KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 29, 2013

GURUMO: MUZIKI WA KIZAZI KIPYA UNALIPA KULIKO DANSI



MWANAMUZIKI mkongwe wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Muhidin Gurumo, ametangaza kustaafu kazi ya muziki, aliyoifanya kwa miaka 53.

Gurumo (73), alitangaza uamuzi huo Agosti 22, mwaka huu, alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), mjini Dar es Salaam.

Mkongwe huyo wa muziki alisema ameamua kustaafu kutokana na umri wake mkubwa.
Licha ya kujihusisha na muziki katika sehemu kubwa ya maisha yake, Gurumo alisema hana mafanikio makubwa kimaisha, licha ya kujenga nyumba anayoishi na familia yake, iliyoko Ubungo Makuburi, Dar es Salaam.

Katika kipindi alichopiga muziki katika bendi za NUTA, JUWATA, OTTU na Mlimani Park, Gurumo anasema ametunga nyimbo  zaidi ya 200.

Alijiunga na NUTA 1964 akiwa mmoja wa waanzilishi kabla ya kuhamia Mlimani Park 1978 na Orchestra Safari Sound (OSS) kuanzia 1985 hadi 1990.

Gurumo ana kipaji cha kutunga nyimbo zenye ujumbe kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Alikuwa gwiji katika uimbaji na jina la Gurumo halikuwa la utani kwa sababu ya kuimba kwa sauti nzito, bali ni jina lake halisi.

Aliposimama jukwaani kuimba katika bendi za Msondo Ngoma, OSS na Mlimani Park Orchestra, mashabiki waliburudika kutokana na sauti yake nzito, ambayo ilikolezwa na nyingine za Hassan Bitchuka, marehemu Moshi William, Thobias Chidumule, hayati Hamisi Juma na Maxi Bushoke.

Katika wimbo wa Kassim aliouimba akiwa Mlimani Park, Gurumo akishirikiana na Hamisi Juma (sasa marehemu), aliimba na kutoa picha halisi ya mlevi wa pombe aliyeanza kufilisika na kubana matumizi, wakati Hamisi aliimba kama mwanamke, aliyezoea kupewa ofa na Gurumo.

“Na mie moja Kassim,” anaimba Hamisi katika wimbo huo.

“Sina hela ya mchezo,” anajibu Gurumo.

Wimbo mwingine uliompa sifa Gurumo ni Celina aliouimba akiwa na Mlimani Park. Katika wimbo huo, Gurumo anasikika akiimba: ‘Na kwa sababu imekuwa hivyo Celina, sioni haja ya kutaka ujiue kwa ajili yangu”. Wimbo huo ulitungwa na marehemu Joseph Mulenga, aliyekuwa akipiga gitaa la solo.

Akiwa OSS, alipata umaarufu kupitia wimbo wa Chatu mkali. Katika wimbo huo, sauti yake nzito inasikika alipoimba: ‘Natoa onyo kwa yeyote anayemchezea chatu ni hatari, atakuwa asipate lolote la manufaa, na ajali imkute bila ya kutegemea, atakuja adhirika ajute na dunia.

Nyimbo zingine, ambazo zinakumbusha kazi ya Gurumo tangu alipojitosa kwenye fani ya muziki ni ‘Salima’, ‘Bwana Abdul’, ‘Dada Fatuma’, ‘Kulima Hadeka’ (umelima bondeni) na ‘Agweti Chole’ (Mwenzangu Twende) zilizoimbwa kwa lugha ya Kizaramo. Alitunga nyimbo hizo alipokuwa Kilwa Jazz.

Gurumo alizaliwa 1940 katika kijiji cha Masaki, Kisarawe mkoani Pwani. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Sungwi na kumaliza darasa la saba 1956. Pia alipata mafunzo ya dini ya Kiislamu katika madrasa ya kijiji alichokuwa akiishi.

Baada ya kumaliza shule, aliamua kujiunga na bendi ya Kilimanjaro Chacha iliyokuwa na maskani Ilala, Dar es Salaam. Alifanya kazi na bendi hiyo hadi 1961 alipojiunga na Rufiji Jazz pia ya Dar es Salaam.

Alidumu na bendi hiyo hadi 1963 alipojiunga na Kilwa Jazz, iliyokuwa maarufu enzi hizo chini ya uongozi wa marehemu Ahmed Kipande. Bendi hiyo ilikuwa na makundi mawili, Kilwa A na B, Gurumo alikuwa kundi B.

Gurumo hakupendezwa na uamuzi wa marehemu Kipande kumuweka katika kundi B, wakati alijiona ana uwezo mkubwa wa kuimba kuliko baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi A. Hali hiyo ilimfanya ajiunge na NUTA Jazz 1964.

Bendi hiyo ilikuwa ikiundwa na Jumuia ya Wafanyakazi Tanzania na baadaye ilibadili majina na kuitwa JUWATA na OTTU Jazz. Baada ya jumuia hiyo kujitoa katika kuendesha bendi, ilikabidhi vyombo kwa wanamuziki, ambao waliamua kuibadili jina na kuiita Msondo Ngoma.

Akiwa OTTU hadi Msondo Ngoma, alitunga nyimbo nyingi ukiwemo wa ‘Wosia kwa Watoto’.
Gurumo ndiye muasisi wa mitindo ya muziki ya Msondo, akiwa na NUTA, JUWATA na OTTU Jazz, Sikinde akiwa na Mlimani Park na Ndekule akiwa na OSS, ambayo ilizipatia umaarufu mkubwa bendi hizo.

Mitindo hiyo ya muziki ilitokana na majina ya baadhi ya ngoma za kabila la Wazaramo na huchezwa kama ilivyo ngoma ya Vanga.

Tofauti ni kwamba, wachezaji wa ngoma hizo huvaa mavazi ya asili, wakati wale wa muziki wa dansi huvaa mavazi ya kawaida.

Kabla ya uamuzi wa kustaafu muziki, Gurumo alishauriwa na daktari aliyekuwa akimtibu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, kujiweka kando na masuala ya muziki baada ya kuugua ugonjwa wa moyo na kulazwa hospitali mara kadhaa.

Ugonjwa wa moyo hutokana na kupungua damu inayoingia kwenye mishipa ya moyo, ambao haukumpata Gurumo kwa sababu ya kuimba.

“Sijapatwa na ugonjwa huu kwa sababu ya kuimba kwa miaka mingi. Baada ya kupata tiba, madaktari walinishauri nipumzike kwa sababu ya umri kubwa mkubwa, siwezi tena kusimama jukwaani kwa muda mrefu na kuimba,” anasema. Alianza kusumbuliwa na maradhi mwaka 2011.

Gurumo ni mmoja wa wanahisa wa bendi ya Msondo. Wengine ni Saidi Mabela, Saidi Kibiriti (meneja), Ramadhani Zahoro, Abdul Ridhiwani, Roman Mng'ande na Huruka Uvuruge.
Wanamuziki hao wanamiliki kiwango sawa cha hisa na malipo yao kwa mwezi ni makubwa ikilinganishwa na waajiriwa.

Hata hivyo, Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti, hakuwa tayari kutaja viwango vya malipo wanavyolipana.

Kwa Gurumo, muziki wa dansi, ambao wanamuziki hutumia ala mbalimbali, kama vile magitaa, tumba, ngoma, tarumbeta na vinanda katika kuupamba na kuufanya uwe na mvuto wa aina yake, utatoweka iwapo vituo vya redio na televisheni nchini vitaendelea kuacha kupiga nyimbo hizo.

"Ukifungua televisheni yoyote, kuanzia asubuhi hadi jioni, nyimbo zinazopigwa ni za bongo fleva tu. Huwezi kusikia nyimbo za muziki wa dansi. Hii maana yake ni kwamba, vyombo hivi vinaua muziki wetu makusudi," anasema.

Hata hivyo, Gurumo anasema wapo watunzi na waimbaji wengi wazuri wa nyimbo za muziki wa dansi na anavutiwa na Hassan Bitchuka wa Mlimani Park na Hussein Jumbe wa Talent Band.

Mkongwe huyo anasema muziki wa kizazi kipya, ambao hutengenezwa studio kwa kutumia kompyuta, na  kuimbwa katika miondoko mbalimbali kama vile, hip hop, R&B na Zouk, ukichezwa kwa kurukaruka na kujinyonganyonga mwili,  ni mzuri kwa wakati uliopo, hususan kwa vijana.

Hata hivyo, anasema hauwezi kudumu kwa vile wasanii wanatumia zaidi kompyuta kuutengeneza.
Gurumo anasema wasanii wa muziki huo wanapata mafanikio tofauti na zama zao, kwani hivi sasa sheria ya hatimiliki inawalinda.

Anasema muziki umemwezesha kujuana na kufahamiana na watu wengi, wakiwemo viongozi wa serikali. Anatoa mfano wa Rais Jakaya Kikwete, ambaye alikwenda kumjulia hali alipokuwa amelazwa Muhimbili.

Mke wa mwanamuziki huyo, Pili Kitwana, anasema mumewe ana jina kubwa kimuziki, lakini maisha yake ni ya kawaida. Pili na Gurumo walifunga ndoa mwaka 1967 na wana watoto wanne.

Mpiga gita la solo wa Msondo Ngoma, Mabela, anasema Gurumo ameshiriki kuimba nyimbo na pia kutunga zingine, zikiwemo Shaba imelia, Kilimo cha kufa na kupona, Ikiwa kama hunitaki,  Nimuokoe nani, Heko Mwalimu Nyerere na Baba nipeleke kwa mama.

Kwa mujibu wa Mabela, watunzi wa nyimbo nyingi za bendi hiyo walikuwa yeye, marehemu Joseph Lusungu, Khalfan Mabruki na Hassan Bitchuka.

Kwa upande wake, Bitchuka anasema Gurumo alikuwa kiongozi msikivu na alitoa ushauri kwa wanamuziki wenzake.

"Gurumo hakuwa mtu wa kuchezewa. Kama hujui muziki, hawezi kuwa rafiki yako na kama unaujua, atakuwa rafiki yako mkubwa," anasema.

Bitchuka anasema Gurumo alikuwa kiongozi jasiri, asiyeyumba, mwenye msimamo na alitunga nyimbo nyingi, hususan akiwa bendi za Mlimani Park na OSS.

Kiongozi wa bendi ya Extra Bongo, Ally Choki, anasema Gurumo ni mwanamuziki aliyekuwa makini katika kazi yake.

"Kwa mtu wa umri wake, isingekuwa rahisi kupanda jukwaani hadi sasa na kuimba. Ni wa kupigiwa mfano na vijana wanaochipukia kimuziki," anasema.

Anasema alihamasika kurekodi albamu na Gurumo kutokana na kuvutiwa na uwezo wake kimuziki.
Albamu hiyo ina nyimbo sita, tatu zimetungwa na Gurumo na tatu za Choki. Albamu hiyo inajulikana Choki/Gurumo remix.

Nyimbo za Gurumo zilizomo kwenye albamu hiyo ni Nipeleke kwa baba, Ikiwa kama hunitaki na Nimuokoea nani.

No comments:

Post a Comment