KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 1, 2013

WACHEZAJI STARS WAPASUA BOMU


BAADHI ya wachezaji wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars wameamua kupasua bomu kwa kusema Kocha Kim Poulsen amekuwa akiwakumbatia wachezaji, ambao kiwango chao kimeshuka.

Wakizungumza na Burudani kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wachezaji hao walisema baadhi ya wachezaji wenzao kwa sasa hawastahili kuendelea kuwemo kwenye kikosi hicho.

Mbali na baadhi yao kushuka kiwango, wachezaji hao walisema baadhi ya chipukizi walioitwa kwenye kikosi hicho bado hawajawiva kuichezea Taifa Stars na wanahitaji kupewa muda zaidi.

Mmoja wa wachezaji waandamizi wa timu hiyo alisema, mchezaji kama Erasto Nyoni, Mwinyi Kazimoto na Vicent Barnabas hawastahili kuwemo kwenye kikosi hicho kwa vile kiwango chao kimeshuka.

"Nyoni amekuwa akifanya makosa ya kizembe tangu tulipocheza na Morocco na Ivory Coast, lakini hatuelewi kwa nini kocha amekuwa akiendelea kumng'ang'ania," alisema mchezaji huyo kutoka moja ya klabu kubwa na kongwe nchini.

"Katika mechi yetu dhidi ya Ivory Coast, hata baadhi ya mashabiki walidiriki kumzomea kocha wakitaka amtoe Nyoni. Hili jambo lipo wazi hata kwa Barnabas, ambaye amekuwa akichezeshwa nafasi, ambayo sio yake,"alisema mchezaji huyo.

Aliongeza kuwa, kiwango cha Kazimoto kimeshuka tangu msimu uliopita wa ligi na amekuwa akishindwa kucheza vizuri kama ilivyokuwa misimu mitatu iliyopita, hivyo hastahili kuwemo kwenye kikosi hicho.

Mchezaji huyo mkongwe alisema pia kuwa, hawaelewi ni kwa nini Kocha Poulsen amemuita Barnabas kwenye kikosi hicho wakati hayuko katika kiwango kizuri kama ilivyokuwa miaka minne iliyopita.

Mmoja wa viungo wa timu hiyo alisema, hawaelewi kwa nini Poulsen amekuwa hamtumii Athumani Iddi 'Chuji', ambaye ana uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa ikilinganishwa na Frank Dumayo, Salum Abubakar na Kazimoto.

Hata hivyo, wachezaji hao wamemsifu mshambuliaji chipukizi, Haruna Chanongo kwa kusema kuwa, ameonyesha mwanzo mzuri na iwapo ataendelea kupatiwa nafasi mara kwa mara, atakuwa tegemeo kubwa la timu hiyo.

Wachezaji hao wamemshauri Poulsen awashirikishe viongozi wenzake wa benchi la ufundi katika upangaji wa timu na ikiwezekana aombe ushauri kwa wachezaji wake.

Wachezaji hao wa Taifa Stars walisema wanaishukuru Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa udhamini wao mzuri kwa timu hiyo na kusisitiza kuwa, hawana deni lolote wanalodai kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

"Kusema ule ukweli, tunaishukuru sana TBL na TFF kwa maandalizi, ambayo zimekuwa zikiyafanya kwetu na hatudai kitu chochote kutoka kwao, ziwe posho za kusafiri nje au kambini, tumelipwa kila kitu,"alisisitiza.

Kauli ya wachezaji hao ni kama ya kumuunga mkono nahodha wa timu hiyo, Juma Kaseja, ambaye alikaririwa mwishoni mwa wiki iliyopita akisema kuwa, baadhi ya wachezaji chipukizi wameiangusha timu hiyo.

Kaseja alisema anaunga mkono uamuzi wa Poulsen kuwaita baadhi ya wachezaji chipukizi kwa lengo la kuwapa uzoefu, lakini baadhi yao hawastahili kwa vile uwezo wao bado mdogo.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Kaseja ilipingwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, ambaye alisema, wanaunga mkono uamuzi wa Poulsen kuwajumuisha chipukizi kwenye kikosi hicho kwa vile hiyo ndiyo sera aliyopewa.

No comments:

Post a Comment