KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, August 12, 2013

YANGA KAMA SIMBA, YAIPIGA SC VILLA 4-1




MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga jana walifuata nyayo za watani wao wa jadi Simba baada ya kuitungua SC Villa ya Uganda mabao 4-1 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kipigo hicho kilikuwa cha pili kwa SC Villa katika muda wa siku mbili. Katika mechi yake ya kwanza ya kusherehekea tamasha la Siku ya Simba, SC Villa ilichapwa mabao 4-1 na Simba.

Yanga ilitumia mechi hiyo kwa ajili ya maandalizi ya pambano lake la kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Azam linalotarajiwa kuchezwa Agosti 17 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.

Wapinzani wao Azam wapo nchini Afrika Kusini, ambako wameweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo na pia kucheza mechi kadhaa za kirafiki za kujipima nguvu.

Katika mechi hiyo, Yanga iliwapa raha na furaha mashabiki wake baada ya kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-1.

Mabao hayo yalifungwa na Mrisho Ngasa, Nadir Haroub 'Cannavaro' na Didier Kavumbagu. Bao la nne lilifungwa na Haruna Niyonzima.Bao la kufutia machozi la Villa lilifungwa na Moses Ndaula dakika ya 18.
  
Kikosi cha Yanga kilikuwa Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, David Luhende/Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan/Rajab Zahir, Athumani Iddi ‘Chuji’/Bakari Masoud, Mrisho Ngassa, Salum Telela, Didier Kavumbangu, Jerry Tegete/Hussein Javu na Haruna Niyonzima/Said Bahanuzi.

No comments:

Post a Comment