'
Wednesday, October 24, 2012
YANGA RAHA TUPU
YANGA jana iliendelea kujiimarisha katika msimamo wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Polisi Morogoro mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yameiwezesha Yanga kuendelea kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza mechi tisa, nyuma ya Azam inayoshika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 18 na mabingwa watetezi Simba wanaoongoza kwa kuwa na pointi 19.
Iliwachukua Yanga dakika tano kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Simon Msuva baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Jerry Tegete.
Dakika moja baadaye, Didier Kavumbagu aliiongezea Yanga bao la pili kwa shuti kali baada ya kupokea pande kutoka kwa Athumani Iddi 'Chuji'.
Yanga nusura iongeze bao dakika ya 13 baada ya Tegete kuwatoka mabeki wawili wa Polisi, lakini shuti lake lilimbabatiza beki mmoja na kuwa kona, ambayo haikuzaa matunda.
Msuva angeweza kufunga bao dakika ya 21 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Tegete, aliyewatoka mabeki wawili wa Polisi, lakini shuti lake lilidakwa na kipa Kondo Salum, aliyeingia dakika ya 19 kuchukua nafasi ya Kulwa Manji, aliyeumia.
Polisi ilifanya shambulizi kali langoni mwa Yanga dakika ya 25 wakati Nadir Haroub na Chuji walipotegeana kuokoa mpira, lakini shuti la Nicholas Jabipe lilitoka sentimita chache nje ya lango.
Vijana wa Polisi walifanya shambulizi lingine dakika ya 35 wakati Mokili Rambo alipomtoka Chuji na kufumua kiki kali, lakini ilitoka nje.
Mwamuzi Alex Mahagi kutoka Mwanza aliizawadia Yanga penalti dakika ya 37 baada ya Msuva kuvutwa jezi na beki John Bosco ndani ya eneo la hatari, lakini shuti la Haruna Niyonzima liligonga mwamba na kuokolewa na mabeki wa Polisi.
Polisi walipata nafasi nzuri za kufunga dakika ya 41 na 41, lakini shuti la Bantu Admini lilidakwa na kipa Ally Mustafa wakati lile la Malimi Busungu lilitoka nje ya lango. Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Timu zote mbili zilikianza kipindi cha pili kwa kasi, lakini ni Yanga iliyopata nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 51 wakati Tegete alipounganishwa kwa kichwa krosi kutoka kwa Niyonzima, lakini mpira ulitoka nje.
Hamisi Kiiza aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 58 kwa shuti kali la mguu wa kulia baada ya kupokea pasi kutoka kwa Luhende.
YANGA: Ally Mustapha, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Mbuyu Twite, Athumani Iddi, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/ Nurdin Bakari, Jerry Tegete/ Hamisi Kiiza, Didier Kavumbagu, David Luhende.
POLISI: Manji Kulwa/ Kondo Salum, Nahodha Bakari, John Bosco, Noel Msakwa, Salmini Kisi, Hamisi Mamiwa, Bantu Admini, Paschal Maige, Mokili Rambo, Malimi Busungu, Nicholas Jabipe.
Wakati huo huo, Azam leo ilishindwa kutwaa uongozi wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Sare hiyo imeifanya Azam iendelee kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi nane wakati Ruvu Shooting ni ya 10 ikiwa na pointi 10.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Coastal Union iliichapa African Lyon bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Bao pekee na la ushindi la Coastal lilifungwa na Nsa Job dakika ya 47.
Nazo Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa Manungu uliopo Turiani mjini Morogoro.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment