KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 24, 2012

MILOVAN AWATOSA BOBAN NA NYOSO




KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema hajutii kuwakosa beki Juma Nyoso na mshambuliaji Haruna Moshi 'Boban', ambao wamesimamishwa na uongozi kwa muda usiojulikana.
Kocha huyo kutoka Serbia ameelezea msimamo wake huo siku moja baada ya uongozi wa Simba kutangaza kuwasimamisha wachezaji hao kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Milovan alisema wachezaji hao wanastahili adhabu waliyopewa na uongozi kwa vile wamekithiri kwa utovu wa nidhamu na pia ni chanzo cha timu kufanya vibaya katika michuano ya ligi.
Kocha huyo alisema, licha ya wachezaji hao kuwa muhimu kwenye kikosi chake na kusimamishwa kwao ni pengo katika timu, suala la nidhamu ni la muhimu zaidi kuliko mchezaji binafsi.
"Boban na Nyoso ni wachezaji wazuri na wanapokosekana katika timu huwa inapwaya, lakini mambo wanayofanya hayawezi kuvumilika,"alisema.
Hata hivyo, Milovan alisema kikosi chake kinaundwa na wachezaji wengi wazuri, wakiwemo waliopandishwa daraja msimu huu, hivyo anaamini timu itaweza kufanya vizuri bila kuwepo kwao.
"Hata Ulaya wachezaji nyota wanapokosa nidhamu, husimamishwa lakini, wapo wengine ambao huchukua nafasi zao na timu ikafanya vizuri, hivyo kusimamishwa kwao kwa utovu wa nidhamu hata mimi naafiki," alisema Cirkovic.
Alisema kwa sasa, timu yake inaendelea na mazoezi ya kujiwinda na mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Azam utakaofanyika keshokutwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mapema jana, Simba kupitia kwa ofisa wake wa habari, Ezekiel Kamwaga ilitangaza jana kuwa, imemsimamisha Boban kuichezea timu ya wakubwa kutokana na vitendo vyake vya utovu wa nidhamu na pia kutokuwa na heshima kwa mwajiri wake.
Kamwaga alisema uongozi umempa Boban siku 21 kutoa maelezo kuhusu makosa yake na iwapo atashindwa kufanya hivyo, klabu inaweza kumchukulia hatua kali zaidi za kinidhamu.
Ofisa huyo alisema, katika kipindi hicho cha siku 21, Boban atalipwa nusu ya mshahara wake wa kila mwezi na hatapata marupurupu yoyote yanayohusiana na timu ya wakubwa.
Akimzungumzia Nyoso, ofisa huyo alisema uongozi umemwagiza afanye mazoezi na kikosi cha timu ya pili ya Simba B hadi hapo atakapoimarisha kiwango chake cha uchezaji.
Alisema hatua hiyo imetokana na ripoti ya benchi la ufundi kuonyesha kuwa, mchezaji huyo amekuwa akifanya makosa mengi uwanjani yanayoigharimu timu, na ingawa amekuwa akipewa maelekezo na walimu, bado amekuwa akiyarudia mara kwa mara.
Kamwaga alisema, kutokana na kosa hilo, Nyoso atafanya mazoezi na wachezaji wa kikosi cha pili hadi walimu watakaporidhika kwamba amejirekebisha na yuko tayari kukitumikia kikosi cha wakubwa.
Aliongeza kuwa, katika muda wote huo atakaokuwa akifanya mazoezi na timu B, Nyoso atakuwa akipata mshahara wake wa kila mwezi kama kawaida na pia atapata marupurupu wanayopata wachezaji wa timu hiyo.

No comments:

Post a Comment