KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 10, 2012

ZIPO WAPI TIKETI ZA ELEKTRONIKI ZA CRDB?

MAPEMA mwaka huu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kuwa, Benki ya CRDB PLC iliibuka mshindi wa tenda ya kutengeneza tiketi za elektroniki kwa ajili ya kuingilia uwanjani iliyotangazwa na shirikisho hilo.
Kwa mujibu wa TFF, kampuni saba zilijitokeza katika hatua ya awali ya kuonyesha nia (Expression of Interest) kwa ajili ya tenda hiyo, ambapo Aprili 19 mwaka huu, Kamati ya Mipango na Fedha ya shirikisho hilo, ambayo ndiyo Bodi ya Tenda, ilipitia maombi hayo na kupitisha manne.
Baadaye kampuni hizo nne; CRDB Bank PLC, Prime Time Promotions, Punchlines (T) Limited na SKIDATA People Access Inc zilitakiwa kuwasilisha rasmi tenda zao, zikionesha jinsi zitakavyofanya shughuli hiyo pamoja na gharama ya utengenezaji kwa tiketi moja.
Bodi ya Tenda ya TFF ilikutana Julai 13 mwaka huu kwa ajili ya kupitia tenda hizo, ambapo kampuni zote nne zilifanya uwasilishaji (presentation) wa jinsi zitakavyofanya shughuli hiyo, na baadaye kuipa kazi hiyo benki ya CRDB.
Uamuzi huo wa Bodi ya Tenda uliwasilishwa mbele ya Kamati ya Utendaji ya TFF, ambayo katika kikao chake kilichofanyika Julai 14 mwaka huu, iliridhia uteuzi huo wa benki ya CRDB.
Baadhi ya vigezo, ambavyo Bodi ya Tenda ya TFF iliangalia na kuipa CRDB tenda hiyo ni uwezo wa kufanya kazi hiyo (capacity), hadhi yake mbele ya jamii (credibility) katika shughuli inazofanya na teknolojia ya kisasa itakayotumika kutengeneza tiketi hizo.
Uamuzi huo wa TFF kutangaza tenda hizo ulilenga kuimarisha udhibiti wa mapato ya milangoni na kurahisisha mtiririko mzima wa mashabiki kupata tiketi na kuingia viwanjani. Benki hiyo ilipaswa kuanza kazi hiyo mara moja.
Nakumbuka Rais wa TFF, Leodegar Tenga akizungumzia suala hilo alisema: “Hatua hii ni muhimu sana, kwani tulikuwa tukiisubiri kwa muda mrefu. Si tu itaimarisha udhibiti wa mapato, bali pia itaondoa matatizo ya tiketi na kuendelea kujenga credibility (kuaminika) ya TFF. Mafanikio haya si kwa TFF pekee bali mpira wa miguu kwa ujumla.”
Kwa mujibu wa Tenga, CRDB ilishaanza mara moja mchakato wa shughuli hiyo na tiketi hizo zilipaswa kuanza kutumika kutumika rasmi katika kipindi cha kati ya miezi miwili na mitatu kuanzia wakati huo.
Huu sasa ni mwezi Oktoba. Ni takriban miezi mitatu imeshapita tangu Bodi ya Tenda ya TFF ilipoiteua CRDB kusimamia kazi hiyo, lakini hakuna chochote kilichoanza kufanyika.
Bahati mbaya sana ni kwamba, sisi waandishi wa habari ni wepesi sana wa kusahau mambo. Huwa tunapenda kulishabikia jambo pale linapotangazwa, lakini baada ya muda kupita, tunalisahau na kuzama kwenye mambo mengine kabisa. Hakuna mwandishi yeyote aliyewahi kuwauliza viongozi wa TFF ni kwa nini uuzaji wa tiketi hizo haujaanza na tatizo ni nini?
Jambo hilo ndilo lililonisukuma kupitia kwenye safu hii kuhoji ni kwa nini CRDB imeshindwa kuanza kazi ya kuuza tiketi za kuingilia uwanjani kwa njia ya elektroniki, ambayo tulielezwa kwamba ingeongeza ufanisi na kudhibiti wizi wa mapato?
Sababu nyingine iliyonisukuma kuhoji jambo hilo ni uchache wa mapato yaliyopatikana katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, kati ya Simba na Yanga iliyochezwa Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mechi hiyo iliripotiwa kuingiza sh. milioni 390.
Kwa watu walioshuhudia mechi ile, bila shaka watakubaliana na safu hii kwamba, kiwango hicho cha mapato ilikuwa ni sawa na kiini macho, hasa ikizingatiwa kuwa, idadi ya mashabiki walioingia uwanjani ilikuwa ni kubwa mno kuliko hata mechi zilizoripotiwa kuingiza sh. milioni 400 hadi 600.
Swali la kujiuliza ni kwa nini mapato yaliyotangazwa kupatikana katika mechi hiyo yalikuwa kidogo wakati idadi ya mashabiki walioingia uwanjani ilikuwa ni kubwa? Kuna mchezo gani unaochezwa katika kudhibiti mapato ya Uwanja wa Taifa?
Katika mazingira ya kawaida tu, ambayo pengine hayahitaji mtu kuwa amesoma sana ili kuweza kung'amua jambo, ni dhahiri kwamba ndani ya TFF kuna watu, ambao hawakuvutiwa na uamuzi wa kuipa CRDB tenda ya kuuza tiketi za kuingilia uwanjani na kwa makusudi wameamua kuukwamisha mpango huo.
Nadhani ni vyema TFF ieleze wazi kuhusu sababu za kukwama kwa CRDB kuanza kazi hiyo na ni nani kikwazo ili watanzania waweze kufahamu ukweli wa mambo badala ya kuendelea kukaa kimya na hivyo kuacha maswali mengi.
Ukimya huu wa viongozi wa TFF ndio unaowafanya watanzania waanze kupata shaka kuhusu kukwama kwa mpango huo na kujenga hisia kwamba, huenda kuna mtandao mkubwa unaojihusisha na wizi wa mapato yanayopatikana kwenye uwanja huo na haupo tayari kutoa nafasi hiyo kwa CRDB kwa vile benki hiyo itakwamisha mipango yao.

No comments:

Post a Comment