'
Wednesday, August 14, 2013
USAJILI LIGI KUU NGOMA BADO NZITO
HATMA ya usajili wa mshambuliaji Mrisho Ngasa imeendelea kuwa kitendawili baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kushindwa kukutana juzi.
Kamati hiyo ilishindwa kukutana juzi na jana kutokana na idadi ya wajumbe wake kushindwa kutimia.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kamati hiyo sasa itakutana leo kuanzia saa nne asubuhi.
"Mwenyekiti wa kamati hiyo Alex Mgongolwa amepanga tarehe hiyo mpya baada ya kikao cha jana na leo kushindwa kupata akidi,"alisema.
Kwa mujibu Wambura, ili kamati hiyo yenye wajumbe saba iweze kufanya kikao, ni lazima wapatikane wajumbe wanne.
Kutofanyika kwa kikao hicho kumesababisha usajili wa Ngasa uendelee kuwa kitendawili kutokana na klabu za Simba na Yanga kuwasilisha jina lake kwenye usajili wao.
Simba ilimsajili mchezaji huyo kwa mkopo msimu uliopita akitokea Azam kabla ya kuhamia Yanga msimu huu baada ya mkataba wake kumalizika.
Uongozi wa Simba umekuwa ukidai kuwa, Ngasa aliingia mkataba mwingine na timu hiyo alipokuwa bado yupo kwenye mkopo na umewasilishwa TFF, lakini mchezaji huyo amekana akidai kuwa, hakufanya kitu kama hicho.
Kutokana na kutofanyika kwa kikao hicho, Ngasa huenda akashindwa kuichezea Yanga keshokutwa itakapomenyana na Azam katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment