KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 15, 2013

TFF KUCHAGUA RAIS OKTOBA 20


KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetangaza kuwa, uchaguzi mkuu shirikisho hilo utafanyika Oktoba 20, mwaka huu Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamid Mbwezeleni alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, nafasi zitakazogombewa ni ya rais, makamu wa rais na wajumbe 13 wa kamati ya utendaji.

Mbwelezeni alisema uchaguzi huo umesogezwa mbele kutokana na kufanyika kwa marekebisho ya katiba ya TFF yaliyofanyika hivi karibuni. Awali, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu.

Mwenyekiti huyo alisema pia kuwa, uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL) umepangwa kufanyika Oktoba 18 mwaka huu. Alizitaja nafasi zitakazogombewa katika uchaguzi huo kuwa ni ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti.

Kwa mujibu wa Mbwelezeni, fomu kwa wagombea zitatolewa kuanzia kesho asubuhi hadi saa 10 jioni kwenye ofisi za TFF na kuongeza kuwa, mwisho wa kuchukua na kurudisha Agosti 20 mwaka huu.

Alisema fomu kwa nafasi ya rais ni sh. 500,000, makamu wa rais sh. 300,000 wakati wajumbe wa kamati ya utendaji sh. 200,000.

Mbwelezeni alisema fomu kwa ajili ya uchaguzi wa bodi ya ligi nazo zitaanza kutolewa kesho hadi Agosti 20 mwaka hii. Alisema ada ya fomu kwa nafasi ya mwenyekiti na makamu wake ni sh 200,000 wakati wajumbe ni sh. 100,000.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya uchaguzi alisema, wagombea wa awali, ambao walilipia fomu katika uchaguzi uliofutwa na wanaokusudia kugombea nafasi zilezile, hawatalia tena ada.

Alisema wagombea hao watatakiwa kuambatanisha risiti za malipo wakati wa kurudisha fomu za maombi hayo ili kuthibitisha malipo hayo.

Mbwelezeni alisema Agosti 27 hadi 29 mwaka huu kitakuwa kipindi cha pingamizi kwa wagombea kabla ya majina yao kutangazwa Agosti 30 mwaka huu. Alisema baada ya majina hayo kutangazwa, yatapelekwa kwa Kamati ya Maadili kwa ajili ya kujadiliwa.

Kamati hiyo inatarajiwa kutangaza majina ya wagombea watakaopitishwa Septemba 7 hadi 13 mwaka huu wakati Septemba 14 hadi 17, wagombea wataruhusiwa kukata rufani iwapo hawataridhika na maamuzi ya kamati hiyo.

Septemba 25 hadi 27, kamati ya rufani itatoa maamuzi ya wagombea waliokata rufani wakati kampeni zimepangwa kuanza Oktoba 6 hadi 17 mwaka huu.

Wakati huo huo, kamati ya Mbwelezeni imetoa onyo kali kwa wagombea watakaowasilisha vyeti vya kughushi kwa ajili ya uchaguzi huo.

Mbwelezeni alitoa onyo hilo jana baada ya kamati yake kubaini kuwa, asilimia kubwa ya wagombea katika uchaguzi uliofutwa mwaka jana, waliwasilisha vyeti vya kughushi.

No comments:

Post a Comment