KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 7, 2013

JOKATE MWEGELO: SIJAWAHI KUTOA MWILI WANGU ILI NISAIDIWE


MREMBO namba mbili wa Tanzania wa mwaka 2006, Jokate Mwegelo amesema kamwe hajawahi kutoa mwili wake kwa mwanaume yeyote ili aweze kufanikiwa katika shughuli zake.

Jokate amesema siku zote amekuwa akipambana kwa nguvu na uwezo wake katika kukabiliana na changamoto zote alizowahi kukumbana nazo katika maisha yake tangu aliposhiriki kuwania taji la Miss Tanzania.

Mmiliki huyo wa Kampuni ya Kutengeneza Nywele ya Kidoti, alisema hayo wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa.

"Sijawahi kutoa mwili wangu ili nisaidiwe. Haijawahi kutokea na haitatokea,"alisema Jokate, ambaye pia ni mcheza filamu, mbunifu wa mavazi, mshereheshaji na mwandaaji wa vipindi vya televisheni.

Jokate amesema licha ya ukweli kwamba wanawake wamekuwa wakipata sapoti kubwa ya kuwawezesha kupata mafanikio kutoka kwa wanaume, si jambo zuri kwao kujirahisisha.

"Siyo kila mtu mwenye kipaji ni rahisi kupata mafanikio kwa sababu ya kuwepo kwa sapoti kubwa kutoka kwa wanaume. Wakati mwingine ni vigumu na inategemea utaratibu, ambao mwanamke amejiwekea,"alisema.

Mrembo huyo amekiri kuwa, wanaume wengi wanaojaribu kumtongoza ni wale wenye uwezo kifedha na walio 'sopusopu' ni hiyo ni kutokana na mwonekano wake.

Jokate alisema hachukii kuitwa Kidoti kutokana na chunusi ndogo nyeusi iliyopo juu ya mdomo wake upande wa kulia kwa sababu kwa sasa imekuwa ndiyo alama ya utambulisho wake.

"Sikuwa nacho nilipozaliwa, kilijitokeza baadaye, lakini sikumbuki lini,"alisema mwanadada huyo, ambaye aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki nyota wa bongo fleva, Naseeb Abdul 'Diamond'.

Jokate alisema yeye ni mwanamke tofauti na wanawake wengine wa umri wake kwa sababu anapenda kujiamini, kuwajibika na kujitahidi aweze kujitegemea katika kuendesha maisha yake.

Amekiri kuwa, tangu alipoanza kujitosa kwenye fani ya urembo, muziki na kucheza filamu, amekumbana na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa familia yake, lakini aliweza kukabiliana nazo na kusonga mbele.

"Bila kupata changamoto katika maisha na kupambana nazo, huwezi kufanikiwa,"alisema mrembo huyo, ambaye pia inadaiwa kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na msanii Izzo Bizness, japokuwa amekuwa akikanusha.

Licha ya kufanya biashara ya kuuza nywele bandia, Jokate alisema hapendelei sana kutumia nywele hizo kwa sababu nywele zake ni nzuri na anaweza kuzitengeneza katika mtindo wowote.

"Baadhi ya siku huwa navaa nywele ninazozitengeneza, lakini napenda kuwa na za kwangu kwa vile naweza kuzitengeneza kwa mtindo wowote,"alisema.

Jokate anasema aliamua kuanzisha biashara ya kutengeneza na kuuza nywele bandia baada ya kugundua kwamba zinapendwa sana na wanawake, hasa katika kujiremba na kuwafanya wawe na mvuto.

Mrembo huyo amekiri kuwa, tangu alipoanza kujihusisha na fani tofauti za sanaa, wapo wanawake wenzake wanaomkubali, lakini wengine wamekuwa wakimkatisha tamaa. Hata hivyo, alisema hawezi kuisumbua akili yake kwa wale wasiomkubali.

"Wivu wangu mimi ni wa kimaendeleo. Nikiona mwanamke mwenzangu fulani yuko hivi, na mimi natamani kuwa kama yeye,"alisema.

Jokate ni mpenzi wa kusoma vitabu vya aina mbalimbali na anasema huo ni utamaduni aliourithi kutoka kwa mama yake, ambaye ni mtunzi wa vitabu.

Akizungumzia wimbi la baadhi ya wasanii kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, Jokate alisema linatokana na tamaa ya kutaka wafike mbali na kufanikiwa haraka katika maisha.

Hivi karibuni, Jokate alianzisha programu iitwayo Kidotitime kwa lengo la kusaidia wanafunzi kutambua na kukuza vipaji vyao wakiwa shuleni. Programu hiyo itaingizwa katika shule zaidi ya 27 mkoani Ruvuma.

Mwanadada huyo anatarajia kuandika kitabu kitakachoelezea mambo mbalimbali kuhusu maisha yake. Hata hivyo, hajasema ni lini kitabu hicho kitakamilika na kuanza kuuzwa madukani.

Joketi alizaliwa Washington DC nchini Marekani mwaka 1987, ambako wazazi wake walikuwa wakifanyakazi. Alisema shule ya msingi ya Olympio  ya mjini Dar es Salaam na baadaye sekondari ya St.Anthony na Loyola kabla ya kuchukua shahada ya sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment