KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, October 16, 2012

MINTANGA AACHIWA HURU


Na Njumai Ngota
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imemwachia huru aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa nchini (BFT), Alhaji Shaaban Mintanga, aliyeshtakiwa kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.
Kuachiwa huru kwa Mintanga, kumetokana na mahakama kueleza kuwa, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Jaji Dk. Fauz Twalib alitoa uamuzi huo jana, kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani, mbele yake ili kuamua endapo mshtakiwa huyo ana kesi ya kujibu au la.
Mintanga alikuwa akikabiliwa na mashtaka mawili ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa Jaji Twaib, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi wanne, ambao ni Christopher Mutarukwa, Nassoro Irenge, Emilia Poliano na Charles Ulaya.
Alisema ushahidi wa Ulaya umezua hali ya kujikanganya katika kesi ya upande wa mashtaka, ikiwemo uzito wa dawa za kulevya, ambao kwenye hati ya kuonyesha thamani yake, inaelezwa ni kilo 4.8 na kwenye kielelezo cha nukushi kutoka Mauritius, inaonyesha ni kilo sita.
Jaji alisema ripoti kamili aliyopewa shahidi huyo hakuiwasilisha mahakamani kama kielelezo na hakuna shahidi yeyote aliyetoa ushahidi kuhusu idadi ya kilo za dawa hizo.
Alisema tangu awali, aliyekuwa akitafutwa kuhusika na usafirishaji wa dawa hizo ni mtuhumiwa Mika na si Mintanga na kwamba, mtuhumiwa Msengwa, ambaye anashikiliwa Mauritius, kwenye maelezo yake alisema hamfahamu Mintanga.
Ulaya katika ushahidi wake alidai kuwa, Msengwa alipatiwa dawa hizo na Mika katika hoteli iliyopo eneo la Manzese, Dar es Salaam na alikuwa akiwasiliana na mwanamke raia wa Kenya.
Jaji alisema upande wa mashtaka pia umeshindwa kuthibitisha mahali na tarehe, ambayo washtakiwa walikula njama.
Baada ya mahakama kumwachia huru Mintanga, ndugu, jamaa na marafiki waliokuwepo mahakamani walijawa na furaha kubwa na kumchukua ndugu yao na kutoweka naye.
Mintanga alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam, Julai 7, 2008 na hadi alipoachiwa huru, alikuwa amekaa rumande kwa zaidi ya miaka mitatu.

No comments:

Post a Comment