KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, August 5, 2013

MSAJILI AIDHINISHA MAREKEBISHO YA KATIBA TFF, TENGA ATOA SHUKURANI


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amemshukuru Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kwa kusajili Katiba ya TFF toleo la 2013 kutokana na marekebisho yaliyofanywa na Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika Julai 13 mwaka huu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo (Agosti 5 mwaka huu), Rais Tenga ameishukuru Serikali, Msajili, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, Naibu wake Amos Makala na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa ushirikiano ambao wametoa kwa TFF katika kufanikisha suala hilo.

Amesema baada ya kupokea usajili huo, kinachofuata ni Katibu Mkuu wa TFF kumwandikia rasmi Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ili aanzishe mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa TFF.

Kuhusu kauli ya Naibu Waziri Makala kuwa marekebisho hayo yasingeweza kusajiliwa kwa sababu hayakufuata Katiba ya TFF, Rais Tenga amesema alikuwa ana haki ya kusema hivyo kwa sababu hakuwepo kwenye Mkutano huo, na kuongeza:

“Makala hakuwepo kwenye mkutano ndiyo maana alisema hivyo. Ana haki ya kuuliza, nina hakika sasa atakuwa ameeleweshwa na ameelewa kwa sababu ni msikivu. Kuhusu marekebisho hayo kupigiwa kura, hilo lisingefanyika kwa sababu hakukuwa na mjumbe aliyepinga marekebisho,” amesema.

Rais Tenga amesema marekebisho hayo yalipitishwa kwa kauli moja (unanimous) hivyo hakukuwa na sababu ya kuanza kunyoosha mikono kupiga kura, kwa maana hiyo mkutano ulipitisha marekebisho kwa asilimia 100 wakati Katiba ilikuwa ikihitaji theluthi mbili tu.

“Hakukuwa na dispute (mabishano) kuhusu marekebisho, isipokuwa wajumbe walitumia muda mwingi kuboresha kanuni na kutoa ushauri wa aina ya watu ambao wangeingia kwenye kamati mbalimbali zikiwemo zile mpya za Maadili,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa vile wote walioingia kwenye Mkutano Mkuu huo Maalumu ni watu wa mpira wa miguu wasingeweza kupinga marekebisho kwa vile yametokana na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

“Labda itokee aliyeingia kwenye mkutano alikosea njia. Mtu yeyote wa mpira wa miguu ni lazima afahamu kuwa maagizo ya FIFA ni lazima yatekelezwe, na Katiba ya TFF inasema hivyo,” amesema Rais Tenga.

Pia Rais Tenga amewataka wapenzi wa mpira wa miguu kushawishi watu wenye sifa na uwezo wa kuongoza kujitokeza kwa wingi wakati Kamati ya Uchaguzi itakapotangaza mchakato na tarehe ya uchaguzi huo.

AZAM YAANZA ZIARA KWA KUIKABILI KAISER CHIEFS
Makamu bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Azam wanaanza rasmi ziara ya mechi za kirafiki nchini Afrika Kusini leo kwa kuikabili timu ya Kaiser Chiefs ambayo inacheza Ligi Kuu ya nchi hiyo (PSL).

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Azam, Jaffer Idd aliyefutana na timu hiyo, mechi hiyo inachezwa jijini Johannesburg. Idd anapatikana kwa namba +27788847399.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment