KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 1, 2013

OWINO ARIPOTI SIMBA, WARUNDI KUTUA LEO


WAKATI beki mpya wa Simba, Joseph Owino ameshatua nchini, nyota wengine wawili wapya kutoka Burundi wanatarajiwa kuwasili leo kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Owino aliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya na kupokewa na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo.

Katibu Mkuu wa Simba, Evod Mtawala alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Owino alitarajiwa kutia saini mkataba wa kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili.

Kwa mujibu wa Mtawala, wachezaji wengine wawili wapya, mshambuliaji Hamisi Tambwe na beki Gilbert Kazwe kutoka klabu ya Vital'O ya Burundi wanatarajiwa kutua leo kwa ndege ya shirika hilo.

Mtawala alisema wachezaji hao wawili walishatumiwa tiketi za ndege tangu wiki iliyopita na walikuwa wakikamilisha taratibu za kuondoka katika klabu yao kabla ya kuja nchini.

Tambwe amesajiliwa kwa lengo la kuimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo wakati Kazwe na Okwino wamesajiliwa kwa ajili ya kuimarisha safu ya ulinzi, ambazo zilipwaya msimu uliopita.

Owino aliwahi kuichezea Simba kwa mafanikio makubwa msimu wa 2010/2011,lakini aliachwa baada ya kupatwa na maumivu ya goti na kwenda kutibiwa nchini India, ambapo aliporudi, alijiunga na Azam.

Ujio wa Owino, Tambwe na Kizwe utaifanya Simba hadi sasa iwe na wachezaji wanne wa kigeni, akiwemo kipa Abel Dhaira kutoka Uganda, ambaye aliichezea timu hiyo katika ligi kuu msimu uliopita.

Wakati huo huo, kikosi cha Simba kilichoweka kambi kwenye hoteli ya Mbamba Beach iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam kimeimarika baada ya wachezaji Amri Kiemba na Haruna Chanongo kuripoti kambini.

Kiemba na Chanongo walikuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kilichokuwa kikishiriki katika michuano ya Kombe la CHAN na kutolewa na Uganda.
Wachezaji wengine waliokuwemo kwenye kikosi hicho, Mwinyi Kazimoto na Shomari Kapombe wapo nje ya nchi.

Kapombe yuko nchini Uholanzi, ambako anafanyiwa majaribio ya kucheza soka ya kulipwa wakati Kazimoto alitoroka kwenye kambi ya Taifa Stars na kwenda Qatar kucheza soka ya kulipwa.

Katika hatua nyingine, Tamasha la Simba Day lililopangwa kufanyika Agosti 8 mwaka huu sasa litafanyika Agosti 10 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tamasha hilo, linalofanyika kila mwaka, litapambwa kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Simba na SC Villa ya Uganda litakalochezwa kwenye uwanja huo.

Katika tamasha hilo, klabu ya Simba itawatambulisha wachezaji wake wote waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, unaotarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka huu.

Kamati ya Utendaji ya Simba ilitarajiwa kukutana jana jioni kujadili maandalizi ya tamasha hilo pamoja na kupitia majina ya usajili wa wachezaji yaliyowasilishwa na benchi la ufundi, linaloongozwa na Kocha Mkuu, Abdalla Kibadeni.

No comments:

Post a Comment