'
Tuesday, October 30, 2012
KAMATI YA LIGI YAWAOMBA RADHI WANAHABARI
1. Kamati ya Ligi jana (Oktoba 29,2012) ilifanya kikao pamoja na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom kujadili mambo kadhaa, likiwemo tukio la Jumamosi iliyopita la kuzuia televisheni na radio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu pamoja na wapiga picha za televisheni kuchukua picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari. Kamati ilifanya mazungumzo na mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), Juma Pinto kuhusu msukosuko huo na kufikia muafaka katika masuala yafuatayo:
a- kwamba uamuzi wa kuzuia vituo vya redio na televisheni kutangaza moja kwa moja ulikuwa sahihi lakini una kasoro katika utekelezaji kwa kuwa hayakuwepo mawasiliano rasmi kwa vyombo vya habari na pia haukutoa muda wa kutosha kwa vyombo hivyo vya habari kufanya maandalizi kwa kadri ya utashi wa klabu za Ligi Kuu.
b- Kwamba Kamati ya Ligi haijakataza redio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu, bali vituo vya redio ambavyo vinataka kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu vifanye hivyo bila ya kuweka matangazo ya wadhamini na kama matangazo hayo ya moja kwa moja yatadhaminiwa, basi vituo hivyo havina budi kuwasiliana kwa maandishi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa maelekezo zaidi.
c- Kwamba vituo vya redio vitakavyotaka kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu, ni lazima zitamke mashindano hayo kuwa ni “Ligi Kuu ya Vodacom”.
d- Kwamba vituo vya televisheni vitakavyotaka kutangaza moja kwa michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom, ni lazima viingie mkataba na TFF ambao utaaridhiwa na klabu husika. Kwa sasa, kituo cha televisheni cha Star TV hakitaruhusiwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya michezo hiyo hadi hapo mkataba utakaposainiwa na tunatumaini mkataba huo utasainiwa kabla ya mechi za kesho na hivyo kuwapa fursa wapenzi wa soka wa maeneo mbalimbali kuendelea kushuhudia Ligi Kuu ya Vodacom.
e- Kwamba vituo vya televisheni vitakavyotaka kuchukua picha kwa ajili ya habari zinaruhusiwa kufanya hivyo. Endapo kituo hicho kitaonyesha mchezo uliorekodiwa, hatua zitachukuliwa dhidi ya kituo hicho.
f- Kamati inaomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa na uamuzi huo, lakini inazidi kusisitiza kuwa uamuzi huo ulifanywa kwa lengo zuri la kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vitakavyoziwezesha klabu kujimudu kiuchumi na kuifanya Ligi Kuu ya Vodacom iendeshwe kwa ubora zaidi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment