KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 28, 2013

ATHUMANI IDDI 'CHUJI': YANGA MWENDO MDUNDO



KIUNGO nyota wa klabu ya Yanga, Athumani Iddi Chuji amesema kikosi cha sasa cha timu hiyo kinatisha kutokana na kukamilika katika kila idara.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Chuji alisema kutokana na kukamilika huko, Yanga ina uwezo mkubwa wa kutetea ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.

"Mwendo wetu msimu huu ni wa ushindi tu, hakuna sare. Hatuna wasiwasi na ubingwa,"alisema kiungo huyo aliyewahi kuichezea Simba.

Chuji ameusifu uongozi wa Yanga kwa kutoa kipaumbele kwa vijana katika usajili wa msimu huu na kuongeza kuwa, watakuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo katika miaka michache ijayo.

Alisema katika mechi yao ya ufunguzi wa ligi dhidi ya Azam, kipa Ally Mustafa 'Barthez' na beki Kevin Yondan waliumia na kushindwa kuendelea na mchezo, lakini vijana walioingia badala yao waliweza kuziba vyema mapengo yao.

"Kusema kweli, timu ina mabadiliko makubwa. Karibu kila namba kuna wachezaji zaidi ya wawili.
Hakuna mapungufu. Yanga ya msimu huu ni bora zaidi kuliko ya msimu uliopita,"alisema.

Kiungo huyo wa Taifa Stars alisema viwango vya baadhi ya wachezaji vimepanda ikilinganishwa na msimu uliopita na alitoa mfano wa Didier Kavumbagu kutoka Burundi, ambaye aling'ara katika mechi dhidi ya Azam na Ashanti.

Chuji alisema pia kuwa kurejea kwa mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Mrisho Ngasa kutaiongezea nguvu zaidi Yanga kutokana na uwezo na uzoefu wake katika ligi na michuano ya kimataifa.

Hata hivyo, Ngasa amezuiwa kucheza mechi sita za ligi hiyo baada ya kubainika kuwa, alitia saini mkataba wa kuichezea Simba kwa mwaka mmoja wakati alipokuwa akiichezea timu hiyo kwa mkopo kutoka Azam.

"Ngasa ni mchezaji mzuri sana. Akicheza pamoja na akina Domayo, Niyonzima, Kavumbagu na Tegete, safu yetu ya ushambuliaji itakuwa tishio,"alisisitiza.

Chuji amemsifu kocha mkuu wa timu hiyo, Ernie Brandts kwa kutoa mafunzo mazuri kwa wachezaji wake na kuongeza kuwa, wamekuwa wakiyafuata vyema ili kuhakikisha wanatangaza ubingwa mapema.

Alisema kocha huyo amekuwa akipendwa na wachezaji, ambao wamekuwa wakifika mazoezini mapema na hakujawahi kutokea mgogoro wowote kati yao.

"Kocha wetu ni mzuri. Kungekuwa na tatizo, nadhani asingeelewana na wachezaji na wangeweza kufanya mgomo, lakini tunakwenda naye vizuri," aliongeza.

Chuji pia alimsifu kocha msaidizi wa timu hiyo, Fred Felix Minziro kwa kuwaweka fiti wachezaji kutokana na kuwapa mazoezi ya kuwajaza stamina kwa saa tatu kila simu.

Licha ya Yanga kuanza ligi hiyo kwa kishindo kwa kuifunga Ashanti mabao 5-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita, Chuji alisema timu hiyo ni nzuri.

"Sidhani kama kuna timu mbaya msimu huu. Hata hao Ashanti tumewafunga kwa sababu ya ugeni wao katika ligi, lakini ni timu nzuri. Nadhani baada ya mechi tatu zijazo watabadilika,"alisema.

Alizitaja timu zinazoweza kutoa upinzani mkali kwa Yanga msimu huu kuwa ni pamoja na watani wao wa jadi, Simba, Azam, Mtibwa Sugar na Coastal Union.

Kwa sasa Chuji ni majeruhi baada ya kuumia kifundo cha mguu katika mechi ya ufunguzi wa ligi hiyo dhidi ya Ashanti. Chuji alishindwa kumaliza mchezo huo na nafasi yake ilichukuliwa na Frank Domayo.

Kiungo huyo kwa sasa amekuwa akifanya mazoezi mepesi na daktari amemshauri aendelee kupumzika ili apone sawasawa kabla ya kuanza mazoezi na wenzake.

Chuji hakuweza kuichezea Yanga katika mechi nyingine ya ligi hiyo dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha iliyochezwa jana mjini Dar es Salaam na huenda akakosa mechi zingine mbili zijazo.

Hata hivyo, Chuji anaamini kuwa atakuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kitakachocheza mechi ya mwisho ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa mwezi ujao mjini Banjui.

No comments:

Post a Comment