KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, December 9, 2011

DILUNGA, MAHADHI WALIWEKA HISTORIA TANZANIAMSHAMBULIAJI Maulid Dilunga wa Yanga na kipa Omar Mahadhi wa Simba ni wachezaji pekee wa Tanzania walioweka historia ya kuteuliwa kuunda kikosi cha Afrika.
Uteuzi huo ulifanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mara baada ya kumalizika kwa michezo ya All Africa Games, iliyofanyika mwaka 1973 mjini Lagos, Nigeria.
Katika michezo hiyo, Taifa Stars ilifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali. Katika mechi za awali, Stars ilitoka suluhu na Nigeria A, ikaichapa Nigeria B mabao 2-1 kabla ya kuzifunga Ghana na Togo bao 1-0 kila moja.
Katika hatua iliyofuata, Stars ilitoka suluhu na Nigeria, ikatoka sare ya bao 1-1 na Misri kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Algeria.
Dilunga ndiye aliyeibuka mchezaji nyota wa Taifa Stars katika michezo hiyo baada ya kuifungia mabao yote katika kila mechi.
Licha ya Stars kutolewa hatua ya nusu fainali, Dilunga na Mahadhi hawawezi kuisahau michezo hiyo kutokana na kuteuliwa kwenye kikosi cha kombani ya Afrika.
Mara baada ya uteuzi huo, kikosi hicho kilifanya ziara katika mataifa sita ya Ulaya na Amerika, ambako kilicheza mechi kadhaa za kirafiki.
Baadhi ya mataifa hayo ni Mexico, Guatemala, Uruguay, Peru, Hungary na Bulgaria. Katika ziara hiyo, kikosi hicho cha Afrika kilishinda mechi tatu, kilitoka sare mbili na kufungwa moja.
Uteuzi wa Dilunga kwenye kikosi hicho uliingia utata baada ya kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT) wakati huo, kudhani mchezaji aliyeteuliwa ni Abdalla Kibadeni.
Katika taarifa yake kwa FAT, CAF ilisema inamhitaji mchezaji aliyekuwa akivaa jezi namba 10. Na katika kikosi cha Stars wakati huo, wachezaji waliokuwa wakivaa jezi hiyo ni Dilunga na Kibadeni.
Ikabidi FAT iombe ufafanuzi kwa CAF na ndipo ilipobainika kwamba, mchezaji aliyekuwa akihitajika ni Dilunga na siyo Kibadeni.
Kilichoivutia CAF kumteua Dilunga kwenye kikosi hicho ni uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao, hasa katika mechi yao dhidi ya Nigeria B, ambapo alipachika wavuni mabao mawili.
Dilunga pia aliwahi kupata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa Ulaya mwaka 1970 wakati timu ya daraja la pili ya West Bromwich ya England ilipofanya ziara nchini.
Hata hivyo, kuna madai kuwa, aliyekuwa mwenyekiti wa FAT wakati huo, Saidi Hamad El-Maamry alimzuia kwenda huko ili aweze kuichezea Taifa Stars katika michuano ya kimataifa.
Viongozi wa West Bromwich walikuja nchini wakiwa wageni wa Yanga na baada ya kucheza mechi moja ya kirafiki, walivutiwa na uwezo wa Dilunga.
Mbali na kuzuiwa na El-Maamry kwenda Uingereza, mwamko mdogo kwa wanasoka wa Tanzania kwenda kucheza soka ya kulipwa nje nao ulichangia kumfanya Dilunga apuuze mwito huo.

Taifa Stars, Simba, Yanga hazijawakuna Watanzania

KIKOSI cha Taifa Stars

KIKOSI cha Simba


KIKOSI cha Yanga


TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars haina rekodi kubwa ya kujivunia katika michuano ya Afrika. Rekodi pekee ilizoweza kufikia ni kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980 na fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CAN) mwaka 2010.
Mshambuliaji Peter Tino ndiye aliyeiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 1980 baada ya kuifungia bao la kusawazisha katika mechi ya marudiano dhidi ya Zambia.
Katika mechi ya awali kati ya timu hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Thuweni Ally.
Katika mechi ya marudiano iliyochezwa mjini Ndola, Zambia ilikuwa mbele kwa bao 1-0 hadi Tino alipoifungia Taifa Stars bao la kusawazisha na hivyo kuiwezesha kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.
Hata hivyo, Taifa Stars haikuweza kufanya vizuri katika fainali za michuano hiyo zilizochezwa mjini Lagos, Nigeria baada ya kufungwa mechi mbili na kuambulia sare mechi moja.
Katika mechi yake ya kwanza, Taifa Stars ilikubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Nigeria. Mabao ya Nigeria yalifungwa na Lawal, Onyedika na Odegbami wakati bao la kujifariji la Taifa Stars lilifungwa na Thuweni.
Taifa Stars ilikubali tena kipigo katika mechi yake ya pili dhidi ya Misri, ambapo ilichapwa mabao 2-1. Mabao ya Misri yalifungwa na Hassan Shehata na Mosaad Nour wakati bao la Stars lilifungwa na Thuweni.
Katika mechi yake ya mwisho, Taifa Stars iliilazimisha Ivory Coast kutoka nayo sare ya bao 1-1. Bao la Ivory Coast lilifungwa na Kobenan wakati lile la Stars lilifungwa na Thuweni.
Kufuatia matokeo hayo, Taifa Stars ilimaliza mechi za kundi lake ikiwa ya mwisho baada ya kuambilia pointi moja wakati Nigeria ilishika usukani kwa kuwa na pointi tano.
Hatua nyingine ya juu iliyofikiwa na Taifa Stars katika michuano ya kimataifa ni kufuzu kucheza fainali za CAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast baada ya kuitoa Sudan.
Katika mechi yake ya kwanza, Taifa Stars ilipigwa mweleka wa bao 1-0 na Senegal kabla ya kuibuka na ushindi wa idadi hiyo ya bao dhidi ya Ivory Coast.
Hata hivyo, matumaini ya Stars kusonga mbele yalizimwa na Zambia baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1. Zambia ndiyo iliyoongoza kundi hilo na kufuzu kucheza nusu fainali.
Rekodi nyingine ya kujivunia kwa Taifa Stars ni kufuzu kucheza hatua ya nusu fainali katika michezo ya All Africa Games iliyofanyika mwaka 1973 mjini Lagos, Nigeria.
Katika michuano hiyo iliyochezwa kwa mtindo wa ligi, Taifa Stars ilitoka sare mechi mbili dhidi ya Nigeria na Misri na kufungwa mechi ya mwisho mabao 2-1 na Algeria.
Kabla ya hatua hiyo, Taifa Stars ilitoka suluhu na Nigeria A, ikaichapa Nigeria B mabao 2-1 kabla ya kutoa kipigo cha bao 1-0 kwa Ghana na Togo. Mshambuliaji Maulid Dilunga ndiye aliyeibeba Taifa Stars baada ya kuifungia mabao yote kwenye michuano hiyo.
Taifa Stars haijawahi kufika hatua za mbali katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia. Mara zote ilizoshiriki, imekuwa ikitolewa aidha raundi ya kwanza ama ya pili.
Katika michuano ya Kombe la Chalenji, Tanzania Bara ililitwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1974 kabla ya kusubiri kwa miaka 20 na kulitwaa tena mwaka 1994. Bara ilitwaa kombe hilo kwa mara ya mwisho mwaka 2010 baada ya kuifunga Ivory Coast bao 1-0 kwa njia ya penalti katika mechi ya fainali.
Kwa upande wa timu za taifa za vijana, hatua pekee ya juu ilifikiwa na timu ya vijana wa chini ya miaka 17, Serengeti Boys mwaka 2004, ilipofuzu kucheza fainali za Afrika baada ya kuitoa Zimbabwe.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), liliiengua Serengeti Boys kushiriki kwenye fainali hizo zilizofanyika Gambia baada ya kubainika kuwa, ilimchezesha mchezaji Nurdin Bakari, ambaye umri wake ulikuwa zaidi ya miaka 17.
Mbali na Serengeti Boys kuenguliwa kwenye fainali hizo, CAF pia iliifungia Tanzania kushiriki kwenye michuano inayozingatia umri kwa kipindi cha miaka miwili kwa kosa hilo.
Timu ya vijana wa chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes haijawahi kufika mbali katika michuano yote iliyoshiriki kama ilivyokuwa kwa timu ya vijana wa chini ya miaka 23, Vijana Stars. Timu hizo zimekuwa zikitolewa hatua ya awali kila ziliposhiriki michuano ya Afrika na ile ya Olimpiki.
Timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars iliyoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 2000, imekuwa ikijitutumia katika michuano ya Afrika na kufuzu kucheza fainali mara mbili.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka juzi ilipofuzu kucheza fainali hizo nchini Afrika Kusini kabla ya kufuzu kucheza fainali za All African Games zilizofanyika mwaka huu nchini Msumbiji.
Katika fainali za mwaka juzi, Twiga Stars ilishindwa kufanya vizuri kutokana na wachezaji wake kutokuwa na uzoefu wa kutosha katika michuano ya kimataifa.
Akina dada hao walipoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi, ambapo katika mechi ya kwanza, walichapwa mabao 2-1 na wenyeji Afrika Kusini. Katika mechi yake ya pili, Twiga Stars ilichapwa mabao 3-2 na Mali kabla ya kucharazwa mabao 3-0 na Nigeria.
Twiga Stars pia ilichemsha katika fainali za mwaka huu za All Africa Games zilizofanyika mjini Maputo, Msumbiji. Katika mechi yake ya kwanza, ilitoka sare ya mabao 2-2 na Afrika Kusini, ikachapwa mabao 2-1 na Ghana kabla ya kufungwa idadi hiyo ya mabao Zimbabwe.

Simba ndiyo timu pekee iliyoweka rekodi ya juu katika michuano ya kimataifa, ambapo mwaka 1993 ilifuzu kucheza fainali ya Kombe la CAF, lakini ikafungwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Katika mechi ya awali ya fainali iliyochezwa mjini Abidjan, timu hizo mbili zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu. Simba ilicheza fainali hiyo ikiwa chini ya makocha Abdalla Kibadeni na Eshente kutoka Ethiopia.
Matokeo hayo yaliwapa imani kubwa mashabiki wa soka nchini kwamba, huenda Simba ingeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutwaa taji la Afrika.
Maandalizi kabambe ya kusherehekea ushindi yalifanyika. Kamati maalumu zikaundwa kwa ajili ya kuhakikisha ushindi unapatikana nyumbani na kanga zikachapishwa zikiwa na maandishi ‘Simba Bingwa CAF 1993’.
Hata hivyo, mambo yaligeuka katika mechi ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi hiyo, iliyoweka rekodi ya kuhudhuriwa na mashabiki lukuki, Simba ilichezea kichapo cha mabao 2-0.
Kipigo hicho kilizusha huzuni kubwa, si kwa wachezaji tu wa Simba, bali hata kwa viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo, ambao walishuhudia Rais Ali Hassan Mwinyi akikabidhi kombe la ubingwa kwa nahodha wa Stella Abidjan.
Kabla ya kufuzu kucheza fainali hiyo, Simba ilikuwa imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika mwaka 1974 huku ikitoa vichapo kwa vigogo kadhaa vya soka. Ilicheza hatua hiyo ikiwa chini ya Kocha Nabi Camara kutoka Guinea.
Katika mechi ya awali ya nusu fainali iliyochezwa mjini Dar es Salaam, Simba iliichapa Mehala El-Kubra ya Misri bao 1-0, lakini ikatolewa kwa njia ya penalti baada ya Wamisri kushinda mechi ya marudiano kwa idadi hiyo ya bao.
Simba pia iliweka rekodi ya kufuzu kucheza ligi ya mabingwa wa Afrika hatua ya makundi mwaka 2003, ikiwa chini ya Kocha James Siang'a kutoka Kenya, baada ya kuwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Zamalek ya Misri kwa njia ya penalti, kufuatia matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.
Katika hatua hiyo ya makundi, Simba ilishinda mechi mbili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, dhidi ya Enyimba na ASEC, lakini ikakubali vipigo vitatu ugenini. Ilimaliza hatua hiyo ikiwa ya pili kutoka mkiani.
Rekodi zingine za kujivunia kwa Simba ni kuweza kuziadhiri timu vigogo za Misri katika mechi tofauti za michuano ya kimataifa. Mwaka 1974 iliichapa mehara El-Kubra bao 1-0 mjini Dar es Salaam, miaka tisa baadaye iliicharaza Al-Ahly mabao 2-1 mjini Mwanza, mwaka 1995 iliinyuka Arab Contractors mabao 3-1 kabla ya kuilaza Ismailia bao 1-0 mjini Dar es Salaam.
Pengine rekodi pekee ya kujivunia kwa Simba ni kutwaa ubingwa wa michuano ya klabu za Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002. Ndio timu pekee iliyotwaa kombe hilo mara nyingi, ikilinganishwa na klabu zingine za ukanda huu.
YANGAYanga ni timu nyingine ya Tanzania iliyoweka rekodi ya kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika mara mbili mwaka 1969 na 1970, lakini mara zote ilitolewa na Asante Kotoko ya Ghana.
Katika robo fainali ya mwaka 1969, Yanga ilitolewa na Asante Kotoko kwa njia ya kura ya shilingi baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.
Katika robo fainali ya pili mwaka 1970, Yanga ilikutana tena na Asante Kotoko, ambapo katika mechi ya awali, zilitoka sare ya bao 1-1 na katika mechi ya marudiano, hazikufungana.
Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane katika muda wa nyongeza, lakini kutokana na giza kutanda uwanjani, mechi ilivunjika dakika ya 19 na hivyo kuhamishiwa kwenye uwanja huru wa mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika mechi hiyo ya tatu, Yanga ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Asante Kotoko na kutolewa kwenye hatua hiyo. Kikosi cha Yanga wakati huo kilikuwa chini ya Victor Stanculescu kutoka Romania.
Yanga pia iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kufuzu kucheza ligi ya mabingwa wa Afrika mwaka 1998, ikiwa chini ya kocha Raoul Shungu kutoka Congo, lakini ilivurunda kwenye hatua ya makundi. Ligi hiyo ilianzishwa rasmi mwaka 1997.
Timu hiyo kongwe nchini ilimaliza mechi za makundi ikiwa mkiani baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa ASEC ya Ivory Coast katika mechi yake ya mwisho iliyochezwa mjini Dar es Salaam.
Katika hatua hiyo ya makundi, Yanga pia ilipokea kipigo kizito cha mabao 6-0 kutoka kwa Raja Casablanca ya Morocco na kutoka sare ya bao 1-1 na Manning Rangers ya Afrika Kusini.
Rekodi pekee ya kujivunia kwa Yanga ni ile ya kutwaa ubingwa wa klabu za Afrika Mashariki na Kati mara nne, mwaka 1975, 1993, 1999 na 2010.
Klabu zingine za Tanzania zilizowahi kushiriki michuano ya Afrika ni Cosmopolitan (1967), Mseto (1975), Pan African (1982), Tukuyu Stars (1986), Coastal Union (1988), Mtibwa Sugar (1999 na 2000), lakini zote ziliishia hatua ya awali.

KITWANA MANARA; Tumepiga hatua kimaendeleo, si kimashindano

KITWANA Manara (kushoto) akiwa na mwanasoka mwenzake mkongwe, Peter TinoKAMA kuna mwanasoka aliyewahi kuweka rekodi ya pekee na ya aina yake hapa nchini, si mwingine zaidi ya mkongwe Kitwana Manara.Ndiye mchezaji pekee aliyeweza kucheza nafasi ya kipa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars na nafasi ya mshambuliaji kwenye klabu yake ya Yanga.
Mkongwe huyo pia ndiye mchezaji pekee aliyeweka rekodi ya kucheza soka kwa miaka mingi kuliko mchezaji mwingine yeyote Tanzania. Alianza kucheza soka mwaka 1960 na kutundika daruga zake ukutani mwaka 1980.
Manara alianza kuvaa jezi za Taifa Stars mwaka 1961 akitokea klabu ya Cosmo ya Dar es Salaam. Alistaafu kuichezea timu hiyo mwaka 1975 akiwa klabu ya Yanga.
Alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Yanga walioiwezesha timu hiyo kuwa ya kwanza nchini kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970.
Katika hatua zote hizo mbili, Yanga ilitolewa na Asante Kotoko ya Ghana, ambapo katika robo fainali ya mwaka 1969, iliondoshwa kwa njia ya kura ya shilingi baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.
Katika robo fainali ya pili mwaka 1970, Yanga ilikutana tena na Asante Kotoko, ambapo katika mechi ya awali, zilitoka sare ya bao 1-1 na katika mechi ya marudiano, hazikufungana.
Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane katika muda wa nyongeza, lakini kutokana na giza kutanda uwanjani, mechi ilivunjika dakika ya 19 na hivyo kuhamishiwa kwenye uwanja huru wa mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika mechi hiyo ya tatu, Yanga ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Asante Kotoko na kutolewa kwenye hatua hiyo. Kikosi cha Yanga wakati huo kilikuwa chini ya Victor Stanculescu kutoka Romania.
Manara pia alikuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza michezo ya All Africa Games mwaka 1973 na kutinga nusu fainali, ambapo ilitolewa na Algeria baada ya kuchapwa mabao 2-1.
“Kwa kweli kama ni rekodi ya mwanasoka aliyecheza soka kwa miaka mingi hapa nchini na kwa nafasi mbili tofauti, hakuna anayeweza kuifikia rekodi yangu,”alisema. “Mimi nilianza kuichezea timu ya taifa kuanzia kwenye michuano ya Gossage hadi ilipobadilishwa jina na kuitwa Chalenji.”
Akizungumza na Uhuru hivi karibuni kuhusu mafanikio ya soka katika miaka ya 50 ya Uhuru, Manara alisema Tanzania imepiga hatua kubwa na kupata mafanikio ya kuridhisha.
Akitoa mfano, Manara alisema japokuwa kiwango cha uchezaji soka miaka ya nyuma kilikuwa juu ikilinganishwa na hivi sasa, kuwepo kwa vifaa vingi vya michezo na viwanja vya kisasa vya kuchezea mchezo huo ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana.
Alisema miaka ya nyuma, vifaa vya michezo vilikuwa vichache na viwanja vilivyotumika kuchezea mchezo huo vilikuwa vya kawaida.
“Hivi sasa, timu yetu ya taifa imepata udhamini mkubwa, wachezaji wanalipwa vizuri, klabu zinamiliki viwanja vyao vya kuchezea soka, haya yote kwangu mimi ni mafanikio makubwa,”alisema.
Manara pia alieleza kufurahishwa kwake kuona Taifa Stars ikipata maandalizi kama ilivyo kwa baadhi ya nchi za mataifa ya Ulaya huku ikipatiwa huduma zote muhimu.
Alisema miaka ya nyuma, ilikuwa vigumu kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo kila ilipocheza ama kuhamasika na kuvaa fulana zenye rangi ya bendera ya taifa.
Manara alisema pia kuwa, soka inayochezwa hivi sasa ni ya kasi ikilinganishwa na miaka ya nyuma, lakini baadhi ya vitu vinavyofanywa na wanasoka maarufu duniani kama vile Lionel Messi wa Barcelona ya Hispania si vigeni kwa Tanzania.
Aliwataja baadhi ya wanasoka wa zamani waliokuwa na uwezo wa kucheza na mpira wanavyotaka, kupiga chenga na kupangua idadi kubwa ya mabeki kwa wakati mmoja kuwa ni pamoja na Mbwana Abushiri, Emily Kondo, Arthur Mambeta, Sunday Manara na Abdalla Kibadeni.
Alisema uwezo wa wanasoka hao haukuweza kutambulika kimataifa kutokana na kutokuwepo kwa vyombo vingi vya habari kwa ajili ya kuwatangaza. Alisema vyombo vilivyokuwepo wakati huo kama vile magazeti, vilikuwa vichache na teknolojia ya televisheni haikuwepo.
Manara alisema Tanzania ni nchi pekee kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki iliyoweza kutoa wanasoka wengi nyota, ikilinganishwa na nchi za Kenya na Uganda.
Akizungumzia uongozi wa soka nchini, Manara alisema viongozi wa zamani wa klabu hawakuwa na elimu kubwa, lakini waliweza kubuni vitu vingi na kuziletea mafanikio makubwa klabu zao.
Akitoa mfano, alisema viongozi wa Yanga waliweza kununua nyumba mtaa wa Mafia kwa sh. milioni 11 kutokana na mapato ya sh. milioni 20 katika mechi kati yao na Abaluya ya Kenya na siku hiyo wachezaji hawakulipwa hata nauli.
“Hivyo utaona kuwa, uongozi wa zamani ulikuwa wa kujitolea zaidi na viongozi walihakikisha kila mchezaji anatafutiwa kazi na walicheza kwa moyo kwa sababu walikuwa wanachama wa klabu wanazochezea hivyo ilikuwa vigumu kuzihujumu,”alisema.
Alisema viongozi wa sasa wa klabu wana elimu kubwa, lakini wanakosa ubunifu na mashabiki wa klabu kongwe za Simba na Yanga wamekosa imani kwa viongozi wao, hasa timu zao zinapofungwa katika mechi muhimu.
Mkongwe huyo alisema ubunifu wa viongozi wa zamani ulianza kutoweka miaka ya 1976, ambapo klabu za Simba na Yanga zilianza kutawaliwa na migogoro mingi, iliyosababisha zigawanyike.
Alisema migogoro hiyo ndiyo iliyosababisha klabu ya Yanga kugawanyika na kuzaliwa Pan African na ile ya Simba nayo kugawanyika na kuzaliwa Nyota Nyekundu.
Manara alisema migogoro ya mara kwa mara ndani ya klabu hizo, ilichangia kwa kiasi kikubwa kudumaza maendeleo ya soka na timu ya taifa kwa vile Simba na Yanga ndizo zinazotoa mchango mkubwa kwenye timu ya taifa.
“Asikudanganye mtu, mafanikio ya Taifa Stars yanapaswa kuanzia klabuni. Kukiwa na migogoro kwenye klabu hizo mbili, timu yetu ya taifa nayo itakuwa mbovu,”alisema.
Manara ameupongeza uongozi wa sasa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuleta mageuzi makubwa katika mchezo huo, ikiwa ni pamoja na kurejesha nidhamu kwa viongozi na kuleta utendaji mzuri.
“Kwa kweli mabadiliko katika uongozi wa chama cha soka yameonekana. Zamani pale uwanja wa Karume kulikuwa na jengo dogo tu kwa ajili ya ofisi za chama, lakini hivi sasa kuna ghorofa na uwanja wa kisasa wa mazoezi. Haya ni mafanikio makubwa,”alisema.
“Serikali nayo imejitahidi sana kutuletea makocha wa kigeni kwa ajili ya timu ya taifa na wachezaji wamekuwa wakihamasika kuichezea. Haya nayo ni mafanikio makubwa,”aliongeza.
Manara alimmwagia sifa kemkem Rais wa TFF, Leodegar Tenga kuwa ni kiongoni pekee aliyeleta mageuzi makubwa katika uongozi wa soka nchini na pia kuleta heshima kwa chama hicho.
Alisema nidhamu ndani ya shirikisho hilo imekuwa kubwa na kamati zimeachwa zifanyekazi zake kwa uhuru mkubwa bila ya kuingiliwa.
“Kwa kweli hajatokea kiongozi aliyeleta amani na utulivu katika chama cha soka kama Tenga. Waswahili wanasema, mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Tenga anastahili pongezi,”alisema.
Hata hivyo, Manara alisema wapo viongozi wengine wa chama hicho waliofanya vizuri huko nyuma, lakini hakuna anayeweza kufikia rekodi ya Tenga.
Manara amelitaka shirikisho hilo kufanya jitihada zaidi liwe na uwanja wake wa kuchezea soka kwa ajili ya kuongeza mapato yake, tofauti na ilivyo sasa, ambapo linategemea zaidi mgawo wa mechi za ligi kuu na za kimataifa.
Ameiomba serikali ifikirie kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo ili vijana wengi zaidi waweze kumudu kuvinunua na hivyo kuongeza hamasa kwao ya kushiriki katika mchezo huo.
Manara pia ametoa mwito kwa viongozi wa klabu na vyama vya soka, wawe wabunifu wa vyanzo vya mapato na uendeshaji wa mchezo huo kisasa zaidi badala ya kuweka mbele maslahi yao binafsi.
"Umefika wakati sasa, lazima kuwe na mabadiliko. Kiongozi anapochaguliwa kuongoza klabu, awe mtendaji wa kazi anayeipenda klabu yake. Asiwe mtu wa kuweka mbele mapato,"alisema.
Amewataka wanasoka wa Tanzania waone thamani ya kucheza soka kwa sababu mpira ni ajira na mchezaji anaweza kulipwa mamilioni ya shilingi kwa ajili ya usajili pekee.
“Kama mchezaji anaweza kulipwa milioni 60 kwa msimu, anapaswa kuuheshimu mpira katika maisha yake kwa sababu ndiyo ajira yake,”aliongeza.
Amewataka viongozi wa klabu kuzithamini timu za vijana kwa vile ndizo chimbuko la wanasoka. Alisema timu hizo zinapaswa kupewa huduma zote muhimu kama ilivyo kwa timu za wakubwa ikiwa ni pamoja na kuzipatia usafiri wa uhakika.
Manara alianza kucheza soka katika timu za mitaani za Sambwisi, Young Boys, Cosmo, TPC ya Arusha, Feisal na baadaye Yanga na Pan African. Alistaafu rasmi kucheza soka mwaka 1983 akiwa Yanga, ambayo katika miaka miwili ya mwisho, aliifundisha akiwa kocha mchezaji.

JELLA MTAGWA; Nahodha aliyeiongoza Stars kwa miaka 10

Jella Mtagwa

HII ni stempu ya lililokuwa shirika la posta na simu wakaati huo


HAKUNA kitu kilichowahi kumkera mwanasoka mkongwe nchini, Jella Mtagwa katika maisha yake kisoka, kama picha yake kutumika kwenye stempu ya lililokuwa Shirika la Posta, bila ridhaa yake. Tukio hilo lilitokea mwaka 1982, kipindi ambacho Jella bado alikuwa aking'ara kisoka.
Jella (58) hakuhusishwa kwa lolote kuhusu uamuzi huo na wala hakulipwa hata senti moja. Alishtukia tu picha yake ikiwa imewekwa kwenye moja ya stempu zilizokuwa zikitumiwa na Posta wakati huo.
Alipouliza kwa viongozi wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT) wakati huo, Saidi El Maamry (mwenyekiti) na marehemu Patrick Songora (katibu), jibu alilopewa ni kwamba, Posta waliomba kwa chama hicho kiwapatie jina la mchezaji wanayeona anafaa picha yake kuwekwa kwenye stempu kama kivutio na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Viongozi hao wawili walimweleza Jella kwamba, waliamua kumpendekeza yeye kwa vile alitoa mchango mkubwa katika kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kilichofuzu kucheza fainali za Afrika mwaka 1980 na pia alikuwa mchezaji bora wa ligi msimu wa 1981/1982.
Kwa sasa, Jella hajihusishi na lolote katika mchezo wa soka kama ilivyo kwa baadhi ya wanasoka wenzake wa zamani, kutokana na kupatwa na maradhi ya kupooza baadhi ya viungo vyake vya mwili. Alipatwa na maradhi hayo miaka takriban mitatu iliyopita.
Hata hivyo, hali ya Jella kwa sasa ina nafuu kwani anaweza kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kujipa mazoezi. Ameshauriwa kufanya hivyo na madaktari. Na kutokana na kuwa mdau wa soka, hupenda sana kutembelea jengo la makao makuu ya klabu ya Pan Africa, lililopo mtaa wa Swahili, Dar es Salaam. Akizungumza na Uhuru mjini Dar es Salaam hivi karibuni kuhusu mafanikio ya mchezo wa soka katika miaka 50 ya uhuru, Jella alisema Tanzania imepiga hatua kubwa hasa kutokana na uwazi uliopo katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na pia Taifa Stars kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
Hata hivyo, Jella alisema wachezaji wengi waliopo kwenye kikosi hicho hivi sasa, hawajapitia misingi mizuri ya soka tangu wakiwa wadogo, ndio sababu timu hiyo inashindwa kupata mafanikio makubwa zaidi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Jella ameishauri TFF kuwatumia wanasoka wakongwe, hasa waliocheza fainali za Afrika mwaka 1980 kwa ajili ya kutoa ushauri kwa wachezaji wa Taifa Stars ili waweze kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
"Nadhani huu unaweza kuwa msaada na mchango wetu mkubwa kwa Taifa Stars kwa sababu baadhi yetu tulicheza soka na kupata mafanikio makubwa. Tunaweza kuwaeleza mengi kuhusu mbinu za soka kuliko watu wengine,"alisema. Mkongwe huyo anayeishi maeneo ya Manzese Friends Corner, Dar es Salaam, amemtaka mshambuliaji nyota wa zamani wa Yanga na Pan African, Sunday Manara kuwa ndiye mchezaji pekee aliyekuwa akimsumbua kila alipokutana naye uwanjani.
Baadaye alikuja kuvutiwa na Zamoyoni Mogella, lakini kwa sasa haoni mchezaji yeyote mwenye mvuto licha ya kuwepo kwa wachezaji kadhaa nyota kwenye ligi kuu walionunuliwa kwa mamilioni ya pesa.
Jella alikuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Taifa Stars kucheza fainali za Afrika kwa mara ya kwanza mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria. Ndiye aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, iliyokuwa ikiundwa na nyota wengi kama vile Leodegar Tenga, Thuweni Ally, Peter Tino, Hussein Ngulungu, Juma Pondamali na wengineo.
Hata hivyo, Taifa Stars haikuweza kufanya vizuri katika fainali hizo. Katika mechi yake ya kwanza, ilichapwa mabao 3-1 na Nigeria, ilifungwa mabao 2-1 na Misri kabla ya kuilazimisha Ivory Coast kutoka nayo sare ya bao 1-1. Katika mechi zote hizo, mabao ya Taifa Stars yalifungwa na Thuweni.
Jella alianza kucheza soka tangu alipokuwa akisoma katika shule ya msingi ya Mwembesongo ya mkoani Morogoro. Kwake mpira ulikuwa ni kipaji alichojaliwa na Mungu kwani enzi zake, alikuwa beki wa aina yake na asiyetishwa ama kubabaishwa na mshambuliaji yeyote.
Alianza kucheza soka ya ushindani mwaka 1970 katika timu ya Nyota Afrika ya Morogoro. Aliteuliwa kuichezea timu ya mkoa huo katika mashindano ya Kombe la Taifa mwaka 1973, ambapo ilitwaa ubingwa baada ya kuichapa Tanga mabao 2-1 katika mechi ya fainali iliyochezwa uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Mwaka huo huo, akiwa bado anasoma shule ya sekondari ya Morogoro, uongozi wa Yanga uliokuwa chini ya mwenyekiti Tabu Mangara na meneja, Shirazi Sharrifu, ulivutiwa na kipaji chake na kuamua kumsajili. Akawa anaichezea Yanga huku akiendelea na masomo.
Alihamia rasmi katika Jiji la Dar es Salaam mwaka 1975 baada ya kumaliza masomo ya sekondari. Kikosi cha Yanga wakati huo kilikuwa kinaundwa na baadhi ya wachezaji kadhaa nyota kama vile Maulid Dilunga, Elias Michael, Abdalah Juma, Muhidin Fadhili, Athuman Kilambo, Omari Kapera, Leonard Chetete na wengineo.
Jella alikuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa klabu za Afrika Mashariki na Kati mwaka 1975 baada ya kuwabwaga watani wao wa jadi Simba mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyopigwa Zanzibar.
Aliitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa mara ya kwanza mwaka 1973 na kushiriki kwenye michuano ya Kombe la Chalenji, lakini walitolewa kwenye fainali baada ya kufungwa na Uganda mabao 2-1. Jella hakupewa nafasi ya kucheza kwenye michuano hiyo iliyofanyika mjini Kampala kutokana na umri wake kuwa mdogo.
Jella aliteuliwa kuwa nahodha wa Taifa Stars mwaka 1973 kutoka kwa Omari Zimbwe. Alishika wadhifa huo hadi mwaka 1983, ambapo nafasi hiyo ikaenda kwa kiungo Charles Boniface. Aliichezea Taifa Stars kwa miaka 10.
Mkongwe huyo aliamua kustaafu soka mwaka 1984 akiwa Pan African baada ya kuumia goti. Alilazimika kufanyiwa operesheni na daktari bingwa wa mifupa, Profesa Phillemon Sarungi.
Ameitaja sababu kubwa iliyomfanya aihame Yanga kuwa, ni mgogoro uliotokea mwaka 1976, ambao ndio uliosababisha kugawanyika kwa klabu hiyo na kuundwa kwa Pan Africa. Alikuwa mmoja wa wachezaji waanzilishi wa Pan Africa.

PETER TINO; Mwanasoka aliyeipeleka Stars fainali za Afrika 1980


Peter Tino (kulia) akiwa na mwanasoka mwenzake mkongwe, Kitwana Manara


IKUWA Agosti 26,1979 wakati timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars ilipokuwa ikirudiana na timu ya soka ya Taifa ya Zambia katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 1980 zilizofanyika nchini Nigeria.Pambano hilo lilichezwa mjini Ndola.
Mechi hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Taifa Stars kwa vile ilikuwa ikihitaji sare ya aina yeyote ili iweke historia ya kufuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza , tangu ilipoanza kushiriki michuano hiyo mwaka 1968.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa wiki mbili nyuma kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars iliishinda Zambia bao 1-0. Bao hilo lilifungwa na kiungo Mohammed Rishard Adolph.
Ushindi huo ulipatikana kwa mbinde kiasi kwamba mashabiki wengi hawakuwa na imani iwapo Taifa Stars ingeshinda ama kupata sare katika mechi ya marudiano. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani Wazambia walifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika za mapema na kudumu nalo kwa takriban dakika 86.
Zikiwa zimesalia dakika tatu pambano hilo kumalizika, mshambuliaji mrefu mwenye kasi na mashuti makali, Peter Tino alibadili sura ya mchezo na kufanya kile kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa mchezo huo nchini.
Ilipigwa kona kwenye lango la Taifa Stars, kipa Juma Pondamali akaupangua mpira kwa ngumi, ukamkuta kiungo Leodegar Tenga, aliyetoa pasi ndefu kwa kiungo mwenzake, Hussein Ngulungu, ambaye naye alitoa pasi ndefu kwa Tino.
Akiwa amezungukwa na mabeki watatu wa Zambia, Tino alilazimika kupiga hesabu za haraka haraka. Aliwachomoka mbio mabeki nao na kukimbia na mpira kwa kasi. Alipofika nje kidogo ya eneo la hatari la Zambia, alifumua shuti kali la mguu wa kulia, lililompita kipa Shileshi wa Zambia na mpira kutinga wavuni.Bao hilo lilipatikana baada ya pasi tatu.
Katika mechi hiyo, Taifa Stars iliwakilishwa na kipa Juma Pondamali,mabeki ni Leopard Tasso, Mohammed Kajole/ Ahmed Amasha, Salim Amir, Jella Mtagwa, viungo ni Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu na washambulaji ni Omari Hussein, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni Ally.
Kikosi hicho kilichokuwa chini ya Kocha Slowmir Work kutoka Poland, akisaidiwa na Joel Bendera na Ray Gama, ndicho kilichoiwakilisha Tanzania katika fainali za kombe hilo zilizofanyika nchini Nigeria.
Katika fainali hizo, Taifa Stars ilichapwa mabao 3-1 na wenyeji Nigeria katika mechi ya ufunguzi, ilitoka sare ya mabao 2-2 na Ivory Coast kabla ya kuchapwa mabao 2-1 na Misri na kutolewa hatua ya makundi.
Hivi sasa Tino hajihusishi kabisa na masuala ya soka, si kwa kazi ya ukocha wala uongozi. Aliamua kutundika daruga zake ukutani mwishoni mwa miaka ya 1980 akiwa klabu ya Yanga. Alistaafu soka kwa kile alichodai kuwa, mwili wake umechoka na pia alitaka kutoa nafasi kwa wanasoka chipukizi kuonyesha vipaji vyao.
Akizungumzia maendeleo ya soka hivi sasa hapa nchini, Tino alisema ni mazuri hasa ikizingatiwa kuwa, serikali ipo mstari wa mbele kuihudumia timu ya taifa na pia wamejitokeza wafadhili wengi, lakini tatizo lipo kwa wachezaji.
Alisema wanasoka wa Tanzania kwa sasa, kuanzia ngazi ya klabu hadi taifa, hawana upendo miongoni mwao, hawajitunzi, wanabweteka na sifa na wameweka mbele zaidi anasa, tofauti na wachezaji wa zamani.
"Enzi zetu hatukuwa tukibweteka na sifa za wapenzi. Binafsi nimechezea timu ya taifa kwa miaka minane mfululizo kwa sababu nilijitunza na sikuwa nikiendekeza anasa,"alisema.
"Lakini sasa hivi, mchezaji msimu wa kwanza anachezea Yanga, wa pili Simba, mara msimu huu anacheza vizuri, msimu unaofuata anavurunda," aliongeza.
Tino alisema enzi zao, kila walipokuwa wakisifiwa na mashabiki, walijiona kama vile wanadanganywa na bado hawajafika kiwango cha juu, tofauti na hivi sasa, ambapo alidai kuwa, wachezaji huanza kujiona nyota baada ya kucheza soka kwa kipindi kifupi.
Mshambuliaji huyo nyota wa zamani wa klabu za Pan African, African Sports na Yanga alisema, hata mazoezi waliyokuwa wakiyafanya wachezaji wa zamani, ni tofauti na sasa na kwamba, walikuwa na nidhamu ya hali ya juu na waliheshimu makocha na viongozi wao.
"Hivi sasa wapo baadhi ya wachezaji wanawazidi nguvu viongozi na makocha na kuamua wanavyotaka, ndio sababu hata viwango vyao vinashuka haraka. Mchezaji mechi mbili anacheza vizuri, ya tatu kiwango kinashuka," alisema.
Tino alisema maslahi ya wachezaji wa zamani yalikuwa madogo, lakini kwa vile soka ilikuwa kwenye damu yao, walicheza kwa nguvu na kujituma.
Alisema iwapo maslahi wanayopata sasa wachezaji wa Taifa Stars, yangekuwepo enzi zao, Tanzania ingeweza kufuzu kucheza fainali za kombe la Dunia miaka ya 1980.
Akitoa mfano, Tino alisema katika mechi ya mwisho ya michuano ya kucheza fainali za kombe hilo mwaka 1982, Taifa Stars iliilazimisha Nigeria kutoka nayo sare ya bao 1-1 katika mechi ya awali iliyochezwa mjini Lagos. lakini ziliporudiana mjini Dar es Salaam, Taifa Stars ulifungwa mabao 2-0.
"Tulikuwa tukihitaji sare ya bila kufungana ili tufuzu kucheza fainali. Tungekuwa tunapata maslahi mazuri na motisha kama ilivyo sasa, nina hakika tungefuzu kucheza fainali kwani Nigeria wasingetufunga nyumbani,"alisema.
"Hivi sasa Rais Jakaya Kikwete ni mhamasishaji mkuu wa maendeleo ya soka, kampuni nyingi zimejitokeza kuidhamini Taifa Stars na wachezaji wamekuwa wakilipwa mamilioni ya pesa. Enzi zetu ukizungumzia soka, ni wachezaji, chama cha soka na labda waziri mwenye dhamana ya michezo,"aliongeza.
Akizungumzia sababu za kufungwa mara kwa mara kwa Taifa Stars katika mechi za kimataifa zinazochezwa hapa nchini, Tino alisema ni kutokana na matatizo binafsi ya wachezaji.
Tino alisema wanasoka wanaoteuliwa kuichezea Taifa Stars wanashindwa kwenda na kasi ya mchezo, kubadilika kulingana na mchezo unavyoendelea na pia kuondokana na dhana kwamba, kumiliki mpira ndio ushindi.
Mwanasoka huyo mkongwe alisema, kama wachezaji wa Taifa Stars wangekuwa na kawaida ya kuonyesha uwezo wao binafsi, wangeweza kushinda mechi nyingi za kimataifa zinazochezwa hapa nchini.
"Mimi huwa nasikitika sana ninapoona wachezaji wa hapa nchini wanapata huduma nzuri, wanalipwa vizuri, wanaye kocha mzuri, lakini wanakosa juhudi binafsi. Ukibebwa unatakiwa ung'ang'anie," alisisitiza.
Alizitaja kasoro zingine alizozigundua kwa wanasoka wengi wa Tanzania kuwa ni pamoja na kukosa ujanja na mbinu za kimchezo, kutojiamini na kutohamasishana wanapokuwa uwanjani.
Akitoa mfano, Tino alisema mchezaji anaweza kuwa peke yake na mpira, lakini badala ya kuuvuta na kwenda nao mbele, anatoa pasi hovyo kwa kuogopa lawama. Alisema mchezo wa soka ni wa lawama, hivyo wachezaji hawapaswi kuziogopa.
"Ni nadra hivi sasa kuwapata washambuliaji wajanja wajanja kama ilivyokuwa kwa Zamoyoni Mogella, Issa Athumani, Saidi Suedi na wengineo. Vilevile ni nadra kuwakuta wachezaji wakihamasishana uwanjani. Enzi zetu tulikuwa tunaongea kwa kustuana. Hivi sasa, vijana wetu wanacheza kama mabubu," alisema.
Tino alisema kama enzi zao kungekuwepo na televisheni, wachezaji wa sasa wangeweza kujifunza mengi kutoka kwao na kupata akili kuhusu soka.
Mshambuliaji huyo mkongwe pia alieleza kushangazwa kwake na maumbile ya wachezaji wa sasa, ambayo alisema ni tofauti na yale waliyokuwa nayo wachezaji wa zamani. Alisema enzi zao walikuwepo wachezaji wafupi kama vile Omari Hussein na Shaaban Katwila, lakini walikuwa na nguvu na kasi.
Ametoa mwito kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuteua wasaidizi wa makocha wa kigeni wenye upeo wa mchezo huo. Alisema wasaidizi wanaoteuliwa sasa, wanashindwa kugundua makosa ya wachezaji na kutoa ushauri wa maana kwa makocha wa kigeni.
Tino alizaliwa mwaka 1956 katika hospitali ya Ocean Road mjini Dar es Salaam, akiwa mtoto wa tano katika familia ya watoto tisa wa mzee Peter Agustino. Familia hiyo ilikuwa ikiishi maeneo ya Msimbazi, Dar es Salaam.
Alianza kucheza soka mwaka 1967 katika timu ya mtaani ya Bonde Sports kabla ya kuhamia Young Kinya ya Kariakoo na baadaye Englebeth ya Manzese. Kutokana na kipaji alichokuwa nacho katika soka, aliajiriwa na kiwanda cha nguo cha urafiki na kuichezea kuanzia mwaka 1974 akiwa na marehemu Gibson Sembuli, Adam Juma, Awadh Gesani, Abdulrahman Juma na Wengineo.
Mwaka 1975 alihamia Mwanza na kujiunga na Mwatex, aliyoichezea kwa miezi mitatu. Mwaka huo huo, alikwenda Arusha na kujiunga na klabu ya Kurugenzi kabla ya kuhamia Tanga na kujiunga na African Sports.
Aliichezea African Sports hadi mwaka 1979 akiwa na baadhi ya wachezaji waliong'ara nchini enzi hizo kama vile Abdalla Luo, Kassim Mwabuda, Omar Bawazir, Peter Mhina, Francis Chausa na Mhando Mdeve.
Aliitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa mara ya kwanza mwaka 1977 na kuichezea hadi mwaka 1985. Aliichezea timu hiyo kwenye michuano mbalimbali ya awali ya kombe la Chalenji, Kombe la Afrika na Kombe la Dunia.
Mwaka 1980, aliihama African Sports na kujiunga na Pan African ya Dar es Salaam. Aliichezea klabu hiyo kwa miaka minne katika ligi ya Tanzania Bara na michuano ya Kombe la Washindi la Afrika kabla ya kuhamia Yanga hadi alipostaafu soka mwaka 1989.

Tuesday, December 6, 2011

VENGU APATA AHUENI


HALI ya msanii Joseph Shamba 'Vengu' wa kundi la Orijino Komedi inaendelea vizuri na amehamishwa kutoka kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na kulazwa kwenye wodi ya Mwaisela katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Vengu, ambaye aliwekwa kwenye chumba hicho kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa, ambao bado haujawekwa wazi, alihamishiwa kwenye wodi ya Mwaisela juzi.
Akizungumza baada ya kumtembelea msanii huyo kwenye wodi hiyo juzi ili kujua maendeleo ya afya yake, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alisema hali ya Vengu inaendelea vizuri.
Dk. Fenella alikanusha taarifa zilizosambazwa kwenye baadhi ya mitandao ya habari mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba Vengu amefariki dunia.
"Binafsi nimemtembelea wodini leo hii (juzi) na kusema kweli hali yake inaendelea vizuri kwa sababu unapotolewa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na kuhamishiwa wodini, maana yake ni kwamba madaktari wameridhishwa na maendeleo yako,"alisema.
Dk. Fenella alisema kinachofanyika kwa sasa ni msanii huyo kuendelea kutumia dawa alizoandikiwa na madaktari huku akiendelea kufanyiwa uchunguzi zaidi wa afya yake.
Kaka wa msanii huyo,Steven Shamba alisema wanamshukuru Mungu kuona hali ya msanii huyo inaendelea vizuri baada ya kutolewa ICU.
"Tunachoshukuru ni kwamba matibabu yake yanasimamiwa na profesa na kitendo cha kutolewa chumba cha wagonjwa mahututi na kulazwa wodini kinaashiria kwamba maendeleo yake ni mazuri,"alisema.
Kiongozi wa kundi la Orijino Komedi, Sekione David, maarufu kwa jina la Seki alisema, matibabu ya Vengu kwa sasa yanagharamiwa na Rais Jakaya Kikwete hivyo kama kuna umuhimu kwa msanii huyo kupelekwa nje kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi, ndiye pekee mwenye uamuzi huo.
"Watu wengi wamekuwa wakitulalamikia kwamba kwa nini asipelekwe India kupatiwa matibabu. Tunachoweza kusema ni kwamba yanaweza kupatikana hapa hapa, kwa nini apelekwe India? Tunachoshukuru Mungu ni kwamba, matibabu yake yanagharamiwa na Rais Jakaya Kikwete,"alisema.
Seki alieleza kusikitishwa kwake na taarifa potofu zilizosambazwe kwenye mitandao wiki iliyopita, zikidai kwamba msanii huyo amefariki dunia. Alisema taarifa za aina hiyo si nzuri kwa jamii na ni vyema wahusika wapate taarifa sahihi kutoka kwa vyanzo husika vya habari kuliko kukurupuka na kueneza uvumi wa uongo.
Vengu hajaonekana kwenye vipindi vya Orijino Komedi vinavyoonyeshwa na kituo cha televisheni cha TBC 1 kwa takriban miezi miwili sasa kufuatia kulazwa Muhimbili.
Hata hivyo, bado haijawekwa wazi kuhusu ugonjwa unaomsumbua, lakini kuna habari kuwa, anasumbuliwa na maumivu ya kichwa.
Msanii huyo alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kuweza kumwigiza Mwenyekiti wa chama cha TLP, Augustine Mrema kwa mavazi na sauti yake wakati wa maonyesho ya Orijino Komedi.

KOCHA MPYA WA SIMBA ATOA YA MOYONINa Ezekiel Kamwaga

KLABU ya soka ya Simba hivi karibuni ilimtangaza Profesa Milovan Cirkovic kuwa kocha wake mkuu akichukua nafasi ya Moses Basena.Cirkovic (inatamkwa Chirkovich) ameingia mkataba wa miezi sita kuifundisha Simba na mkataba huo umeanza rasmi Desemba Mosi mwaka huu.Tovuti ya Simba, www.simba.co.tz ilifanya naye mahojiano hivi karibuni ambapo alieleza kwa kirefu mambo ambayo wapenzi wa Simba na mchezo wa soka nchini kwa ujumla wangependa kuyafahamu.Pata uhondo.

Simba: Karibu tena Simba Sports Club.

Milovan: Ahsante sana. Naipenda Simba. Naipenda Tanzania na kwa kweli nimefurahi kurejea hapa.

Simba: Tanzania na Serbia ni mbali kwelikweli. Kabla hujaja Tanzania kuifundisha Simba kwa mara ya kwanza miaka ya nyuma, je ulikuwa umewahi kusikia chochote kuhusu Simba au Tanzania?

Milovan: Kusema ukweli, sikuwa nimewahi kusikia chochote kuhusu Simba hadi nilipokuja kufundisha. Kila kitu nilikipata hapa kuhusu Simba.Hata hivyo, nilikuwa nafahamu kuhusu nchi ya Tanzania. Nilisoma shuleni na sisi tunafundishwa mengi sana katika jiografia. Na usisahau kuwa mimi nimewahi kuwa mwalimu wa Chuo Kikuu na hivyo kwa wasomi ni rahisi kufahamu mambo ya nchi za mbali.

Simba: Jambo gani ambalo bado unalikumbuka kuhusu Tanzania ulipokuja mara ya kwanza.

Milovan: (Anacheka). Siku moja nilikuwa matembezini na Hagila (Evarist, miongoni mwa waliokuwa viongozi wa Simba wakati Milovan alipokuja mwaka 2007) na ghafla nyani akatokea mbele yetu.Sitaisahau siku hiyo kwa sababu hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwangu kumwona nyani uso kwa uso. Mara zote nimekuwa nikiwaona kupitia luninga.Hilo nalikumbuka sana.

Simba: Turudi kwenye soka sasa. Hebu kwanza tueleze kwa kifupi historia yako kisoka

Milovan: Ok. Nilizaliwa katika iliyokuwa Yugoslavia ya zamani katika mji wa Cacak (inatamkwa tatak) mwaka 1955.Nilicheza soka hadi kiwango cha daraja la kwanza na niliachana na soka wakati nilipovunjika mguu mpirani wakati nilipokuwa na miaka 31. (Anaonyesha kovu la jeraha lake mguuni).Niliwahi kuchezea klabu maarufu ya Partizan Belgrade na mara baada ya kuumia nikaingia katika masuala ya taaluma kiasi cha kuwa mwalimu katika Chuo Kikuu cha Belgrade.Nina vyeti mbalimbali vya ukocha kuanzia Shahada ya Chuo Kikuu katika Elimu ya Viungo (Physical Education) na nimefundisha pia somo hilo vyuo vikuu na ndiyo maana naitwa Profesa.Nina leseni ya ukocha inayotambuliwa na UEFA, pamoja na vyeti vingine vinavyotambuliwa.

Simba: Kwanini uliamua kuwa kocha wa soka?

Milovan: Mara baada ya kuachana na kucheza soka mapema, niliona njia pekee ya kuendelea kubaki katika mchezo huu ni kuwa kocha.Napenda sana mpira wa miguu na sidhani kama ningeweza kufanya kingine chochote kwenye maisha yangu zaidi ya kucheza au kujihusisha kwa namna yoyote ile na mchezo huu.

Simba: Serbia si miongoni mwa nchi kubwa za Ulaya lakini imekuwa na sifa kubwa ya kutoa makocha wazuri duniani hususani katika nchi za Afrika na Asia. Nini unafikiri ni siri ya mafanikio haya?

Milovan: Kwanza tunapenda sana mpira –sisi raia wa Serbia. Kwa hiyo kuwa kocha au mchezaji mzuri kunakuja tu kwenye damu.Lakini la pili ni kuwa kuna vyuo vingi sana vya ukocha kule kwetu na pia tuna uwezo wa kuishi katika mazingira magumu.Mimi nimekuja Tanzania na sina ndugu, jamaa wala rafiki yeyote. Kila kitu nawaamini ninyi. Inahitaji roho ngumu kidogo kuchukua maamuzi magumu kama haya.Hizo zinaweza kuwa sababu za msingi zaidi.

Simba: Nimesikia kuwa mmoja wa marafiki zako wa karibu zaidi ni Milovan Rajevac, Kocha aliyeipeleka Ghana katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika. Je taarifa hizi zina ukweli wowote?

Milovan: Milovan ni rafiki yangu. Nilipokuwa kocha wa FC Borak Cacak mwaka 2008, yeye alikuwa msaidizi wangu kwa maana ya kocha msaidizi.Ni rafiki yangu wa karibu sana.

Simba: Nini falsafa yako ya soka? Unataka soka ichezweje na wachezaji wako?

Milovan: Rahisi. Timu zote zinazofundishwa na mimi zinakuwa na sifa ya kucheza soka la pasi nyingi na zinazomiliki mpira.Nataka timu ianze kucheza kuanzia nyuma. Nafahamu kuwa kuna wakati timu inaweza kutengeneza nafasi na kufunga kwa pasi chache lakini si kitu cha kutokea mara kwa mara.Nataka timu icheze kama Barcelona ya Hispania. Mimi nimeanza kuipenda Barcelona zamani kabla hata Josep Guardiola hajawa kocha wa timu hiyo.Siku zote Barcelona imekuwa ikicheza vizuri. Real Madrid inatwaa makombe lakini Barca inacheza soka la kuvutia zaidi. Soka ni burudani na inanoga zaidi kama inaendana na ushindi. Hata Arsenal ya miaka mitano iliyopita ilikuwa inacheza soka ninayoipenda.Ninachokisema ni hivi, Simba si Barcelona. Lakini inaweza kucheza kama Barca kwa kiwango chake. Huo ndiyo mtazamo wangu.

Simba: Kuna wachezaji wowote wa Simba uliowafundisha miaka minne iliyopita na bado unawakumbuka?

Milovan: Namkumbuka Chollo (Nassor Said Masoud), mimi ndiye niliyembadilisha kucheza kutoka kiungo na kuwa mlinzi wa pembeni.Nilimuona tu namna ya uchezaji wake na nikashauriana na wenzangu katika benchi la ufundi kuwa anafaa kuwa mlinzi wa pembeni.Nimefurahi kuwa sasa ni mlinzi wa kulia tegemeo kwa taifa. Namkumbuka pia Juma Nyoso, Victor Costa, ingawa alikuwa anaumwa goti wakati nilipokuja na Emmanuel Gabriel ambaye alikuwa anajua sana kufunga.
Nimeangalia michuano ya Chalenji na tayari nimewaona Jabu, Kapombe, Kaseja, Kazimoto na Okwi. Wote ni wachezaji wazuri na nasubiri kwa hamu kufanya nao kazi.

Simba: Kikosi cha pili cha Simba maarufu kwa jina la U20, hivi karibuni kimetwaa Kombe la Uhai na wengi wanakizatama kama sehemu muhimu ya mafanikio ya Simba katika miaka ijayo. Una mpango gani na kikosi hiki.

Milovan: Kwanza nimefurahi sana kwa Simba kuwa na kikosi hiki cha vijana. Huu ndiyo utaratibu duniani kote, huwezi kuwa na timu nzuri ya wakubwa kama huna timu nzuri ya vijana.Kwa bahati nzuri, mimi nina historia ya kufundisha timu za wakubwa na watoto ndani na nje ya Serbia. Nina uzoefu na najua nini wanahitaji.Sifa yangu moja kubwa ni kuwa, kama kijana akiwa na uwezo, hata kama ni mdogo, mimi ninampa nafasi. Lakini ni lazima nihakikishe yuko tayari kiakili kukabiliana na changamoto alizonazo.Kama mchezaji ni mzuri, atapata nafasi.

Simba: Hebu tueleze kuhusu familia yako kwa ufupi.

Milovan: Nina mke, Dionezia na watoto watatu wa kike – Anna, Sara na Marta.S: Unavuta sigara gani? Ngapi kwa siku.M: Navuta Malboro. Kwa kawaida huwa navuta pakiti moja na nusu kwa siku.

Simba: Una jina lolote la utani?

Milovan: Ukienda Serbia na ukaniulizia kwa jina la Milovan hutonipata. Uliza Profesa Cirko (Profesa Chirco). Kwa hiyo, sina tatizo kama Watanzania watakuwa wakiita kwa ufupi Chirco.

Simba: Miongoni mwa wanasoka maarufu zaidi kutoka Serbia kwa sasa ni Nemanja Vidic. Je, unamfahamu kivipi?

Milovan: Sifahamiani naye kibinafsi. Isipokuwa anatoka katika eneo la Uzice (tamka Ujitse), kijiji kinachofuata kutoka cha kwangu cha Cacak.

Simba: Unawaahidi nini wapenzi na wanachama wa Simba watakaosoma mahojiano haya.

Milovan: Nawaomba waipe timu muda wa kunielewa na mimi kuwaelewa wachezaji wangu. Soka si sawa na spea ya gari ambayo ukiiweka gari inawaka hapohapo.Itachukua muda kidogo kuelewana na hivyo naomba uvumilivu kutoka kwa washabiki. Kwa bahati nzuri washabiki wa Simba ni watu waelewa sana na nadhani watavuta subira kidogo.
Simba: Kila la kheri kocha.

Milovan: Ahsante sana.

BAYI ASHINDA TUZO YA MIAKA 50 YA UHURU

Filbert Bayi alivyo sasa

Filbert Bayi akiwa ameshikilia tuzo aliyoshinda enzi zakeBINGWA wa zamani wa dunia wa mbio za mita 1500, Filbert Bayi ameibuka mshindi wa tuzo ya mwanamichezo bora wa miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika baada ya kuzoa kura 13.
Upigaji kura kwa ajili ya kuwania tuzo hiyo umefanyika kupitia blogu hii ya liwazozito. Kura alizopata Bayi ni sawa na asilimia 72 ya kura zilizopigwa na wasomaji wa blogu hii.
Bayi alikuwa mwanariadha wa kwanza wa Tanzania kushinda medali ya dhahabu baada ya kushinda mbio za mita 1500 katika michezo ya Jumuia ya Madola iliyofanyika mwaka 1974 mjini Christchurch, New Zealand.
Mshindi wa pili wa mbio hizo alikuwa John Walker wa New Zealand wakati nafasi ya tatu ilinyakuliwa na Ben Jipcho wa Kenya.Bayi pia aliweka rekodi ya dunia ya mbio hizo kwa kutumia dakika 3:32:16
Mwaka 1975 Bayi alivunja rekodi ya mbio hizo iliyodumu kwa miaka minane iliyokuwa ikishikiliwa na Ryun baada ya kukimbia kwa dakika 3:51:0 mjini Kingston, Jamaica. Hata hivyo rekodi hiyo ilidumu kwa miezi michache baada ya kuvunjwa na Walker, aliyekimbia kwa dakika 3:49.4.
Bayi pia alishinda medali ya fedha katika mbio za mita 3000 kuruka vikwazo katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 1980 iliyofanyika Moscow, Russia. Alishinda mbio hizo kwa kutumia dakika 8:12:5.
Mwanariadha huyo mkongwe pia alishinda mbio za mita 1500 katika michezo ya All Africa-Games iliyofanyika mwaka 1973 mwaka 1978 na kumbwaga Kipchoge Keino, aliyeambulia medali ya fedha.
Bayi won a silver medal in the 3000 m steeplechase at the 1980 Summer Olympics in
Moscow. He ran 8:12.5 behind Bronisław Malinowski.
Kwa sasa, Bayi ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na anamiliki Taasisi ya Bayi, ambayo lengo lake kubwa ni kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana katika michezo.
Bayi pia anamiliki shule ya awali na msingi za Filbert Bayi zilizopo Kimara pamoja na shule ya sekondari iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

Mshindi wa pili wa tuzo hiyo ni bondia Habibu Kinyogoli, ambaye alishinda medali ya fedha katika michezo ya All Africa-Games iliyofanyika mwaka 1978 nchini Nigeria.

Kinyogoli ni mmoja wa mabondia wanaoheshimika nchini kutokana na mchango mkubwa aliotoa katika ndondi za ridhaa na zile za kulipwa. Ni kocha aliyewafundisha mabondia wengi wa ndondi hizo nchini.

Kinyogoli amepata kura nne, ambazo ni sawa na asilimia 22 ya kura zilizopigwa na wasomaji wa blogu hii.

Nafasi ya tatu imechukuliwa na mwanasoka mkongwe Jella Mtagwa, aliyepata kura mbili ambazo ni sawa na asilimia 11 wakati Peter Tino ameshika mkia kwa kutoambulia kura.

Jela ni nahodha aliyeiongoza Taifa Stars kwa miaka 10 na picha yake ilikuwa kutumika katika moja ya stempu zilizotengenezwa na lililokuwa shirika la posta na simu Tanzania miaka ya 1980, lakini hakulipwa chochote. Tino ndiye mchezaji aliyeiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Afrika kwa mara ya kwanza mwaka 1980 baada ya kuifungia bao la kusawazisha katika mchezo kati yake na Zambia uliofanyika mjini Ndola mwaka 1979.

Hongera sana Bayi kwa kuibuka mshindi wa tuzo hii. Blogu ya liwazozito inakutakia kila la heri katika maisha yako. Pia tunawapongeza Kinyogoli, Jella na Tino, ambao tuliwashirikisha bila ridhaa yenu, lakini kwa kutambua mchango mkubwa mlioutoa katika maendeleo ya michezo hapa nchini.

Pia tunawashukuru wale wote walioshiriki kuwapikia kura wanamichezo hawa. Mungu awabariki.

Friday, December 2, 2011

HISTORIA FUPI YA MR. EBBOJina kamili ni Abel Loshilaa Motika a.k.a Mr Ebbo, azaliwa tarehe 26 may 1974 jijini Arusha. Elimu ya msingi aliianza mwaka 1982 katika shule ya msingi kijenge baadae mwaka 1984 aliamia tanga na kuendelea na masomo katika shule ya msingi nguvumali na kumaliza elimu ya msingi mwaka 1988.

Alijiunga na elimu ya sekondari katika shule iitwayo jumuiya sec school. iliyopo jijini Tanga. Alimaliza elimu ya sekondari mwaka 1992. Na kwa kipindi hicho chote wakati yuko shuleni alikuwa akiimba kwaya kanisani kwenye kanisa la kisosora (lutheran church) ambapo ilimsaidia sana kujifunza muziki.

Alirudi Arusha mwaka 1993 na kubahatika kupata kazi kwenye night club ambapo alitumia mishahara yake kurekodi nyimbo ambazo hazikumpa mafanikio yeyote isipokuwa zilimuweka katika ramani ya muziki.

Baada ya hapo alifanya kazi ya kuandaa matangazo ya biashara na vipindi vya redio kwenye studio iliyojulikana kama Supreme recording studios iliyopo mjini Arusha. kipindi hicho kilijulikana kama “Mambo gani haya”

Alirekodi nyimbo kadhaa ambazo hazikumpa mafanikio yoyote kwa mara nyingine na hali hiyo ikamkatisha tamaa kabisa.

Baadae mwaka 1995 alipata kazi ya kuuza nguo kwenye duka la JJ BLACK lililopo jijini Arusha. Mwaka 1999 aliamua kurudi jijini Tanga na akafanikiwa kufunga ndoa na kubahatika kupata watoto wawili Ashley na baadaye Alicia.

Alianza kazi ya uwakala wa kuuza magazeti mwaka 2000, kazi ambayo pia haikumletea mafanikio yeyote makubwa kama alivyokuwa anatarajia. Baadaye mwaka 2001 akaanzisha biashara ya kuuza mchele kwa jumla ambayo pia haikuwa na mafanikio aliyoyatarajia.

Kipindi hicho chote alipokuwa Tanga, alifahamiana na wasanii wa muziki wa Bongo Fleva,Professor J na Wagosi wa kaya, na wao pia walijua kuwa Mr. Ebbo ni msanii asilia.

Baadae alijiunga na chuo cha kozi za computer jijini tanga.Wagosi waliporekodi wimbo wao wa Tanga kunani ,Mr Ebbo alihamasika kurudi tena kwenye Muziki na ndipo alipoandika wimbo wa kwanza wa "Mimi Mmasai mwaka 2002". Wimbo huo ukatambulisha album yake ya kwanza kisha wimbo wa 'Fahari yako'. Baadaye mwaka 2003 akafungua studio ( MOTIKA RECORDS) ambayo ilifanikiwa kuwatambulisha wasanii kama Danny Msimamo, Dr Leader, Mo-Kweli, na wengineo wengi , wote hawa aliwaproduce yeye mwenyewe kama producer wa MOTIKA RECORDS.

Mwaka 2003 akarekodi Album yake ya pili iliyojulikana kwa jina la Bado Ijasungumiswa. Mwaka 2004 akarekodi Album yake ya tatu iliyoitwa Kazi gani. Mwaka 2005 akarekodi Album ya nne iliyoitwa Alibamu. Mwaka 2006 akarekodi Album ya tano inayoitwa Kamongo.ambayo ndio albamu ya mwisho kwa uhai wake.

Mr. Ebbo kuzikwa J'tatu, sababu za kifo chake zaelezwa


Na Shabani Mdoe, Arusha
MSANII maarufu wa muziki wa kizazi kipya Abel Motika maarufu kama Mr.Ebbo amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Mission Usa River wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Akizungumza na Uhuru kwa nja ya simu, msemaji wa familia hiyo ambae pia ni msanii mwenzake wa muziki huo, Fred Maliki (Mkoloni) alisema, Ebbo alifariki majira ya saa 5 usiku katika hospitali hiyo alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Mkoloni alisema Ebbo alifariki kutokana na ugonjwa uliokua ukimsumbua wa kukaukwa na damu mwilini hali iliyosababisha kupatiwa matibabu pamoja na kuongezewa damu kila mara katika hospitali mbalimbali.
Alisema Ebbo mara ya mwisho alikwenda katika hospitali ya rufaa ya KCMC mjini Moshi,ambapo alifanyiwa uchunguzi mbalimbali pasipo kuonekana sababu ya kukaukwa na damu,hali iliyolazimu kuongezewa damu.
Alisema kutokana na tatizo hilo kuonekana kuwa kubwa na la kila mara, alilazimika kuhamisha makazi yake kwa muda toka mkoani Tanga alikokuwa anafanya kazi yake ya sanaa na kuhamia eneo la Sekei jijini Arusha, ambako ndiko nyumbani kwao kwa ajili ya kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo ya Mission.
Aidha alisema katika siku za hivi karibuni, Ebbo alikuwa amepumzika nyumbani akisubiri majibu ya vipimo vyake vilivyofanyika ili kubaini tatizo lililokuwa likisababisha kukaukwa na damu kila mara.
Mkoloni alisema msanii huyo anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwao Sekei jijini Arusha siku ya jumatatu na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru ukisubiri taratibu za maziko.
Alisema Ebbo ameacha mke na watoto wawili wote wa kike wenye umri katika ya miaka 5 hadi 9 ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi.


Hadi marehemu Ebbo anafariki, alikuwa akiendelea na shughuli zake na muziki katika studio yake iliyoko mkoani Tanga ya Motika Recods na haijafahamika kama ameacha albamu au wimbo wowote mpya aliokuwa ameandaa siku za hivi karibuni.
Mara ya mwisho, msanii huyo alionekana mkoani hapa akitumbuiza katika mikutano ya kampeni za ubunge na urais za mgombea ubunge wa jimbo la Arusha kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk.Batilda Buriani.
Akizungumzia kifo hicho, Dk. Batilda alisema kimemsikitisha sana na kwamba yupo bega kwa bega na familia ya msanii huyo na wengine pamoja na watanzania wote katika kipindi hiki kigumu kwa kumuombea dua njema marehemu huyo pamoja na ndugu na watoto ili wapewe wepesi na pepo njema.
Dk.Batilda, ambaye katika baraza lililopita la mawaziri alikuwa waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais mazingira alisema, Mr. Ebbo atakumbukwa kwa mengi ikiwa ni pamoja na kuenzi mila za kabila la kimasai kwa nyimbo alizokuwa akiimba pamoja na kuhamasisha amani ya taifa.

Mr Ebbo afariki dunia


MWIMBAJI nguli Tanzania aliyeibuka na staili ya bongofleva kwa ‘tune’ na staili ya Kimasai, Abel Rusheraa Motika, almaarufu – Mr Ebbo amefariki dunia.
Habari za uhakika zilizoifikia blogu hii leo zinaeleza kwa, Mr. Ebbo alifariki kufuatia kusumbuliwa na ugonjwa wa kichomi kwa muda mrefu.
Amefariki akiwa nyumbani kwa familia yake, maeneo ya Usa River, Arusha.Mwanamuziki huyo alifahamika zaidi kwa nyimbo zake zenye lafudhi ya Kimasai, ikiwamo – Mi Mmasai Bwana, Kamongo na nyingine nyingi zilizoteka uwanja wa muziki.
Pia alikuwa miongoni mwa wanamuziki walioinukia kwa kufanya ‘kolabo’ na wanamuziki wengine, hasa wanaotoka Mkoa wa Tanga wakiwamo; Wagozi wa Kaya.
Mipango ya mazishi inafanywa na familia yake na huenda akapumzishwa katika mashamba ya familia yake yaliyoko Usa River.
Blogu hii inatoa pole kwa mashabiki wa muziki, marafiki, watoto, ndugu jamaa na marafiki wote wa marehemu Mr. Ebbo.

Innalilah Wainailaihi rajiuun
Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake litukuzwe.