KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, December 9, 2011

DILUNGA, MAHADHI WALIWEKA HISTORIA TANZANIA



MSHAMBULIAJI Maulid Dilunga wa Yanga na kipa Omar Mahadhi wa Simba ni wachezaji pekee wa Tanzania walioweka historia ya kuteuliwa kuunda kikosi cha Afrika.
Uteuzi huo ulifanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mara baada ya kumalizika kwa michezo ya All Africa Games, iliyofanyika mwaka 1973 mjini Lagos, Nigeria.
Katika michezo hiyo, Taifa Stars ilifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali. Katika mechi za awali, Stars ilitoka suluhu na Nigeria A, ikaichapa Nigeria B mabao 2-1 kabla ya kuzifunga Ghana na Togo bao 1-0 kila moja.
Katika hatua iliyofuata, Stars ilitoka suluhu na Nigeria, ikatoka sare ya bao 1-1 na Misri kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Algeria.
Dilunga ndiye aliyeibuka mchezaji nyota wa Taifa Stars katika michezo hiyo baada ya kuifungia mabao yote katika kila mechi.
Licha ya Stars kutolewa hatua ya nusu fainali, Dilunga na Mahadhi hawawezi kuisahau michezo hiyo kutokana na kuteuliwa kwenye kikosi cha kombani ya Afrika.
Mara baada ya uteuzi huo, kikosi hicho kilifanya ziara katika mataifa sita ya Ulaya na Amerika, ambako kilicheza mechi kadhaa za kirafiki.
Baadhi ya mataifa hayo ni Mexico, Guatemala, Uruguay, Peru, Hungary na Bulgaria. Katika ziara hiyo, kikosi hicho cha Afrika kilishinda mechi tatu, kilitoka sare mbili na kufungwa moja.
Uteuzi wa Dilunga kwenye kikosi hicho uliingia utata baada ya kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT) wakati huo, kudhani mchezaji aliyeteuliwa ni Abdalla Kibadeni.
Katika taarifa yake kwa FAT, CAF ilisema inamhitaji mchezaji aliyekuwa akivaa jezi namba 10. Na katika kikosi cha Stars wakati huo, wachezaji waliokuwa wakivaa jezi hiyo ni Dilunga na Kibadeni.
Ikabidi FAT iombe ufafanuzi kwa CAF na ndipo ilipobainika kwamba, mchezaji aliyekuwa akihitajika ni Dilunga na siyo Kibadeni.
Kilichoivutia CAF kumteua Dilunga kwenye kikosi hicho ni uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao, hasa katika mechi yao dhidi ya Nigeria B, ambapo alipachika wavuni mabao mawili.
Dilunga pia aliwahi kupata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa Ulaya mwaka 1970 wakati timu ya daraja la pili ya West Bromwich ya England ilipofanya ziara nchini.
Hata hivyo, kuna madai kuwa, aliyekuwa mwenyekiti wa FAT wakati huo, Saidi Hamad El-Maamry alimzuia kwenda huko ili aweze kuichezea Taifa Stars katika michuano ya kimataifa.
Viongozi wa West Bromwich walikuja nchini wakiwa wageni wa Yanga na baada ya kucheza mechi moja ya kirafiki, walivutiwa na uwezo wa Dilunga.
Mbali na kuzuiwa na El-Maamry kwenda Uingereza, mwamko mdogo kwa wanasoka wa Tanzania kwenda kucheza soka ya kulipwa nje nao ulichangia kumfanya Dilunga apuuze mwito huo.

No comments:

Post a Comment