'
Thursday, October 18, 2012
YONDAN: ACHENI KUNICHONGANISHA NA BOBAN
KITENDO cha kiungo Haruna Moshi 'Boban' wa Simba kumchezea rafu mbaya beki, Kelvin Yondan wa Yanga kilipokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa soka nchini, hasa wa klabu hizo mbili kongwe na zenye mashabiki lukuki.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 3 mwaka huu wakati Simba ilipomenyana na Yanga katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi hiyo, timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Wapo waliomuona Boban kuwa alifanya kitendo kile kwa makusudi kwa lengo la kupunguza makali ya safu ya ulinzi ya Yanga, iliyokuwa ikiongozwa na Yondan, lakini wengine walilitafsiri kuwa ni tukio la kawaida katika soka.
Siku chache baada ya mechi hiyo, Boban alijitokeza hadharani na kumuomba radhi Yondan pamoja na mashabiki wa Yanga kwa madai kuwa, tukio hilo lilikuwa la bahati mbaya na kwamba hakuwa amedhamiria kumuumiza mchezaji mwenzake huyo wa zamani wa Simba.
Boban alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa, yeye na Yondan walikuwa marafiki wakubwa walipokuwa pamoja Simba na kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, hivyo isingekuwa rahisi kudhamiria kumvunja.
Kufuatia rafu hiyo, Yondan alilazimika kukaa nje ya uwanja kwa wiki mbili, akiuguza mguu wake, ambao ulivunjika mfupa mdogo. Tayari beki huyo ameshaanza mazoezi na wenzake na anatarajiwa kurejea uwanjani hivi karibuni.
Tukio hilo pia lilisababisha mwamuzi Mathew Akrama kutoka Mwanza, aliyechezesha mechi hiyo, aondolewe kwenye orodha ya waamuzi kwa kosa la kuvurunda na pia kushindwa kumuonyesha kadi nyekundu Boban kutokana na kutenda kosa hilo.
Akihojiwa na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Yondan alisema anaamini Boban hakuwa amekusudia kumvunja mguu kwa makusudi bali ni tukio la bahati mbaya na kawaida katika soka.
Yondan alisema hana kinyongo na Boban kutokana na rafu hiyo na kusisitiza kuwa, ni rafiki yake wa karibu na amekuwa akimtembelea mara kadhaa ikiwa ni pamoja na kumuomba radhi.
"Nawaomba mashabiki wa Yanga watulie na kuniombea dua nirudi uwanjani mapema na nikiwa na afya njema,"alisema Boban, ambaye aliwashukuru viongozi wa Yanga kwa kusimamia matibabu yake kwa umakini mkubwa.
Kwa mujibu wa Yondan, Boban alimfuata nyumbani kwake siku chache baada ya mchezo ule na kumuomba radhi kutokana na tukio lile na kusisitiza kuwa, uamuzi wake huo ulimfanya amuone muungwana.
"Binafsi nilimuelewa na kumsamehe kwa vile kitendo alichokifanya ni cha kiungwana na kiuanamichezo. Nawaomba mashabiki wasitumie tukio lile kunichonganisha na Boban. Wasiwe na kinyongo naye chochote,"alisisitiza.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi wake wa kuihama Simba na kujiunga na Yanga, Yondan alikiri kwamba ulikuwa mgumu kwa vile alikumbana na vipingamizi vingi kutoka kwa viongozi na wanachama wa Simba.
Yondan alisema binafsi aliamua kujiunga na Yanga kutokana na ofa nzuri aliyopewa na viongozi wa klabu hiyo na kuongeza kuwa, lengo la mwanasoka yeyote siku zote huwa ni kukitumia kipaji chake kupata pesa za kuweza kuyaendesha vizuri maisha yake.
"Viongozi wa Yanga wamenipa mkataba mzuri, ambao ndani yake kuna vitu vingi, ambavyo kwa asilimia kubwa vimetimizwa. Kwa sasa nina furaha kubwa ya kuichezea Yanga," alisema beki huyo kisiki.
Yondan amewashukuru viongozi, wanachama na wachezaji wenzake kwa kumpa ushirikiano mzuri tangu alipojiunga na klabu hiyo na kuongeza kuwa, lengo lake kubwa ni kusaidia ili iweze kufanya vizuri katika michuano mbali mbali.
Beki huyo alikiri kuwa, changamoto kubwa inayomkabili kwa sasa ni kupigania namba kwenye kikosi cha kwanza kutokana na ukweli kwamba, timu hiyo inaundwa na wachezaji wengi wazuri katika idara zote.
Yondan pia aliwashukuru viongozi na wanachama wa Simba kwa kumpa ushirikiano mkubwa alipokuwa akiichezea timu hiyo na kusisitiza kuwa, kuondoka kwake kulilenga kutafuta malisho mazuri zaidi.
"Unajua soka ni mchezo wa muda mfupi, ukifanya makosa unaweza kujiharibia kila kitu, hivyo mchezaji unapaswa kuwa makini katika kujenga maisha yako ya baadaye,"alisema.
Yondan alisema ameondoka Simba akiwa hana kinyongo na kiongozi ama mchezaji yeyote na kwamba hata anapokutana nao, wamekuwa wakisalimiana na kuzungumza vizuri.
Beki huyo kisiki wa Yanga alisema, katika muda wote ambao amekuwa akicheza soka, amekutana na changamoto nyingi na kubaini kuwepo kwa vitu vingi ndani ya soka, lakini ni mapema kuvizungumza kwa sasa.
Alisisitiza kuwa, jambo la muhimu ni kwa viongozi wa klabu za soka kuwatimizia wachezaji wao yale yanayokuwemo kwenye mikataba kati yao na kuacha kutoa ahadi zisizotekelezeka.
Alisema matatizo mengi yanayotokea sasa kati ya wachezaji na viongozi wa klabu, yanatokana na viongozi kupenda kutoa ahadi kwa wachezaji na kuwatelekeza wanapopatwa na matatizo.
Ametoa ushauri kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutilia mkazo ufuatiliaji wa vipaji vya vijana na kuwaendeleza kwa kuwekeza zaidi kwenye soka la vijana na kuziimarisha timu za taifa za vijana wa umri mbali mbali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment