'
Wednesday, August 7, 2013
'NGASA WA YANGA'
KAMATI ya Usajili ya klabu ya Yanga imesema haina wasiwasi kuhusu usajili wa mshambuliaji, Mrisho Ngasa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Yanga imesema mchezaji huyo ni mali halali ya klabu hiyo kwa vile imefuata taratibu zote muhimu katika kumsajili baada ya kumaliza mkataba wake na klabu yake ya zamani ya Azam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdalla Bin Kleb alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wameshangaa kusikia kuwa, klabu ya Simba imepeleka jina la mchezaji huyo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya usajili wa msimu ujao.
"Tunachotambua ni kwamba, Ngasa aliuzwa kwa mkopo kwa klabu ya Simba na baada ya muda wa mkopo kumalizika, alikuwa mchezaji huru. Isingewezekana kusajiliwa tena na Simba akiwa kwenye mkopo bila ridhaa ya Azam,"alisema.
Yanga imeelezea msimamo wake huo baada ya kuwasilisha jina la mchezaji huyo TFF kama ilivyofanya Simba. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake,
Alex Mgongolwa inatarajiwa kukutana Agosti 13 na 14 mwaka huu kwa ajili ya kupitia na kufanyia uamuzi usajili wa wachezaji wenye matatizo.
Bin Kleb alisema uamuzi wa Simba kuwasilisha jina la Ngasa kwa shirikisho hilo umelenga kuvuruga usajili wa klabu hiyo na kusisitiza kuwa, hawatakubali hilo litokee.
"Kwa hali hiyo, tunahisi viongozi wa Simba wanataka kumkomoa Ngasa baada ya kukataa kuongeza mkataba wa kuichezea. Tunaamini kamati ya usajili itatenda haki katika kuidhinisha usajili wake,"alisema.
Mapema wiki hii, Ngasa alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa, yeye ni mchezaji halali wa Yanga kwa vile alishamaliza muda wa kuichezea Simba kwa mkopo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment