KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 18, 2012

AHMED AMASHA 'MATHEMATICIAN': SIVUTIWI NA KIWANGO CHA TAIFA STARS



L Aziponda Simba na Yanga kwa kupapatikia wachezaji wa kigeni
L Ataka klabu za ligi kuu ziwekeze zaidi kwenye soka ya vijana
L Bado alikumbuka jinamizi la Yussuf Ambwene wa CDA

JINA la Ahmed Amasha si geni miongoni mwa mashabiki wa soka nchini. Ni mmoja wa wachezaji waliojipatia sifa kubwa kutokana na staili ya uchezaji wake kiasi cha kupachikwa jina la Mathematician.
Amasha alianza kujipatia umaarufu mwaka 1980 baada ya kujiunga na Tumbaku ya Iringa kabla ya kuhamishiwa Tumbaku ya Morogoro, iliyokuwa ikishiriki michuano ya ligi daraja la kwanza.
Mwaka huo huo, Amasha alichaguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, ambacho kilishiriki kwa mara ya kwanza kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika nchini Nigeria.
Katika kikosi hicho, Amasha alikuwa akicheza nafasi ya kiungo mkabaji, lakini baada ya kuumia kwa beki wa kushoto, Mohamed Kajole, Makocha Slowmir Work kutoka Poland na Joel Bendera waliamua kumuhamishia nafasi hiyo.
Amasha alicheza mechi zote tatu, ambazo Taifa Stars ilicheza katika fainali hizo. Katika mechi ya kwanza, Taifa Stars ilichapwa mabao 3-1 na wenyeji Nigeria, ikacharazwa mabao 2-1 na Misri kabla ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Ivory Coast.
Wachezaji wengine waliokuwa wakiunda kikosi cha Taifa Stars wakati huo ni Athumani Mambosasa, Mohamed Rishard Adolph, Kajole. Jella Mtagwa, Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu, Mohamed Salim, Omar Hussein, Peter Tino, Leopald Tasso Mukebezi na wengineo.
Baada ya kurejea kutoka Nigeria, Amasha alijiunga na klabu ya Yanga na kuichezea kwa miaka sita, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa ligi kuu mara tatu.
Katika kikosi hicho cha Yanga, Amasha alicheza pamoja na Hamisi Kinye, Yussuf Bana, Athumani Chama,Isihaka Hassan, Allan Shomari, Charles Boniface, Juma Mkambi, Abeid Mziba, Makumbi Juma, Saleh Hija,Hussein Iddi, Juma Kampala, Joseph Fungo na wengineo.
Amasha, ambaye aliwahi kuchaguliwa kuwa mwanasoka bora wa Tanzania mwaka 1984, aliichezea Yanga katika michuano ya ligi, klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati pamoja na klabu bingwa Afrika, ambapo timu hiyo kongwe ilikuwa ikitolewa hatua za awali.
Mwaka 1986, Amasha aliamua kuondoka nchini na kwenda Arabuni, ambako alijiunga na timu ya Fanja, iliyokuwa ikiundwa na wachezaji wengi kutoka Afrika, wakiwemo watanzania.
Wachezaji kutoka Tanzania aliocheza nao kwenye kikosi hicho ni pamoja na Twalib Hilali, Hilal Hemed na Abdulwakati Juma kutoka Zanzibar.
Alidumu Fanja kwa miaka minne, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa nchi hiyo mara kadhaa pamoja na kombe la Mfalme.
Baadaye alijiunga na klabu ya Dhofar, aliyoichezea kwa miaka minne kabla ya kuhamia Saeeb, ambayo aliichezea kwa miaka mitatu na kutwaa nayo mataji kadhaa.
Kwa sasa, Amasha ni kocha msaidizi katika klabu ya Saeeb. Aliamua kuchukua mafunzo ya ukocha na kupata leseni daraja C na B baada ya kustaafu kucheza soka.
Moja ya matukio, ambayo yataendelea kubaki kwenye kumbukumbu ya Amasha ni lile la kuvunjika mguu beki Yussuf Ambwene wa CDA katika mechi ya ligi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ambwene alivunjika mguu baada ya kugongana na Amasha wakati wakigombea mpira na jeraha hilo lilisababisha alazwe hospitali ya Muhimbili kwa wiki kadhaa na hatimaye kulazimika kuachana kabisa na soka.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Amasha alisema hakuwa amedhamiria kumuumiza Ambwene, bali waligongana kwa bahati mbaya.
Amasha alikiri kuwa, tukio hilo lilimsababishia matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na baadhi ya mashabiki kudhani alidhamiria kumuumiza mchezaji huyo kwa makusudi.
“Katika soka, jambo kama hilo kutokea ni la kawaida, lakini maneno ya watu huwezi kuyazuia. Lilitokea kwa bahati mbaya ndiyo sababu nilikuwa nikimtembelea mara kwa mara alipolazwa hospitali na hata alipokuwa Dodoma,”alisema.
Akizungumzia kiwango cha soka nchini, Amasha alisema kipo juu kwa klabu za Simba na Yanga, lakini ni cha chini kwa klabu zingine, hasa za mikoani, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Alisema alibahatika kushuhudia mechi ya ligi kuu ya watani wa jadi, Simba na Yanga iliyochezwa Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuvutiwa na viwango vya baadhi ya wachezaji.
Aliwataja wachezaji waliomvutia kuwa ni safu ya ulinzi ya Simba, iliyokuwa ikiundwa na Nassoro Masoud Cholo, Paul Ngelema, Shomari Kapombe, Juma Nyoso na Jonas Mkude.
Kwa upande wa Yanga, aliwataja wachezaji waliomvutia kuwa ni Athumani Iddi Chuji na nyota wa kigeni, Haruna Niyonzima na Didier Kavumbagu.
Amasha alisema pia kuwa, alipata nafasi ya kushuhudia mechi ya fainali ya Kombe la Kagame kati ya Yanga na Azam, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kutwaa ubingwa.
Kwa mujibu wa Amasha, katika mechi hiyo alivutiwa na viwango vya mshambuliaji John Bocco na kiungo Salum Abubakar, ambao alisema wana uwezo wa kucheza soka ya kimataifa barani Ulaya.
Amasha alilaumu tabia ya klabu kubwa za soka nchini kuwapa vipau mbele katika usajili wachezaji wa kigeni na kuwaacha wanasoka wazalendo wenye vipaji.
Alisema havutiwi na staili hiyo ya usajili kwa sababu baadhi ya wachezaji wa kigeni waliosajiliwa na Simba na Yanga, uwezo wao ni wa chini ikilinganishwa na wanasoka wazalendo.
“Enzi zetu, soka ilitiliwa umuhimu sana kuanzia shule ya sekondari. Huko ndiko tulikotokea wachezaji wengi wa zamani, ambao baadhi yetu tulichezea Simba, Yanga na Taifa Stars,”alisema.
Aliwataja baadhi ya wachezaji aliocheza nao katika michezo ya shule za sekondari nchini kuwa ni pamoja na George Kulagwa, Nico Njohole, Abbas Kuka, Rahim Rumelezi, Peter Mhina, Salim Omar, Charles Mngodo na wengineo.
Amasha alisema hafurahishwi na kiwango kinachoonyeshwa na Taifa Stars katika michuano ya kimataifa kutokana na makocha wanaoteuliwa kuinoa timu hiyo kubadili wachezaji mara kwa mara.
Alisema itakuwa vigumu kwa Taifa Stars kupata mafanikio katika michuano ya kimataifa,iwapo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halitawekeza katika soka ya vijana na kuziimarisha timu za vijana wa umri mbali mbali.
Aliipongeza klabu ya Simba kwa kuwa na timu nzuri za vijana, ikiwemo ya vijana wa chini ya miaka 20, ambayo ilifanikiwa kutwaa Kombe la Benki ABC hivi karibuni baada ya kuzifunga timu ngumu za Azam na Mtibwa Sugar.
Alisema ni vyema klabu zingine za ligi kuu kuiga mfano huo ili ziweze kuwa na timu bora hapo baadaye badala ya kutegemea wachezaji wa kigeni.
Amasha alisema inafurahisha kuona kuwa, mashabiki wa soka nchini wana mwamko mkubwa wa kuhudhuria mechi za ligi na kimataifa, lakini timu zao hazifiki mbali.
Mkongwe huyo alisema iwapo pesa zilizopo sasa katika soka zingekuwepo enzi zao, Taifa Stars iliyocheza fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980, ingekuwa na uwezo wa kucheza fainali za Kombe la Dunia.
Amasha alisema pesa zinazotumika sasa katika usajili wa wachezaji wa kigeni na kuwalipa mishahara zingekuwa zikitumika kuimarisha timu za vijana, Tanzania ingekuwa imepiga hatua kubwa kimaendeleo.
Alisema wachezaji waliokuwa wakiunda kikosi hicho walikuwa na vipaji vya aina yake na uwezo mkubwa wa kucheza soka na kuonyesha maajabu kuliko waliopo hivi sasa.
Mwanasoka huyo wa zamani alisema pia kuwa, wanasoka wa Tanzania wanashindwa kupata soko nje kutokana na vyombo vya habari nchini kuwapa kipaumbele wanasoka wa kigeni.
“Kila ukisoma magazeti na kutazama televisheni, utasikia habari za akina Okwi na Niyonzima. Hakuna wachezaji wazalendo wanaosifiwa na kama wapo ni wachache. Utaratibu huu hauwezi kuwasaidia kuwatangaza kimataifa,”alisema.
Mwanasoka huyo mkongwe anayeishi na kufanyakazi ya ukocha Arabuni ametoa mwito kwa vyama vya soka vya wilaya,mikoa na TFF kuchagua viongozi wenye sifa na kuongoza mchezo huo.
“Ni vyema kuwepo na mabadiliko katika uongozi wa soka. Tusichagua ilimradi viongozi. Tuchague watu waliowahi kucheza soka na wanaofahamu ABC ya mchezo huo,”alisema Amasha.
“Haiwezekani kwa mtu, ambaye hajawahi kucheza soka kupewa uongozi. Mtu wa aina hii hawezi kuleta mabadiliko yoyote zaidi ya kuitumia nafasi hiyo kwa maslahi yake binafsi,”aliongeza.
Amasha ametoa mwito kwa wanasoka wa Tanzania kuacha kuweka pesa mbele zaidi kuliko mchezo wenyewe. Alisema enzi zao, walikuwa wakiweka mbele zaidi uzalendo ndio sababu waliweza kucheza soka kwa miaka mingi.

No comments:

Post a Comment