KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, August 23, 2013

BANANA ATAKA WASANII WAWE WABUNIFU


MWANAMUZIKI nyota wa muziki wa dansi nchini, Banana Zorro amewataka wasanii wa muziki wa kizazi kipa wawe wabunifu na kwenda na mabadiliko ya wakati.


Banana amesema wasanii wa muziki huo wanapaswa kuboresha kazi zao ili ziweze kuwa katika kiwango cha kimataifa na hivyo kukubalika sehemu mbalimbali duniani.

Kiongozi huyo wa B Band alisema hayo hivi karibuni katika mazungumzo maalumu na gazeti hili yaliyofanyika mjini Dar es Salaam.

Banana alisema binafsi aliamua kujitosa katika muziki wa dansi kutokana na kukua kimuziki na pia kubadili mfumo wa muziki wake.

"Huwezi kutegemea mauzo ya CD kwa miaka yote. Unapaswa kuwa mbunifu zaidi. Inapobidi, unapaswa ujitegemee,"alisema mwanamuziki huyo, ambaye kipaji chake kilianza kuchomoza alipokuwa katika bendi ya In Africa.

Banana alisema msanii anayetumia na kutegemea CD kufanya maonyesho yake, hawezi kupata mafanikio makubwa kimuziki kwa vile kuna wakati anaweza kutakiwa kupiga nyimbo zake laivu, akashindwa.

Kutokana na mfumo mbovu uliopo sasa, Banana alisema mauzo ya CD si mazuri kwa vile baadhi ya watu wamekuwa wakitengeneza CD feki na kuziuza kwa wingi bila ya ridhaa ya wasanii na hivyo kuwafanya waendelee kuwa masikini.

"Ukiweza kupiga muziki laivu, ni rahisi kupata tenda na kupata shoo. Biashara ya kuuza CD kwa sasa ni ngumu,"alisema mwanamuziki huyo, ambaye bendi yake imekuwa ikifanya maonyesho katika hoteli mbalimbali za kitalii mjini Dar es Salaam.

Banana alisema si kweli kwamba maprodyuza wa muziki nchini hawatimizi wajibu wao ipasavyo kutokana na kutengeneza mipigo ya ala isiyokuwa na mvuto. Alisema msanii ndiye mtu wa kwanza, anayepaswa kubuni mipigo ya ala anayoitaka.

Alisema sehemu kubwa ya nyimbo zake zimekuwa zikitengenezwa na prodyuza Allan Mapigo, lakini baada ya kumpa maelekezo ya nini anachokitaka. Alimsifu Mapigo kuwa ni mtaalamu aliyebobea katika fani hiyo na mwenye uwezo wa kumbadili msanii kimuziki.

Licha ya serikali kuanza kutoza kodi kazi za wasanii, Banana alisema bado baadhi ya watu wanaendelea kutengeneza CD feki za nyimbo za wasanii na hivyo kujipatia fedha kwa njia haramu.

"Uamuzi huu wa serikali unaweza kuongeza umakini katika kudhibiti wizi wa kazi za sanaa, lakini wapo watu wanatengeneza CD na kuweka nembo feki za TRA (Mamlaka ya Kodi ya Mapato),"alisema Banana, ambaye ni mtoto wa mwanamuziki mkongwe nchini, Zahir Ally Zorro.

Mwanamuziki huyo ametoa mwito kwa serikali kuiongezea nguvu sheria ya hatimiliki kwa vile inayotumika sasa imeshindwa kudhibiti wizi wa kazi za wasanii kwa vile wahusika wamekuwa wakitozwa faini kidogo.

Amesema ni vyema serikali ishirikiane na wasanii katika kulinda kazi zao na za wasanii wa nje ili iwe rahisi kukabiliana na biashara hiyo haramu, ambayo imekuwa ikiwafaidisha watu wachache na kuwaacha wasanii wakiteseka.

Alisema kuna wakati msanii mmoja kutoka nje ya nchi aliwahi kufika nchini na kukuta kazi zake zinauzwa holela mitaani bila wahusika kuchukuliwa hatua yoyote.

"Ni vyema watu waache kununua CD feki, wanunue CD halali. Naamini wakati utafika udhibiti utakuwa mzuri na CD feki hazitakuwepo kwenye soko la muziki,"alisema Banana.

No comments:

Post a Comment