'
Sunday, August 11, 2013
SIMBA YAWAPA RAHA MASHABIKI WAKE, YAITUNGUA VILLA 4-1
SIMBA jana iliwapa raha mashabiki wake baada ya kuitungua SC Villa ya Uganda mabao 4-1 katika mechi ya kirafiki ya kimataifaya soka iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Vijana chipukizi ndio walioichangamsha Simba katika kipindi cha pili hasa baada ya kuingia Abdalla Seseme, Willia, Lucian, Ramadhani Singano. Vijana hao walicheza soka ya kasi, tofauti na kaka zao na kuwafanya wachezaji wa Villa wachanganyikiwe.
Mechi hiyo ilikuwa sehemu ya tamasha la Siku ya Simba, ambalo huandaliwa kila mwaka na uongozi wa klabu hiyo kwa ajili ya kuwatambulisha wachezaji wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao.
Villa ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tisa lililofungwa na Muganda Ronald baada ya kupokea krosi kutoka kwa Sijari Jamal.
Simba ilisawazisha dakika ya 44 kupitia kwa kiungo wake, Jonas Mkude kwa shuti kali baada ya kupokea pasi kutoka kwa Haruna Chanongo. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
William aliiandikia Simba bao la pili dakika ya 53 baada ya kuunganisha wavuni kwa shuti kali krosi kutoka kwa Idrisa Rashid 'Baba Ubaya', aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi.
Bao hilo liliongeza kasi ya Simba, ambayo ilifanikiwa kuongeza bao la tatu dakika ya 70 lililofungwa na Betram Mombeki baada ya shuti la mpira wa adhabu lililopigwa na Nassoro Masoud 'Cholo' kugonga mwamba wa goli na kurudi uwanjani, ambako ulimkuta mfungaji.
Mombeki aliihakikishia Simba ushindi dakika ya 72 baada ya kufunga bao la nne baada ya kupokea pasi nyingine maridhawa kutoka kwa Cholo.
Villa inatarajiwa kushuka tena dimbani leo kukipiga na Yanga kwenye uwanja huo kabla ya kurejea nyumbani kesho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment