KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 29, 2013

BONGO FLEVA ALMASI INAYONG'ARISHA VIJANA



MUZIKI wa kizazi kipya upo juu ikilinganishwa na muziki wa dansi, kutokana na idadi ya mashabiki wanaohudhuria maonyesho ya muziki huo.

Si hilo tu, hata maisha ya wasanii wa muziki huo ni ya juu ikilinganishwa na ya wa muziki wa dansi.
Utofauti huo unatokana na malipo ya fedha nyingi wanayolipwa kwa kuuza albamu au kufanya onyesho.

Muziki wa kizazi kipya, hutengenezwa studio kwa kutumia kompyuta, hupigwa na kuimbwa katika miondoko mbalimbali kama vile, hip hop, R&B na Zouk na unapendwa zaidi na vijana.  Uliingia nchini miaka ya mwanzoni mwa 1990 muasisi akiwa Saleh Jabir, ambaye kwa sasa anaishi nje ya nchi.

Wasanii wengi wa muziki huo wanamiliki magari ya kifahari, yakiwemo Toyota Land Cruiser, yenye thamani ya mamilioni ya shilingi na wengine wamemudu kujenga nyumba bora za kuishi, ambazo zimejengwa kwa matofali na wengine kuezeka kwa vigae.

Kutokana na malipo ya fedha nyingi wanayolipwa, baadhi wanaishi maisha ya anasa, ya kustarehe kwenye hoteli zenye hadhi ya juu, kama vile Serena au kutembelea kumbi maarufu za burudani kama vile Billicanas na Maisha Club, zilizoko Dar es Salaam.

Wapo wasanii wanaolipwa kati ya sh. milioni moja na sh. milioni 10 kwa onyesho moja, wakati bendi za muziki wa dansi zenye idadi kubwa ya wanamuziki, zinakodiwa kwa kati ya sh. 400,000 na sh. milioni moja kwa onyesho.

Muziki wa dansi, wanamuziki wake hutumia ala mbalimbali, kama vile magitaa, tumba, ngoma, tarumbeta na vinanda katika kuupamba na kuufanya uwe na mvuto wa aina yake. Ni tofauti na bongo fleva.

Zipo baadhi ya bendi ambazo kutokana na kukosa mashabiki, zinalazimika kufanya maonyesho bure kwa mashabiki, kwa kuingia makubaliano maalumu na wamiliki wa kumbi za burudani.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, bendi hulipwa kati ya sh. 50,000 na sh. 200,000 kwa onyesho moja, huku mmiliki wa baa akiongeza bei kwa kila kinywaji ili kufidia malipo anayotoa kwa bendi husika. Utaratibu huu  umelenga kuwaongezea mapato wamiliki wa baa.

Wasanii chipukizi katika muziki wa kizazi kipya, hulipwa kati ya sh. 100,000 na sh. 300,000. Malipo hayo bado ni makubwa ikilinganishwa na yale ya bendi za muziki wa dansi.

Si hilo tu, wanamuziki wa taarab, ambao ni maarufu kwa mashairi na mipigo ya kinanda, waimbaji wakijimwaya kwa kutikisa miili yao, pia wanalipwa kiasi kikubwa cha fedha ikilinganishwa na wale wa muziki wa dansi.

Baadhi ya vikundi maarufu vya muziki wa taarab, kama vile Jahazi vimekuwa vikilipwa kati ya sh. milioni moja na sh. milioni 1.5 kwa onyesho moja, wakati vikundi vinavyochipukia hulipwa kati ya sh. 600,000 na sh. 800,000.

Msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' ndiye anayeongoza kwa kulipwa fedha nyingi kwa kila onyesho. Msanii huyo amekuwa akilipwa dola za Marekani 10,000 (sh. milioni 16) anapofanya onyesho nje ya nchi.

Diamond anasema katika baadhi ya nchi, kiwango cha malipo kwa kila onyesho ni kati ya dola 15,000 (sh. milioni 24) na 25,000 (sh. milioni 42).

"Sifanyi shoo nje ya nchi chini ya dola 10,000. Katika nchi kama vile Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), kiwango changu ni dola 25,000. Wakati mwingine nalipwa hadi dola 30,000," anasema.

Diamond anasema kwa nchi kama vile Comoro, ambako alikwenda kufanya onyesho hivi karibuni, malipo kwa onyesho yalikuwa dola 25,000 (sh. milioni 42).

Hata hivyo, Diamond anasema wakati mwingine amekuwa akilipwa zaidi ya anavyotarajia, akitoa mfano wa Rwanda, ambako promota aliyemwalika alimlipa sh. milioni 180.

"Nina msimamo, ninapoalikwa nje ni lazima nifuatane na wacheza shoo wangu," anasema.
Diamond amezaliwa 1986 mkoani Dar es Salaam. Amesoma katika Shule ya Msingi Olympio na sekondari ya Loyola. Amehitimu kidato cha sita 2006.

Kabla ya kujitosa katika muziki, Diamond anasema aliwahi kufanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza mikoba kilichoko Mikocheni, Dar es Salaam kati ya 2008 na 2009 na kulipwa mshahara wa sh. 2,000 kwa saa nane.

Anasema mshahara huo ulikuwa mdogo, haukuweza kukidhi mahitaji yake ya kila siku kwa sababu alikuwa akitumia sh. 1,000 kwa nauli na sh. 1,000 kwa ajili ya chakula.

Licha ya malipo makubwa ya fedha katika maonyesho yake nje na ndani ya nchi, Diamond anasema hajawahi kulipa kodi kwa kuwa hakuna utaratibu wa kuwawezesha wasanii kulipa kodi.

Anasema anatarajia kuanza kulipa kodi kutokana na mauzo ya albamu baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuamua kuweka stempu kwenye kila kazi ya msanii.

Diamond anasema ana vitega uchumi ambavyo ni hoteli, nyumba, viwanja, magari na pikipiki anazozitumia kwa biashara. Anasema mali hizo zina thamani ya sh. bilioni moja.

Mratibu wa maonyesho katika ukumbi wa Dar Live, ulioko Mbagala, Dar es Salaam, Luqman Maloto, anasema wasanii wa muziki wa kizazi kipya ndio wanaoongoza kwa kupata idadi kubwa ya mashabiki kila wanapofanya maonyesho kwenye ukumbi huo.

Hata hivyo, Luqman anasema wingi wa mashabiki unategemea umaarufu wa wasanii husika na aina ya maonyesho yanayoandaliwa.

Amewataja wasanii wenye idadi kubwa ya mashabiki kuwa, Naseeb Abdul 'Diamond', Ally Kiba, Joseph Haule 'Profesa Jay', Ommy Dimples na kundi la TMK Wanaume Family linalopiga muziki wa kizazi kipya

"Kuna wakati tuliwahi kuandaa maonyesho ya usiku wa hip hop, usiku wa Sugu na old is gold ya bongo fleva, tulipata idadi kubwa ya mashabiki kuliko maonyesho mengine kama vile ya muziki wa dansi na taarab," anasema.

Usiku wa hip hop ni onyesho lililowahusisha wasanii wa muziki wa kizazi kipya wanaopiga aina hiyo ya muziki, usiku wa sugu ni onyesho lililomuhusisha msanii Joseph Mbilinyi, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Sugu (kwa sasa ni mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na old is gold ya bongo fleva ni onyesho lililohusisha nyimbo za zamani za muziki wa kizazi kipya.

Maloto anasema bendi za muziki wa dansi hazina mashabiki wengi katika ukumbi huo. Anasema wamewahi kuandaa maonyesho ya bendi kama vile Extra Bongo, Mashujaa, Twanga Pepeta na FM Academia, lakini idadi ya mashabiki haikuwa kubwa.

Anasema hilo linatokana na mashabiki wengi wanaofika kwenye ukumbi huo ulioko Mbagala Zakhem, wilayani Temeke, Dar es Salaam, kuwa vijana, ambao wanaushabikia zaidi muziki wa kizazi kipya.

Mratibu huyo anasema vikundi vya muziki wa taarab vinashika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya mashabiki, hususan kikundi cha Jahazi, ambacho hakijawahi kupata mashabiki wachache.

"Kuna wakati tuliwahi kuandaa onyesho la Mitikisiko ya Pwani, ambalo lilivihusisha vikundi vingi vya taarab. Onyesho hili lilivunja rekodi ya wingi wa mashabiki," anasema.

Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel, Jackson Mmbando, anasema wamekuwa wakiwatumia wasanii wa aina zote katika kutangaza bidhaa zao kwa kuzingatia mazingira ya maeneo husika.

Hata hivyo, Mmbando anasema wamekuwa wakiwatumia zaidi wasanii wa muziki wa kizazi kipya, kwa kuwa wana mashabiki wengi.

"Hatubagui tunapofanya maonyesho kutangaza bidhaa zetu, tunawatumia wasanii wa aina zote, iwe muziki wa kizazi kipya au bendi za muziki wa dansi, lakini hilo linazingatia sehemu tunakofanya maonyesho hayo na watu wanapenda nini," anasema.

Mmbando anasema mara nyingi wamekuwa wakifanya utafiti wa maeneo wanakokwenda kufanya maonyesho ili kujua wakazi wa maeneo hayo wanataka nini.

Meneja wa hoteli ya Koyanga, iliyoko Kiwalani, Dar es Salaam, Twaha Mohamed, anasema vikundi vya taarabu ndivyo vinavyoongoza kwa kupata mashabiki kila vinapofanya maonyesho kwenye hoteli hiyo.

No comments:

Post a Comment