KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, December 2, 2011

Mr. Ebbo kuzikwa J'tatu, sababu za kifo chake zaelezwa


Na Shabani Mdoe, Arusha
MSANII maarufu wa muziki wa kizazi kipya Abel Motika maarufu kama Mr.Ebbo amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Mission Usa River wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Akizungumza na Uhuru kwa nja ya simu, msemaji wa familia hiyo ambae pia ni msanii mwenzake wa muziki huo, Fred Maliki (Mkoloni) alisema, Ebbo alifariki majira ya saa 5 usiku katika hospitali hiyo alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Mkoloni alisema Ebbo alifariki kutokana na ugonjwa uliokua ukimsumbua wa kukaukwa na damu mwilini hali iliyosababisha kupatiwa matibabu pamoja na kuongezewa damu kila mara katika hospitali mbalimbali.
Alisema Ebbo mara ya mwisho alikwenda katika hospitali ya rufaa ya KCMC mjini Moshi,ambapo alifanyiwa uchunguzi mbalimbali pasipo kuonekana sababu ya kukaukwa na damu,hali iliyolazimu kuongezewa damu.
Alisema kutokana na tatizo hilo kuonekana kuwa kubwa na la kila mara, alilazimika kuhamisha makazi yake kwa muda toka mkoani Tanga alikokuwa anafanya kazi yake ya sanaa na kuhamia eneo la Sekei jijini Arusha, ambako ndiko nyumbani kwao kwa ajili ya kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo ya Mission.
Aidha alisema katika siku za hivi karibuni, Ebbo alikuwa amepumzika nyumbani akisubiri majibu ya vipimo vyake vilivyofanyika ili kubaini tatizo lililokuwa likisababisha kukaukwa na damu kila mara.
Mkoloni alisema msanii huyo anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwao Sekei jijini Arusha siku ya jumatatu na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru ukisubiri taratibu za maziko.
Alisema Ebbo ameacha mke na watoto wawili wote wa kike wenye umri katika ya miaka 5 hadi 9 ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi.


Hadi marehemu Ebbo anafariki, alikuwa akiendelea na shughuli zake na muziki katika studio yake iliyoko mkoani Tanga ya Motika Recods na haijafahamika kama ameacha albamu au wimbo wowote mpya aliokuwa ameandaa siku za hivi karibuni.
Mara ya mwisho, msanii huyo alionekana mkoani hapa akitumbuiza katika mikutano ya kampeni za ubunge na urais za mgombea ubunge wa jimbo la Arusha kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk.Batilda Buriani.
Akizungumzia kifo hicho, Dk. Batilda alisema kimemsikitisha sana na kwamba yupo bega kwa bega na familia ya msanii huyo na wengine pamoja na watanzania wote katika kipindi hiki kigumu kwa kumuombea dua njema marehemu huyo pamoja na ndugu na watoto ili wapewe wepesi na pepo njema.
Dk.Batilda, ambaye katika baraza lililopita la mawaziri alikuwa waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais mazingira alisema, Mr. Ebbo atakumbukwa kwa mengi ikiwa ni pamoja na kuenzi mila za kabila la kimasai kwa nyimbo alizokuwa akiimba pamoja na kuhamasisha amani ya taifa.

No comments:

Post a Comment