KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 1, 2013

DOMAYO 'OUT' YANGA


                
KIUNGO wa timu ya soka ya Yanga na Taifa Stars, Frank Domayo atakuwa nje ya dimba kwa kipindi cha wiki mbili kutokana na kupatwa na maumivu ya misuli.

Domayo alipatwa na maumivu hayo wiki iliyopita wakati Taifa Stars iliporudiana na Uganda katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la CHAN.

Daktari wa Yanga, Festo Mwankemwa alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa,
Domayo amegundulika kuwa na tatizo la nyama za misuli kuvia damu katika mguu wa kulia.

Festo alisema kiungo huyo alipatiwa matibabu ya awali wakati akiwa Uganda kabla ya kuendelea kutibiwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kurejea Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mandela mjini Kampala, Taifa Stars ilichapwa mabao 3-1 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-1. Katika mechi ya awali iliyochezwa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars ilichapwa bao 1-0.

Domayo alitolewa dakika tano kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika na nafasi yake kuchukuliwa na Vicent Barnabas.

Wakati huo huo, baadhi ya wachezaji wa Yanga waliokuwa katika kikosi cha Taifa Stars, wamepewa mapumziko ya siku tano na kutakiwa wajiunge na wenzao mwishoni mwa wiki hii.

Wachezaji hao ni  Mrisho Ngasa, Athuman Idd, Nadir Haroub 'Cannavaro',Kelvin Yondan, Saimon Msuva,David Luhende na Ali Mustapha.

No comments:

Post a Comment