KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 14, 2013

VIWANJA VYA KIRUMBA, MKWAKWANI, SOKOINE HAVIFAI



WAKATI michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara imepangwa kuanza Agosti 24 mwaka huu, baadhi ya viwanja vitakavyotumika imebainika kuwa ni vibovu na havifai kutumika kwa ligi hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na Burudani wiki hii umebaini kuwa, viwanja hivyo vimebainika kuwa na mapungufu baada ya ukaguzi uliofanywa na maofisa ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, uwanja pekee uliobainika kuwa katika hali nzuri ni Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.

Uchunguzi huo umebaini kuwa, mapungufu yaliyobainika kwenye viwanja hivyo ni pamoja na sehemu za kuchezea, vyumba vya mapumziko kwa wachezaji na vyoo.

Uwanja wa CCM Kirumba ulioko Mwanza umebainika kuwa na kasoro kwenye vyumba vya wachezaji na vyoo na wamiliki wake wametakiwa kuzifanyia marekebisho sehemu hizo kabla ya ligi. 

Uwanja wa Mkwakwani wa Tanga umebainika kuwa na kasoro kwenye vyumba vya wachezaji na waamuzi wakati Uwanja wa Sheikh Amri Abeid wa Arusha umebainika kuwa na vichuguu kwenye baadhi ya maeneo ya kuchezea mpira hivyo unahitaji kufanyiwa ukarabati.

Uchunguzi huo pia umebaini kuwa, Uwanja wa Sokoine wa Mbeya nao una mapungufu katika eneo la kuchezea mpira, Uwanja wa Jamhuri wa Morogoro nyasi zake zimekauka wakati Uwanja wa Kaitaba wa Kagera una kasoro ya vipimo vya urefu wa uwanja na magoli.

Ofisa mmoja wa TFF, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, ameithibitishia Burudani kuwepo kwa mapungufu hayo kwenye viwanja hivyo na kwamba wamewataka wamiliki wake wafanye marekebisho kabla ya kuanza kwa ligi.

"Katika viwanja vyote hivyo, uwanja wa Kaitaba una mapungufu mengi zaidi na tumeiandikia Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kuitaka ifanye marekebisho, vinginevyo hautatumika kwa mechi za ligi,"alisema ofisa huyo.

No comments:

Post a Comment