KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, December 9, 2011

JELLA MTAGWA; Nahodha aliyeiongoza Stars kwa miaka 10

Jella Mtagwa

HII ni stempu ya lililokuwa shirika la posta na simu wakaati huo


HAKUNA kitu kilichowahi kumkera mwanasoka mkongwe nchini, Jella Mtagwa katika maisha yake kisoka, kama picha yake kutumika kwenye stempu ya lililokuwa Shirika la Posta, bila ridhaa yake. Tukio hilo lilitokea mwaka 1982, kipindi ambacho Jella bado alikuwa aking'ara kisoka.
Jella (58) hakuhusishwa kwa lolote kuhusu uamuzi huo na wala hakulipwa hata senti moja. Alishtukia tu picha yake ikiwa imewekwa kwenye moja ya stempu zilizokuwa zikitumiwa na Posta wakati huo.
Alipouliza kwa viongozi wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT) wakati huo, Saidi El Maamry (mwenyekiti) na marehemu Patrick Songora (katibu), jibu alilopewa ni kwamba, Posta waliomba kwa chama hicho kiwapatie jina la mchezaji wanayeona anafaa picha yake kuwekwa kwenye stempu kama kivutio na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Viongozi hao wawili walimweleza Jella kwamba, waliamua kumpendekeza yeye kwa vile alitoa mchango mkubwa katika kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kilichofuzu kucheza fainali za Afrika mwaka 1980 na pia alikuwa mchezaji bora wa ligi msimu wa 1981/1982.
Kwa sasa, Jella hajihusishi na lolote katika mchezo wa soka kama ilivyo kwa baadhi ya wanasoka wenzake wa zamani, kutokana na kupatwa na maradhi ya kupooza baadhi ya viungo vyake vya mwili. Alipatwa na maradhi hayo miaka takriban mitatu iliyopita.
Hata hivyo, hali ya Jella kwa sasa ina nafuu kwani anaweza kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kujipa mazoezi. Ameshauriwa kufanya hivyo na madaktari. Na kutokana na kuwa mdau wa soka, hupenda sana kutembelea jengo la makao makuu ya klabu ya Pan Africa, lililopo mtaa wa Swahili, Dar es Salaam. Akizungumza na Uhuru mjini Dar es Salaam hivi karibuni kuhusu mafanikio ya mchezo wa soka katika miaka 50 ya uhuru, Jella alisema Tanzania imepiga hatua kubwa hasa kutokana na uwazi uliopo katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na pia Taifa Stars kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
Hata hivyo, Jella alisema wachezaji wengi waliopo kwenye kikosi hicho hivi sasa, hawajapitia misingi mizuri ya soka tangu wakiwa wadogo, ndio sababu timu hiyo inashindwa kupata mafanikio makubwa zaidi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Jella ameishauri TFF kuwatumia wanasoka wakongwe, hasa waliocheza fainali za Afrika mwaka 1980 kwa ajili ya kutoa ushauri kwa wachezaji wa Taifa Stars ili waweze kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
"Nadhani huu unaweza kuwa msaada na mchango wetu mkubwa kwa Taifa Stars kwa sababu baadhi yetu tulicheza soka na kupata mafanikio makubwa. Tunaweza kuwaeleza mengi kuhusu mbinu za soka kuliko watu wengine,"alisema. Mkongwe huyo anayeishi maeneo ya Manzese Friends Corner, Dar es Salaam, amemtaka mshambuliaji nyota wa zamani wa Yanga na Pan African, Sunday Manara kuwa ndiye mchezaji pekee aliyekuwa akimsumbua kila alipokutana naye uwanjani.
Baadaye alikuja kuvutiwa na Zamoyoni Mogella, lakini kwa sasa haoni mchezaji yeyote mwenye mvuto licha ya kuwepo kwa wachezaji kadhaa nyota kwenye ligi kuu walionunuliwa kwa mamilioni ya pesa.
Jella alikuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Taifa Stars kucheza fainali za Afrika kwa mara ya kwanza mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria. Ndiye aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, iliyokuwa ikiundwa na nyota wengi kama vile Leodegar Tenga, Thuweni Ally, Peter Tino, Hussein Ngulungu, Juma Pondamali na wengineo.
Hata hivyo, Taifa Stars haikuweza kufanya vizuri katika fainali hizo. Katika mechi yake ya kwanza, ilichapwa mabao 3-1 na Nigeria, ilifungwa mabao 2-1 na Misri kabla ya kuilazimisha Ivory Coast kutoka nayo sare ya bao 1-1. Katika mechi zote hizo, mabao ya Taifa Stars yalifungwa na Thuweni.
Jella alianza kucheza soka tangu alipokuwa akisoma katika shule ya msingi ya Mwembesongo ya mkoani Morogoro. Kwake mpira ulikuwa ni kipaji alichojaliwa na Mungu kwani enzi zake, alikuwa beki wa aina yake na asiyetishwa ama kubabaishwa na mshambuliaji yeyote.
Alianza kucheza soka ya ushindani mwaka 1970 katika timu ya Nyota Afrika ya Morogoro. Aliteuliwa kuichezea timu ya mkoa huo katika mashindano ya Kombe la Taifa mwaka 1973, ambapo ilitwaa ubingwa baada ya kuichapa Tanga mabao 2-1 katika mechi ya fainali iliyochezwa uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Mwaka huo huo, akiwa bado anasoma shule ya sekondari ya Morogoro, uongozi wa Yanga uliokuwa chini ya mwenyekiti Tabu Mangara na meneja, Shirazi Sharrifu, ulivutiwa na kipaji chake na kuamua kumsajili. Akawa anaichezea Yanga huku akiendelea na masomo.
Alihamia rasmi katika Jiji la Dar es Salaam mwaka 1975 baada ya kumaliza masomo ya sekondari. Kikosi cha Yanga wakati huo kilikuwa kinaundwa na baadhi ya wachezaji kadhaa nyota kama vile Maulid Dilunga, Elias Michael, Abdalah Juma, Muhidin Fadhili, Athuman Kilambo, Omari Kapera, Leonard Chetete na wengineo.
Jella alikuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa klabu za Afrika Mashariki na Kati mwaka 1975 baada ya kuwabwaga watani wao wa jadi Simba mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyopigwa Zanzibar.
Aliitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa mara ya kwanza mwaka 1973 na kushiriki kwenye michuano ya Kombe la Chalenji, lakini walitolewa kwenye fainali baada ya kufungwa na Uganda mabao 2-1. Jella hakupewa nafasi ya kucheza kwenye michuano hiyo iliyofanyika mjini Kampala kutokana na umri wake kuwa mdogo.
Jella aliteuliwa kuwa nahodha wa Taifa Stars mwaka 1973 kutoka kwa Omari Zimbwe. Alishika wadhifa huo hadi mwaka 1983, ambapo nafasi hiyo ikaenda kwa kiungo Charles Boniface. Aliichezea Taifa Stars kwa miaka 10.
Mkongwe huyo aliamua kustaafu soka mwaka 1984 akiwa Pan African baada ya kuumia goti. Alilazimika kufanyiwa operesheni na daktari bingwa wa mifupa, Profesa Phillemon Sarungi.
Ameitaja sababu kubwa iliyomfanya aihame Yanga kuwa, ni mgogoro uliotokea mwaka 1976, ambao ndio uliosababisha kugawanyika kwa klabu hiyo na kuundwa kwa Pan Africa. Alikuwa mmoja wa wachezaji waanzilishi wa Pan Africa.

No comments:

Post a Comment