Hassan Bitchuka, mwimbaji nyota wa Mlimani Park Orchestra
Shabani Dede, mwimbaji nyota wa Msondo Ngoma
Ally Choki, kiongozi na mwimbaji nyota wa Extra Bongo
Isha Mashauzi, kiongozi na mwimbaji wa Mashauzi Classic
Kalala Junior, kiongozi na mwimbaji wa bendi ya Twanga Pepeta
KUMBI mbalimbali za burudani za mjini Dar es Salaam leo na kesho zinatarajiwa kuwaka moto wakati bendi za muziki wa dansi na vikundi vya taarab vitakapofanya maonyesho ya kusherehekea sikukuu ya Idd el Fitr.
Katika maonyesho hayo, bendi kongwe ya muziki wa dansi nchini, Mlimani Park Orchestra (Sikinde) itahanikiza maraha kwenye ukumbi wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam.
Katibu wa Mlimani Park Orchestra, Hamisi Milambo alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, katika onyesho hilo, bendi hiyo itaporomosha vibao viwili vipya.
Alivitaja vibao hivyo kuwa ni Tabasamu Tamu na Dole Gumba vilivyotungwa na mwimbaji nyota nchini, Hassan Bitchuka.
Milambo alisema bendi yake pia inatarajia kulitumia onyesho hilo na mengineyo ya sikukuu ya Idd el Fitr kumtambulisha mpiga solo wake mpya, Adolph Mbinga, ambaye amewahi kupigia bendi mbalimbali maarufu nchini kama vile Twanga Pepeta na Mchinga Sound.
Kwa mujibu wa Milambo, siku ya Idd Pili bendi hiyo itafanya onyesho kwenye ukumbi wa Pentagon uliopo Kurasini wakati Idd Tatu itafanya onyesho kweny bwalo la maofisa wa Magereza, Ukonga, Dar es Salaam.
Bendi nyingine kongwe nchini, Msondo Ngoma itasherehekea sikukuu ya Idd el Fitr kwa kufanya onyesho kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti alisema juzi kuwa, katika onyesho hilo, bendi yake itatambulisha nyimbo nne mpya, Dawa ya deni (Huruka Uvuruge), Lipi jema (Eddo Sanga), Nadhiri (Juma Katundu) na Suluhu (Shabani Dede).
Kibiriti alisema siku ya Idd Pili, bendi hiyo itafanya onyesho kwenye ukumbi wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam wakati Idd Tatu itahamishia burudani kwenye klabu ya Ghymkhana iliyopo visiwani Zanzibar.
Bendi ya Extra Bongo inayoongozwa na mwimbaji machachari Ally Choki, itasherehekea sikukuu hiyo Idd Mosi kwa kufanya onyesho kwenye ukumbi wa Meeda uliopo Sinza, Dar es Salaam.
Choki alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, siku ya Idd Pili, bendi hiyo itatoa burudani kwenye ukumbi wa Dar Live ulioko Mbagala, Dar es Salaam.
Katika maonyesho hayo, Choki alisema bendi hiyo itawatambulisha wacheza shoo wake wawili wapya wa kike na pia kuporomosha vibao vipya vitatu. Alivitaja vibao hivyo kuwa ni Tuwalinde wanawake (Papii Katalogi), Hafidhi (Athanas) na Mgeni (Khadija Mnoga).
"Nawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kushuhudia mambo mapya kutoka kwetu,"alisema Choki.
Kikundi cha taarab cha Five Stars kitasherehekea sikukuu hiyo siku ya Idd Mosi kwa kufanya onyesho katika kitongoji cha Kigogo Fresh kilichopo Pugu, Ilala, Dar es Salaam.
Kiongozi wa kundi hilo, Ally J alisema juzi kuwa, siku ya Idd Pili, kundi hilo litatoa burudani kwenye ukumbi wa Roshi Garden ulioko Mwandege, Mbagala, Dar es Salaam wakati siku ya Idd Tatu itahanikiza maraha Kibiti, Rufiji mkoani Pwani.
Ally J alisema katika maonyesho hayo, kundi hilo litatambulisha kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la Habari ya mjini.
Kundi la muziki wa taarab la Dar Modern litasherehekea siku ya Idd Mosi kwa kushusha burudani nzito kwenye kiota kipya cha maraha kinachojulikana kwa jina la Serengeti Golden Paradise Resort, Mbagala, Mbande, Dar es Salaam.
Meneja wa hoteli hiyo, Wambura Sungura alisema juzi kuwa, kundi hilo limeahidi kuporomosha vibao vyake vipya zaidi ya vitano, vitakavyokuwemo kwenye albamu yao mpya.
Sungura amewataka wakazi wa Mbagala na vitongoji vya jirani kufika kwa wingi kwenye ukumbi huo ili kupata burudani adhimu kutoka katika kundi hilo, ambalo lilikuwa kimya kwa zaidi ya miezi miwili.
Kwa mujibu wa Sungura, kabla ya burudani hiyo, kutakuwepo na onyesho ya utangulizi la muziki wa disco kwa ajili ya watoto. Alisema onyesho hilo litaanza saa sita mchana na kuhitimishwa saa kumi na moja jioni.
Bendi ya Twanga Pepeta International itawapa burudani ya sikukuu hiyo mashabiki wake siku ya Idd Pili katika onyesho litakalofanyika kwenye ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni, Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Asha Baraka amesema watalitumia onyesho hilo kumtambulisha mwanamuziki wao wa zamani, Ige Moyaba, aliyerejea nchini hivi karibuni kutoka Ufaransa.
Mbali na kumtambulisha mwanamuziki huyo, Asha alisema watalitumia onyesho hilo kuwatambulisha wacheza shoo wapya waliowanasa hivi karibuni kutoka katika vikundi mbalimbali.
Kundi la Mashauzi Classic linaloongozwa na Isha Mashauzi limeamua kukwea basi kwenda Morogoro kuwapa burudani ya kusherehekea sikukuu hiyo mashabiki wake katika kitongoji cha Mji Mpya.
Mashauzi alisema juzi kuwa, siku ya Idd Pili kundi hilo litahamishia burudani zake kwenye ukumbi wa City Pub mjini Mbeya wakati Iddi Tatu litamwaga lazi kwenye ukumbi wa Garden Park ulioko Mafinga mkoani Iringa.
Katika maonyesho hayo, Mashauzi alisema kundi hilo litatambulisha nyimbo zake nne mpya, zinazotarajiwa kuwemo kwenye albamu yao mpya, itakayokuwa na nyimbo sita.
Alizitaja nyimbo hizo, watunzi wakiwa kwenye mabano kuwa ni Asiyekujua hakuthamini (Isha na Saida), Bonge la bwana (Hashim Said), Ropokeni yanayowahusu (Saida) na Ni mapenzi tu (Zubeda Maliki).
No comments:
Post a Comment