwenye mechi namba 5 ya Kundi la Ligi Daraja la Kwanza katika mechi dhidi ya Pamba iliyofanyika Septemba 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.


Mchezaji Hussein Nyamandulu wa Transit Camp amesimamishwa kucheza wakati akisubiri suala lake la kufanya vurugu kwenye benchi la Toto African kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.


Nyamandulu aliyekuwa amevaa jezi namba 10 alifanya vurugu hizo baada ya mechi dhidi ya Toto Africans iliyofanyika Septemba 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kumalizika. Mchezaji huyo amesimamishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Kwanza.


Timu ya Polisi Dar imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi (pre match meeting) wakati wa mechi yao namba 7 dhidi ya KMC iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu Chamazi Complex, Dar es Salaam.

Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni 14(2) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu dhidi yao imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake kilichopita ilipitia taarifa mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2017/2018 zinazoendelea hivi sasa.

Dodoma FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na timu hiyo kuonesha vitendo vinavyoashiria ushirikina kwa kumwaga vitu kwenye mlango wa kuingilia uwanjani, na pia golikipa namba pili aliweka kitu golini.

Timu hiyo ilifanya vitendo hivyo kabla ya mechi ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Biashara United Mara iliyochezwa Septemba 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.Adhabu yao ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.

Mwamuzi Youngman Malagila ameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi wa Ligi Daraja la Kwanza kutokana na kuchezesha chini ya kiwango mechi kati ya Rhino Rangers FC na JKT Oljoro FC ya Arusha iliyofanyika Septemba 30, 2017 katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Uamuzi dhidi ya Mwamuzi huyo umezingatia Kanuni ya 38(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi. Hivyo, amerejeshwa kwenye Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa hatua zingine.

Nao waamuzi Steven Patrick (Mwamuzi wa Kati) na Msaidizi wake Adrian Kalisa wameondolewa kuchezesha Ligi Daraja la Kwanza kutokana na kuchezesha chini ya kiwango mechi kati ya Pamba na Biashara United Mara iliyofanyika Oktoba 2, 2017 katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Uamuzi dhidi ya Mwamuzi huyo umezingatia Kanuni ya 38(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi. Alama walizopata waamuzi hao kwenye mechi namba 12 haziwaruhusu kuchezesha Ligi hiyo.

MWAMUZI AONDOLEWA LIGI KUU YA VODACOM



Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imemuondoa Mwamuzi Msaidizi Grace Wamara kuchezesha Ligi Kuu ya Vodacom kwa kukosa umakini na kutomsaidia Mwamuzi, hivyo kusababisha akubali bao lenye utata la Stand United dhidi ya Mbeya City.


Wamara alikuwa Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili kwenye mechi hiyo namba 31 iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na wenyeji Stand United kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.


Uamuzi wa kumuondoa Wamara ambaye amerejeshwa katika Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa ajili ya hatua nyingine umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.


Klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na wachezaji wake kuvaa jezi zenye namba tofauti na zile zilizosajiliwa. Wachezaji hao walivaa namba tofauti kwenye mechi namba 40 dhidi ya Simba iliyofanyika Oktoba 1 mwaka huu Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.


Stand United ilikiuka Kanuni ya 60(11) ya Ligi Kuu inayelekeza kuwa kila mchezaji atatumia namba ya kudumu ya jezi iliyosajiliwa na klabu yake wakati wa maombi ya usajili. Adhabu dhidi ya Stand United ni uzingativu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu.


Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh 500,000 (laki tano) kutokana na timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi dhidi ya Mbao FC iliyofanyika Septemba 21 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.


Kitendo hicho cha Simba ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu, na adhabu dhidi yao ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu. Pia Kamishna wa mechi hiyo, Maliki Tibabimale amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo hicho cha Simba.


Singida United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mashabiki wa timu hiyo kuingia uwanjani kushangilia ushindi baada ya mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyofanyika Septemba 23 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.


Adhabu dhidi ya Singida United imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu, wakati kitendo cha mashabiki wao ni kosa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(11) ya Ligi Kuu.


Nayo Stand United imepigwa faini ya jumla ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City na Simba, zote zilichezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.


Katika mechi namba 31 iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu, mashabiki hao waliwafanyia vurugu wachezaji wa Mbeya City wakati wakielekea vyumbani baada ya mchezo kumalizika, kabla ya Polisi kuingilia kati na kuwatawanua.
 

Adhabu hiyo ambayo ni sh. 500,000 (laki tano) kwa kila mechi imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
 

Kamati imeionya klabu ya Stand United endapo vitendo hivyo vitatokea tena haitasita kuichukulia hatua kali zaidi za kikanuni.

UCHAGUZI BODI YA LIGI JUMAPILI HII


Uchaguzi wa Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) unafanyika Jumapili, Oktoba 15 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
 

Wagombea saba wamepitishwa kuwania uongozi wa TPLB baada ya Kamati ya sasa kumaliza muda wote. Kamati mpya ya Uongozi itakayochaguliwa katika uchaguzi huo unaosimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF utakaa madaraka kwa kipindi cha miaka minne.
 

Waliopitishwa kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya orodha ya mwisho iliyotolewa Oktoba 9, mwaka huu ni Clement Andrew Sanga kutoka Yanga na Hamad Yahya Juma wa Mtibwa Sugar wanaowania uenyekiti wa TPLB.
 

Wengine ni Shani Christoms Mligo wa Azam FC ambaye ni mgombea pekee wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti. Nafasi tatu za kuwakilisha klabu za Ligi Kuu kwenye Kamati ya Uongozi zimevutia wagombea wawili; Hamisi Mshuda Madaki (Kagera Sugar) na Ramadhani Marco Mahano (Lipuli).
 

Almasi Jumapili Kasongo kutoka Ashanti United FC ni mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi ya uwakilishi wa klabu za Ligi Daraja la Kwanza. Klabu za Daraja la Kwanza zina nafasi mbili.
 

Klabu za Ligi Daraja la Pili zina nafasi moja kwenye Kamati ya Uongozi ya TPLB, na mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo Edgar William Chibura kutoka Abajalo FC.
 

Jumla ya wajumbe 44 watashiriki Mkutano huo wa uchaguzi wa Baraza Kuu la TPLB. Wajumbe hao ni klabu 16 za Ligi Kuu, klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza na wawakilishi wanne wa klabu za Ligi Daraja la Pili.
 

Nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa kuwakilisha klabu za Ligi Kuu zitapigiwa kura na klabu 16 pekee za Ligi Kuu.

Wednesday, October 4, 2017

AVEVA, KABURU WAZIDI KUSOTA RUMANDE




Na Furaha Omary

UPELELEZI wa kesi inayowakabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange 'Kaburu' bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter akishirikiana na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai, walidai hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hayo walidai mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa kutajwa, ambapo waliomba kuahirishwa hadi tarehe nyingine.

Hakimu Mwambapa aliahirisha shauri hilo hadi  Oktoba 11, mwaka huu, kwa kutajwa na washitakiwa walirudishwa mahabusu.

Mara ya mwisho, upande wa jamhuri uliieleza mahakama kuwa jalada la shauri hilo liko kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), hivyo wanasubiri lirejeshwe ili kujua kinachoendelea na usikilizwaji wa shauri kama DPP atakuwa amejiridhisha na uchunguzi kuwa umekamilika.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matano, yakiwemo ya kutakatisha fedha, hivyo kuwafanya wakae mahabusu kwa kuwa shitaka hilo halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mashitaka mengine yanayowakabili ni  kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha Dola za Marekani  300,000.

Washitakiwa hao wanadaiwa Machi Machi 15, mwaka jana,  walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 5, mwaka jana,  wakionyesha klabu ya Simba inalipa mkopo wa  USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati siyo kweli.

Pia, washitakiwa hao wanadaiwa  Machi 15, mwaka jana, katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe, Ilala, Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo, ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016, wakati akijua ni kosa.

Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29, mwaka jana, Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15, mwaka jana, katika benki ya Barclays, Mikocheni, alijipatia USD 300,000, wakati akijua zimetokana na kughushi.

Nyange anadaiwa kuwa Machi 15, mwaka jana, katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni, alimsaidia Aveva kujipatia USD 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.




Monday, October 2, 2017

YANGA YABANWA MBAVU NA MTIBWA SUGAR, SIMBA YAKWEA KILELENI MWA LIGI KUU



MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita walikwaa kisiki mbele ya Mtibwa Sugar baada ya kulazimishwa kutoka nayo suluhu.

Kutokana na sare hiyo iliyopatikana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Mtibwa iliendelea kushikilia usukani wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi tano huku Yanga ikiwa nafasi ya sita.

Hata hivyo, Mtibwa Sugar ilienguliwa kwenye uongozi na Simba jana, baada ya timu hiyo kongwe kuilaza Stand United mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Ushindi huo uliifanya Simba iongoze ligi hiyo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yake na Mtibwa na Azam, kufuatia kila moja kuwa na pointi 11.

Iliwachukua Simba dakika 17 kuhesabu bao la kwanza kupitia kwa winga wake, Shiza Kichuya, kwa shuti kali la umbali wa mita 20, baada ya kupewa pasi na Erasto Nyoni. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Bao la pili la Simba lilifungwa na Laudit Mavugo dakika ya 47 baada ya kuwatoka mabeki wa Stand United, akiwa amepokea pasi kutoka kwa Haruna Niyonzima.

Stand United ilipata bao la kujifariji dakika ya 52 kupitia kwa Mtasa Munashe kwa njia ya penalti.

Katika mechi nyingine iliyochezwa mwishoni mwa wiki, Azam iligawana pointi na Singida United baada ya kutoka nayo sare ya bao 1-1.

TANZANITE YAPIGWA 6-0 NA NIGERIA


TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake ya vijana wa chini ya umri wa miaka 17, Tanzanite, imetupwa nje ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia baada ya kupigwa mweleka wa mabao 6-0 na Nigeria.

Katika mechi hiyo iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Nigeria ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 4-0.

Kipigo hicho kimeifanya Tanzanite itolewe nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 9-0. Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita mjini Lagos, Tanzanite ilichapwa mabao 3-0.