KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, August 4, 2013

MSIMAMO WA KLABU 13 ZA LIGI KUU KUHUSU AZAM TV



"KATIKA siku za karibuni, kumekuwapo na mjadala kuhusiana na hatua ya klabu ya
Yanga kupinga udhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania unaotarajiwa kufanywa na Azam
Media.

Tumeona ni vema tukatoa msimamo wetu wa pamoja kuhusiana na hatua hiyo ya
wenzetu kwa lengo la kuweka rekodi sawa.
Tunataraji hatua hii ya vilabu hivi 13 itafunga mjadala huu na tungependa wana
habari, kama mtaamua kuuendeleza, basi muundeleze katika mrengo ambao
wadau, yaani sisi vilabu vinavyoshiriki mashindano hayo, zimeamua kuufuata.

Simba SC

Tunapenda kukumbusha kwamba kwa muda mrefu, kilio cha vilabu vya Ligi Kuu ya
Tanzania vilikuwa ni ukosefu wa wadhamini na kwa bahati nzuri kuna dalili kwamba
Mungu ameanza kukisikia kilio hicho msimu huu.

Kwa faida ya umma, tungependa kutoa takwimu za nchi jirani zinazotuzunguka.
Kenya, kila klabu hupata Sh milioni saba za Kenya (sawa na Sh milioni 125 za
Kitanzania) kwa mwaka –fedha ambazo zimeifanya ligi ya Kenya kuwa na uwiano na
ushindani wa kweli (fedha hizo ni mjumuisho wa gharama za matangazo ya
televisheni na udhamini wa bia ya Tusker).
Tanzania leo tunajivunia kuwazidi Kenya kutokana na udhamini wa Azam ambapo
kwa mwaka huu, kila klabu itapata zaidi ya Sh milioni 170 (Jumla kutoka milioni 100 za
Azam na milioni 70 za Vodacom).
Hatuna sababu ya kutaja viwango vya udhamini kwa nchi nyingine jirani kama
Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia nk kwa vile zote zina udhamini wa chini kuliko
Kenya.
SuperSport, ambao wanaliliwa na baadhi yetu, udhamini wao kwa ligi ya Uganda ni
dola 350,000 ambazo ni pungufu kulinganisha na dola milioni moja zilizotolewa na
Azam Media hapa nchini.

Coastal Union

Ni imani yetu kwamba udhamini huu utaifanya ligi ya Tanzania kuwa bora kuliko zote
za Afrika Mashariki. Hili litasaidia kutengeneza timu bora ya Taifa ya Tanzania.
Tungependa kutoa ufafanuzi wa masuala machache ambayo yaliongelewa na
wenzetu wa Yanga kama sababu za kupinga udhamini huu.

BODI YA TPL
Kwa mujibu wa Katiba za FIFA, CAF na TFF, Haki za Televisheni zipo chini ya FA ya
nchi husika. TFF iliamua kukasimu shughuli ya majadiliano kwa Kamati ya Ligi
ambayo ilishirikisha vilabu vyote 14, ikiwamo Yanga na wawakilishi wake walihudhuria
mchakato mzima hadi mwisho.
Hoja ya Yanga kuwa bodi haina nguvu/Mamlaka kisheria kwa kuwa ni ya mpito
inakosa mashiko kwa sababu kimsingi ni TFF ndiyo iliyoingia mkataba kwa sababu
ndiyo iliyopewa mrejesho na Kamati ya Ligi kwamba mchakato umekwenda
sawasawa.
Hoja ya kuwa Bodi ya TPL iliyoko sasa hivi haina mjumbe hata mmoja aliyeteuliwa
kutoka YANGA. Hili si kweli hata kidogo. Mmoja wa wajumbe wa TPL ni Seif Ahmed
almaarufu Seif Magari; ambaye vyeo vyake ndani ya Yanga vinajulikana.

JKT Ruvu

Kama alikuwa hahudhurii vikao vya TPL, hilo ni suala la Wanayanga wenyewe
kumuhoji kwanini alikuwa hahudhurii hivyo na hivyo kuinyima klabu yake ushiriki katika
mijadala muhimu kwa maslahi ya soka hapa nchini.
Ifahamike pia kwamba TPL haikuhodhi mchakato huu bali ilitoa fursa kwa vilabu
vyote vya Ligi Kuu kushiriki ambapo Yanga ilikuwa ikiwakilishwa na Makamu
Mwenyekiti wake, Clement Sanga na Katibu Mkuu, Lawrance Mwalusako.
Hii maana yake ni kwamba hoja kuwa Yanga haikushirikishwa ni mfu.
Yanga walitumia neno UTARATIBU WA DUNIA NZIMA wakisema eti hakuna mahala
duniani ambapo kampuni yenye klabu inayocheza ligi husika kupewa mkataba wa
udhamini au urushwaji wa matangazo.
Inaonekana Yanga hawakufanya utafiti kwani ligi ya Afrika ya kusini ina timu
inayoitwa Super Sports United na inarushwa na kituo cha TV chaSupersports.
Pia majirani zetu Kenya wana timu inayoitwa Tusker FC huku ligi hiyo ikidhaminiwa na
bia ya Tusker.
Tunawashauri Yanga kuwa ni vema kufanya utafiti kabla ya kuibuka na hoja za
namna hii ili kuepuka kuwapotosha wanachama wao.

Mgambo JKT

Yanga pia katika hoja zao wamepinga utaratibu wa kugawana mapato sawa. Hoja hii
ni ya msingi na majadiliano yetu yalilitazama hili kwa kina lakini tukaona kwa mazingira
ya Tanzania na uchanga wa ligi yenyewe kwa sasa ni heri kugawana sawa ili pesa
kwa usawa ili itoke kwa wakati na kusaidia vilabu kujiendesha. Yanga wanakosea
wanaposema eti wao wanastahili kupewa zaidi kwa sababu ni klabu kubwa na yenye
mashabiki wengi kwa kuwa sababu hii haitumiki sehemu yoyote duniani.
Tuchukulie mfano wa nchi ya England ambako ingawa Liverpool ina washabiki wengi
kuliko Manchester City na Chelsea, imezidiwa kwenye mapato ya televisheni na timu
hizo.
Hii ni sababu kinachoamu mapato mwisho wa siku ni kiasi cha mechi za timu ambazo
zimeonyeshwa na televisheni kwenye msimu husika na nafasi ya timu kwenye
msimamo wa ligi.
Hata hivyo, ikumbukwe kwamba nchini England, malipo haya hufanyika baada ya
msimu kumalizika na hapo ndipo watu hukaa chini na kupigiana hesabu za nini
kilipatikana. Sasa ukitumia mfumo huu, ina maada timu zitalazimika kusubiri ligi iishe ili
kuangalia msimamo ya ligi kisha kugawana mapato. Sote tunajua jinsi timu
zinavyoteseka kwa kukosa nauli, posho, mishahara, pesa za kambi nk.
Kwa mazingira yetu ya Tanzania kwa sasa, mfumo kama huu haufai. Hii ni kwa
sababu timu zinahitaji fedha kuanzia kwenye maandalizi ya mechi ya kwanza na
hazikopesheki fedha kwenye mabenki.

Mtibwa Sugar

Tanzania inachohitaji kwa sasa ni ligi yenye ushindani tofauti na sasa ambapo
ushindani uko kwa timu chache zenye uwezo wa kifedha.
Tukizijengea uwezo timu zote taifa litakuwa na ligi nzuri na hatimaye timu nzuri ya
taifa. Pia itawezesha wadhamini wengi zaidi kuingia kwenye mpira na hivyo timu
nyingi zaidi kufaidika.

Tukifikia huko, tunaweza kukaa chini na kutazama mfumo wa kugawana mapato
utakaokuwa bora zaidi wakati huo.

Mambo ya Kuzingatia.Tangu ligi ianze hapa nchini takribani miaka 50 iliyopita, hakuna
timu iliyowahi kulalamikia mfumo wa kugawana mapato sawa kwa kila mechi ambao
umekuwa ukitumika. Mfano mapato ya mlangoni tumekuwa tukigawana sawa na
Yanga haijawahi kulalamika, Pesa za udhamini wa Vodacom tangia ilipokuwa
ikidhaminiwa na TBL hadi leo hii  tumekuwa tukigawana sawa na Yanga haijawahi
kulalamika kutaka kupata zaidi kwa kuwa eti ina mashabiki wengi, pia hata pesa za
haki ya matangazo ya Televisheni zilizowahi kutolewa huko nyuma nailiyokuwa ikiitwa
GTV, na Star TV kwa nyakati tofauti pesa ziligawiwa sawa kwa kila timu.
Hii ni kwa sababu kikanuni, timu zote zinazoshiriki kwenye ligi ni sawa na zote
zinaweza kuwa bingwa au kushuka daraja.

Kagera Sugar

Ni mdudu gani huyu aliyeingia kwenye soka ya Tanzania na kuanza kuleta siasa za
kubaguana? Baba wa Taifa alipata kutuasa kwamba dhambi ya ubaguzi ni sawa na
kula nyama ya mtu. Ikianza, haitaishia kwenye ligi pekee na itakwenda hadi mahali
tusipotaka.

MGOGORO WA MASLAHI
Yanga imekuwa ikilalamikia uwepo wa kiongozi mwandamizi wa makampuni ya
Bakhresa kwenye bodi ya Ligi na kusema inaleta mgongano wa maslahi.
Sisi vilabu tunaamini kwamba uwepo wa kiongozi huyu ndiyo umesaidia makampuni
yake kuwekeza fedha kwenye mpira. Na mifano ipo hai tukianzia na michuano ya
Vijana ya Uhai Cup, ujenzi wa kituo cha michezo cha Chamazi ambacho kinatumiwa
na timu nyingi za Tanzania.
Na sasa tunafaidika na udhamini huu mnono ambao haujapata kutokea katika
historia ya Tanzania.
Tungependa viongozi wengi zaidi wa makampuni yanayoheshimika hapa nchini
wakijitokeza kuongoza mpira badala ya kuanza kuwapinga.
Kwa mfano, tungependa kuona mkurugenzi wa benki ya CRDB akiwa kiongozi wa
Ashanti, bosi wa Barrick akiongoza Mbeya City na Mkurugenzi wa Tanga Cement
akiongoza Coastal Union.

JKT Oljoro

Hivi ndivyo namna mpira unavyoweza kuvutia wawekezaji. Ndiyo maana tulifurahi
wakati Yusuf Manji, alipoomba uongozi Yanga.
Bado tunataraji kwamba naye atajitosa kuingiza fedha zake kwenye ligi ya Tanzania
(mpira) kama alivyofanya Bakhresa ambaye pamoja na kutumia fedha zake Azam
FC, bado ameamua kusaidia na timu nyingine kwa ujumla.
Tunapenda kumuahidi Yusuf Manji kwamba iwapo naye atataka kudhamini Ligi Kuu
iwe kibiashara au kiufadhili, sisi tutamuunga mkono na hatutajali suala la mgongano
wa maslahi.

UPOTEVU WA MAPATO
Wenzetu Yanga wamedai kwamba kwa kuonyesha mechi kwenye televisheni,
mapato yake ya mlangoni yatapungua.
Hili pia halikufanyiwa utafiti wa kutosha. Katika siku za karibuni, mechi zilizoingiza
mapato makubwa zaidi ya milangoni ni zile ambazo zilionyeshwa Live kwenye
televisheni za ndani na nje ya nchi.

Mifano ni mechi za watani wa jadi msimu uliopita zilizoonyeshwa Live na SuperSport
na mechi za Kombe la Kagame zilizoonyeshwa wakati huo.

Ruvu Shooting

Hata mechi ya Taifa Stars na Ivory Coast iliyoonyeshwa Live pia, ilijaza uwanja.
Ulaya ambako karibu kila familia inamiliki televisheni na umeme wa uhakika, bado
watu wanajaa katika viwanja vya soka.
Mpira kuonyeshwa kwenye televisheni unaufanya utangazike zaidi na watu watake
kuona. Kuna faida nyingi za mpira kuonyeshwa kwenye televisheni kuliko hasara
moja ya kufikirika ambayo Yanga wanaiona.
Ingekuwa vema iwapo Yanga wangetoa takwimu za kuonyesha ni kwa namna gani
mechi kuonyeshwa kwenye televisheni kuliwahi kupunguza mapato ya milangoni.
Kwa faida ya umma, mpira kuwa kwenye televisheni kuna faida zifuatazo; jezi
kuongezeka thamani na hivyo kuvutia makampuni makubwa kutaka kudhamini klabu
wakitumia fursa ya kutangaza bidhaa zao, matangazo ya viwanjani (touchline fence)
kuwa na thamani zaidi ambapo kwa sasa vilabu havipati chochote, kuchochea
michezo ya kubahatisha, kutabiri matokeo na kupata habari kupitia simu za mkononi
na hivyo vilabu vitaanza kutengeneza fedha za kutosha.

Azam FC

Ulaya wamesonga mbele kutokana na televisheni. Anayekataa mpira kuonyeshwa
kwenye televisheni ni sawa na mtu anayegoma kutumia mfumo wa digitali katika
ulimwengu wa leo.

UWAZI KWENYE MCHAKATO WA KUUZWA KWA HAKI ZA MATANGAZO
Yanga wameandika kwenye taarifa yao rasmi eti hakukuwa na uwazi kwenye
mchakato wa kuipata kampuni ya kurusha matangazo ya Televisheni.
Sote tunajua kuwa vituo vya televisheni vilivyopo nchini kama Star TV ambayo iliwahi
kurusha mechi kadhaa msimu uliopita vilikuwa vikijua kuwa kuna nafasi hiyo na TFF
mara kadhaa wamekuwa wakitangaza hilo kupitia idara ya Habari ya TFF.
TFF kwa mfano walikwenda mbali kwa kuialika Supersports kuja kuonesha mechi
bure kwa kilichokuwa kikiitwa Super Week ili kuwashawishi waje kuwekeza na mara ya
mwisho ni Yanga hawa hawa walioongoza harakati za kuikataa Supersports kuonesha
mechi bure wakisema kuwa kama ni kuwavutia inatosha.
Katika mazingira kama haya tunastaajabishwa na ukigeugeu wa Yanga leo kusema
eti tenda haikuwekwa wazi. Sote tunajua kuwa ni Super Sports pekee tuliokuwa
tukiwategemea na kuwashawishi ambao hawakuonesha kuhitaji kuja kuwekeza. Kwa
nini leo tuikatae Azam TV?
Yanga wanaposema eti TFF/Kamati ya Ligi imeipa haki za matangazo kampuni
ambayo haina ofisi wala kituo cha televisheni kilicho hewani kwa sasa wanasahau
kuwa huko nyuma TFF iliwahi kuwapa haki za matangazo GTV ambao hawakuwa na
ofisi wala kituo cha TV na baada ya miezi michache walifungua ofisi zao na kuleta
vingamuzi na kuaza kurusha mechi zetu. Vilabu vilifaidi udhamini ule kabla ya ile
kampuni kufilisika. Kwa hiyo hii si mara ya kwanza kwa jambo hili kufanyika na kama
Azam TV hawataonesha mechi za ligi hiyo sisi kama vilabu haituhusu kwani ni hasara
yao.

Tunachowaomba Azam Media sisi kama vilabu ni kuhakikisha wanatulipa pesa zetu
kwa haraka ili zitusaidie kwenye maandalizi,Tunawaomba Yanga wasichafue hali ya
hewa kwa kuwa wao hawana shida ya Pesa.

Mwenyekiti wa Simba SC, Mbunge Alhaj Ismail Aden Rage kushoto akipeana mkono
na Mkurugenzi wa Azam TV, Abubakar Bakhresa baada ya kusaini Mkataba wa
kipindi maalum cha klabu hiyo katika kituo hicho kipya cha Televisheni mwezi uliopita 

Sisi Umoja wa Vilabu 13 vinavyoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania tunapinga, kwa nguvu
zote, madai ya Yanga kwamba hatukushirikishwa kama vilabu kwenye mchakato
huu.
Mfumo wa ugawanyaji wa mapato tuliouchagua, tuliuchagua wenyewe bila
kushurutishwa na yeyote na tunadhani ndiyo mfumo unaotufaa kwa sasa hadi hapo
ligi yetu itakapokuwa na nguvu maana kwa sasa inaruhusiwa klabu kupata fedha
mwanzoni kulingana na hali halisi ya vilabu vyetu.
Tunawashauri wenzetu wa Yanga waanze kuamini kwenye kitu kinachoitwa
Uwajibikaji wa Pamoja (Collective Responsibility). Mambo yanayoamuliwa kwenye
vikao hayapaswi kupingwa nje ya vikao.

Kama hoja ililetwa kwenye vikao na ikazidiwa nguvu na hoja nyingine, hakuna sababu
ya kuikataa kwa sababu tu hukubaliani nayo. Mfumo wa kidemokrasia una kanuni
moja kuu; Wengi Wape,"

Imetolewa na
Vilabu 13 vya Ligi Kuu ya Tanzania
Simba SC, Azam FC, Ashanti United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting Stars, Mgambo JKT,

JKT Oljoro, Rhino Rangers, Mbeya City, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Coastal
Union na Kagera Sugar.

No comments:

Post a Comment