Mkurugenzi wa Kampuni za Bakhresa, Said Salim Bakhresa
UONGOZI wa Azam TV umetoa jumla ya sh. milioni 325 kwa klabu 13 kati ya 14 zitakazoshiriki michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu ujao.
Kiasi hicho cha pesa ni malipo ya awali kwa klabu hizo kwa ajili ya kuonyesha mechi za ligi hiyo 'laivu' kupitia Azam TV. Kila klabu imepata mgawo wa sh. milioni 25.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, pesa hizo zimelipwa moja kwa moja na Azam TV kupitia kwenye akaunti za klabu hizo.
"Nimepokea taarifa leo (jana) kutoka Azam TV ikieleza kwamba, wameshazilipa klabu zote 13 za ligi kuu shilingi milioni 25 kila moja, zikiwa ni malipo ya awali kulingana na mkataba kati yetu,"alisema Karia.
Karia alisema klabu ya Yanga haijahusishwa katika malipo hayo kutokana na kutoutambua mkataba huo.
Kwa mujibu wa Karia, hadi jana, uongozi wa Yanga ulikuwa haujawasilisha barua inayoelezea kuhusu uamuzi wake huo zaidi ya kuzisoma taarifa hizo kupitia kwenye vyombo vya habari.
Karia alisema Azam TV imeamua kutoa fedha hizo mapema ili ziweze kuzisaidi timu katika maandalizi ya ligi hiyo, inayotarajiwa kutimua vumbi kuanzia Agosti 24 mwaka huu.
"Azam TV imeamua kutoa malipo hayo kwa njia ya hundi ili kuepuka pesa hizo kutumika kwa matumizi mengine na pia ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa,"alisema.
Karia alisema wameshatoa taarifa kwa viongozi wa klabu zote 13 kuhusu malipo hayo ili ziweze kutumia fedha hizo kwa ajili ya maandalizi ya ligi.
Aliongeza kuwa, iwapo uongozi wa Yanga utaendelea kusisitiza msimamo wake, mechi zake zitakazoonyeshwa laivu na Azam TV ni zile itakazocheza ugenini.
"Kwa sasa bado tunasubiri barua kutoka kwa Yanga, iwapo hawatatoa taarifa ya maandishi, hawatapata mgawo huo na mechi zao zitakazoonyeshwa laivu zitakuwa za ugenini,"alisema.
Azam TV imeingia mkataba wa kuonyesha laivu mechi zote za ligi hiyo kwa kuilipa kila klabu sh. milioni 100. Katika malipo ya awali, kila klabu itapata sh. milioni 25 na fedha zilizobaki zitalipwa baada ya ligi hiyo kumalizika.
Yanga imepinga mkataba huo kwa madai kuwa, haikuhusishwa katika kuupitia na kwamba malipo yanayotolewa na Azam TV ni madogo ikilinganishwa na ukubwa wa klabu hiyo.
Viongozi wa Yanga hawakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hilo kwa vile kila walipopigiwa simu zao za mkononi, hazikupokelewa.
No comments:
Post a Comment